Moto wateketeza vibanda 13 soko la Singida

Muktasari:
- Moto huo ulianza jana saa nne usiku na sasa Jeshi la Zimamoto na Tanesco wanafanya uchunguzi kubaini chanzo.
Dodoma. Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika umeteketeza vibanda 13 vilivyomo ndani ya Soko Kuu la Singida na kuharibu mali ambazo bado thamani yake hakijafahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale amethibitisha leo Jumamosi Julai 5, 2025 kwamba sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara ziliokolewa.
Moto huo ulianza saa nne usiku na kwamba taarifa zilifika kwa wakati kwa vyombo husika ndiyo maana hakukuwa na madhara zaidi.
Kamanda Kakwale amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, kwani Jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na Tanesco bado wanafanya uchunguzi.
"Tulipata taarifa mapema na kuwahi eneo la tukio, hakuna madhara kwa binadamu lakini tulifanikiwa kuokoa mali nyingi kwenye mabanda mengine na hadi muda huu tumeimarisha ulinzi," amesema Kakwale.
Mbali na kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na Jeshi la Zimamoto, amesifu ushirikiano waliouonyesha wananchi kwenye uzimaji na uhamishaji wa mali za wafanyabiashara katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, vibanda vilivyoteketea mali chache ndizo ziliokolewa, lakini sehemu kubwa zimeteketea.
Jakobo Annamlingi amesema moto huo licha ya kutoteketeza sehemu kubwa ya mali, madhara yamekuwa makubwa kwani wengi walianza kubomoa mabanda kukwepa moto.
Jakobo amesema hofu ilisababisha waanze kuhamisha mali kwa haraka bila utaratibu hata kusababisha vingine kupotea na kuvunjika.
"Bahati yetu moto ulianza mapema na tulipotoa taarifa Zimamoto walikuja kwa wakati wakakuta watu tupo wengi tukaanza kumsaidiana," amesema Jakobo.
Mama lishe, Anastazia Mkumbo amezungumzia tukio hilo kwamba limewatia hasara kwa kuvunja mabanda ili yasidake moto.
Amesema hakuna wizi wala udokozi uliofanyika katika eneo hilo kutokana na idadi kubwa ya Polisi waliokesha wakilinda, bali hofu iliwafanya watu kuvunja mabanda na kuchomoa nyaya za umeme na sasa wanatakiwa kuanza ukarabati.