Msimamo Necta wagawa wadau
Dar es Salaam. Hatua ya Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (Necta) kutotoa orodha ya shule wala wanafunzi waliofanya vizuri au vibaya, imeibua mjadala kwa wadau wa elimu waliokuwa na maoni tofauti.
Alipotangaza matokeo hayo jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema baraza limeona hakuna tija ya kuweka orodha hiyo hivyo watu waache mazoea ya miaka ya nyuma.
“Ina tija gani kumtaja mmoja kati ya shule nyingi na tena bahati mbaya unamlinganisha na mwingine ambaye hawakusoma kwenye mazingira yanayofanana?” alihoji Amasi.
Kupanga orodha ya shule 10 zilizofaulisha zaidi alisema ni sawa na kuzitangazia soko badala ya ushindani. “Kutangaza shule ya kwanza huenda tunaifanyia marketing (kuiuza), ni jambo ambalo halina tija tumeona tuondokane nalo,” alisisitiza.
Msimamo huo umeibua mjadala kutoka kwa wadau baadhi wakisema inadidimiza ushindani na wengine wakiusifu kuwa utadumisha usawa kwa wanafunzi bila kujali mazingira wanayosoma.
Mkuu wa Idara ya Misingi ya Elimu na Utawala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Dk Oscar Magava alihoji “kama sababu ni tofauti ya mazingira kama inavyosema Necta, kwa nini wote wanatungiwa mtihani mmoja?”
Hata kwenye utunzi wa mitihani, alisema Serikali ilipaswa kuzingatia mazingira ya kila mwanafunzi.
“Kama unashindwa kuwalinganisha katika matokeo mbona uliwatungia mtihani mmoja, iweje utambue utofauti wa mazingira mwishoni?” alihoji.
Dk Faraja Kristomas wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema utaratibu huo haukuwatendea haki baadhi ya wanafunzi kwani sio sawa kumshindanisha mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza kutoka shule ya kata na mwenye ufaulu kama huo kutoka shule binafsi.
“Kimsingi yule aliyepata daraja la kwanza kutoka shule ya kata anastahili pongezi zaidi kwa sababu mara nyingi uwekezaji katika shule binafsi ni mkubwa ukilinganisha na shule za kata.”
“Pia, baadhi ya shule binafsi huwa na utaratibu wa kuchuja wanafunzi na kuwachukua wale wenye uwezo mkubwa tu na kuwaacha wenye uwezo wa chini jambo ambalo halifanyiki kwenye shule za kata,” alisema.
Benjamin Nkonja kutoka Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongosco) alisema utaratibu huo hautokuwa na afya kwani utaondoa ushindani kwa shule na wanafunzi hatimaye kuporomosha ubora wa elimu.
“Hakuna binadamu anayeweza kupata maendeleo ikiwa haoni mtu mwingine aliyeendelea zaidi yake, wanafikiri kufanya hivyo wanatafuta jawabu la tatizo kumbe wanakwenda kutengeneza tatizo kubwa zaidi,” alisema.
Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Amina Salum alisema kutajwa kwa shule na wanafunzi bora mbali na kuchochea ushindani kwa wanafunzi na shule, kuliwasaidia wazazi kujua shule zipi zinafanya vizuri kwa wakati husika ili kumpeleka mtoto.
“Ingewezekana kutengeneza hata orodha ya shule za Serikali zilizofanya vizuri na zile za binafsi,” alishauri Amina.
Mwalimu wa sekondari ya Serikali aliyeomba kuhifadhiwa jina lake aliunga mkono uamuzi wa Necta akisema “wanafunzi wanalelewa katika mazingira tofauti, huenda anasoma shule hizi za saint akawa bora akiwa huko na anayesoma (shule za kata) naye atakuwa bora katika mazingira ya huko.”