Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka mitatu baada ya CDA, wakazi Dodoma walala usingizi

Rais John Magufuli Mei, 2017 alitangaza kuvunjwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) kutokana na kero mbalimbali zilizokuwa zikilalamikiwa na wananchi miongoni ikiwa ni kuvunjwa kwa nyumba za makazi. Uamuzi huo ulipokewa kwa shangwe na wananchi ambao hivi sasa wanasema angalau wanalala usingizi kwa kuwa hakuna tena hofu ya bomoabomoa.

CDA ilikuwa na migogoro mingi kati yake na wananchi iliyosababisha watu kuchukuliwa viwanja na kuvunjiwa makazi yao bila kulipwa fidia.

Migogoro hiyo iliambatana na uchache wa viwanja vilivyopimwa na wakati mwingine kuliwafanya baadhi ya watu kulala kwenye ofisi za mamlaka hiyo ili kuwahi foleni ya kupatiwa viwanja.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi migogoro ya ardhi 1,563 kati ya 1,631 ambayo ni (sawa na asilimia 96) imetatuliwa tangu halmashauri ya Jiji la Dodoma ikabidhiwe majukumu na CDA.

Wakizungumza na Mwananchi ikiwa ni miaka mitatu baada ya kuvunjwa kwa mamlaka hiyo, wanasema wanalala usingizi kwa kuwa ile hofu ya kuvunjiwa nyumba zao haipo tena.

Hofu ya watu kuvunjiwa nyumba zao ilikuwa ikitokana na sheria ambayo walipewa Mamlaka hiyo kwamba eneo lote la wilaya ya Dodoma Mjini walimilikishwa wao kwa kipindi cha miaka 99, lakini wao waliendelea kuuza viwanja na kuwamilikisha watu kwa miaka 33.

Tangu mwaka 1973 ilipotamkwa Dodoma kuwa makao makuu, watu waliojenga hata nje ya mji lakini akiwa ndani ya wilaya hiyo ilikuwa lazima wawe na vibali vya CDA na kwa ujenzi ilikuwa ni ngumu kuvipata kwa madai kuwa hadi eneo hilo lipimwe na waliojenga walibomolewa.

Mitaa ya Njedengwa, Mtube, Bochela, Kikuyu na Chadulu ni miongoni mwa iliyoathirika zaidi na mamlaka hiyo, kwa sababu walikuwa wakibomolewa kila wakati licha ya wakazi wake kuwa wa asili hata kabla ya uwapo wa CDA.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, mkazi wa Mtaa wa Msangalalee, Margareth Mwanjila anasema hivi sasa hawana hofu ya kubomolewa nyumba zao kama ilivyokuwa kabla ya kuvunjwa kwa CDA.

Mwanjila anasema kipindi cha utawala wa CDA kila siku walikuwa wanatishiwa kubomolewa nyumba zao kwa sababu hawakuwa na hati miliki ya ardhi wanayoishi.

“Lakini tangu mamlaka hiyo ivunjwe, hali imekuwa shwari na watu wameanza kufanya shughuli za kimaendeleo kwenye ardhi wanayoimiliki tangu enzi za mababu licha ya kuwa haikuwa na hati,” anasema.

Mkazi wa Jiji la Dodoma, Innocent Chuwa anasema wakati wa CDA kulikuwa na ugumu mkubwa katika upatikanaji wa viwanja kutokana na baadhi ya watu kuhodhi na kuviuza kwa wengine.

Anasema baada ya kukabidhiwa jiji, viwanja unapata kwa ukubwa wowote unaotaka bila kumfahamu wala kupitia kwa mtu, jambo ambalo limewafanya watu kutogombana tena.

Diwani wa Viwandani (CCM), Jaffar Mwanyemba ambaye alikuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, anasema matatizo hayawezi kuisha kwa sababu ya ardhi.

Anasema jambo kubwa lililofanyika ni kupimwa kwa viwanja vingi kuliko ilivyokuwapo kipindi cha CDA na matokeo yanajionyesha kwa mapato ya jiji kuongezeka.

Mwaka wa fedha 2018/19 jiji lilipima viwanja 65,706 katika maeneo ya Michese, Mtumba, Kikombo, Nzuguni Chahwa, Iyumbu na Nala.

Mwaka 2017/2018 Jiji la Dodoma liliongoza kwa makusanyo, lilikusanya Sh25.05 bilioni kati ya Sh19.32 bilioni sawa na asilimia 130 ya lengo lake.

Mauzo ya viwanja yalilipatia jiji hilo Sh13 bilioni na Sh12 bilioni ni vyanzo vingine vya mapato.

Mwanyemba anasema sasa hivi mambo yamebadilika kabla ya kubomoa nyumba za watu na kwamba, matukio hayo si mengi kama kipindi cha ilipokuwapo CDA.

Hata hivyo, anasema kuna haja ya kufanyiwa kazi kwa suala la nidhamu kwa kuhakikisha watumishi hasa wa ardhi wanatekeleza kazi zao kwa uadilifu. “Sisemi kuwa si waadilifu hawa, lakini ni vyema tukahakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa uadilifu kwa kudhibiti rushwa,” anasema Mwanyemba.

Anasema vyombo vyote zikiwano halmashauri, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waangalie kwa umakini ili kuepuka kuja kutafuta majibu madhara yakishatokea.

Hata hivyo, Diwani wa Nzunguni, Aloyce Luheja anasema ardhi bado ni changamoto kubwa na kwamba, jiji bado halijaweza kuzitatua.

Anasema ingawa kumekuwa na upimaji wa fujo wa viwanja, lakini hakuna mitaro ya kutiririshia maji iliyojengwa kwenye barabara ingawa wakati wa upimaji wananchi wamekuwa wakitoa asilimia 16 ya eneo lao.

“Asilimia 75 ya maeneo ya Nzuguni tumekuwa tukifanya urasimishaji. Maana ya urasimishaji kwenye maeneo holela maana yake ni wananchi wawe na makazi mazuri lakini bado kuna changamoto katika kata yangu,” anasema Luheja.

Anasema Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, (Nemc) linaruhusu watu kujenga mita 60 kutoka kwenye makorongo ama mabwawa lakini hali imekuwa tofauti.

Anasema katika baadhi ya maeneo yaliyorasimishwa kuna nyumba zimejengwa kwenye viwanja vinavyopitiwa na mkondo wa maji na wakati wa mvua, maji hujaa katika maeneo yao.

Anasema maji yanayotoka sehemu mbalimbali Jijini Dodoma yanapita Nzuguni na hivyo, kutoweka mitaro kunasababisha kujaa kwenye maeneo hayo.

Anasema wana shida ya kupeleka maji katika baadhi ya maeneo, hali inayowalazimu Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (Duwasa) kuzungumzia jambo hilo.

Anasema katika maeneo hayo kuna watu wanamalalako halali ambayo yanapaswa kushughulikiwa lakini yapo ambayo hayana uhalali.

Ofisa Uhusiano wa Jiji la Dodoma, Denis Gondwe anasema diwani ni mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata, hivyo anajua mahali pa kuwasilisha matatizo ya wapiga kura wake.

“Barabara zipo chini ya Tarura, waulizwe hao ndiyo wanaohusika na hizo barabara sisi hatuwezi kulisemea jambo hilo,” anasema Gondwe.

Alipotafutwa Mhandisi wa Wilaya wa Tarura jijini Dodoma, Geofrey Mkinga anasema changamoto iliyopo katika kata hiyo ni kukosekana kwa sehemu ya kupitisha miundombinu.

Anasema wakazi wa maeneo hayo wamejenga hadi barabarani na hivyo hakuna eneo la kupitisha maji.

“Two weeks (wiki mbili) tulikuwa huko pamoja na Mstahiki Meya (Profesa Davis Mweamfupe) tukiwataka watuonyeshe ni wapi maji yatapita. Kila ukigusa mahali pa kuweka mifereji unaambiwa ni kiwanja,” anasema.

Anasema wanatambua shida iliyopo katika maeneo hayo na kwamba katika utatuzi wa kujaa kwa maji kwa barabara ya Nzuguni Serikali katika mwaka wa fedha 2019/20 imetenga Sh650 milioni kwa ajili ya ujenzi wa daraja.

Pia, anasema wametenga Sh120 milioni kwa ajili ya usanifu wa barabara hiyo kusudi kuwawezesha watu wa maeneo hayo kutoka na kwenda katika maeneo mengine ya jiji.

Anasema kazi ya usanifu wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 15 inakaribia kukamilika.

Hata hivyo, anasema changamoto nyingine katika ujenzi wa barabara hiyo ni wapi maji yatakwenda baada ya ujenzi ambao utalazimu kuinyanyua juu.

Anawataka wakazi wa kata hiyo kushirikiana na kampuni inayofanya urasimishaji wa maeneo kuhakikisha wanaacha eneo kwa ajili ya miundombinu ya maji, umeme na mifereji.

“Sisi tunatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa kuunganisha maeneo ya sokoni, stendi na mji wa Serikali lakini tunatambua umuhimu wa hiyo ya barabara usanifu,” anasema.

Anaomba watu waelewe badala kuendelea kung’ang’ania kuacha mita mitano ambayo hawawezi kuweka mifereji, miundombinu ya maji na umeme.