Mtanzania mbaroni Marekani tuhuma utakatishaji fedha Sh8 bilioni
Muktasari:
- Imeelezwa, kati ya mwaka 2013 na 2019, Sunna na mwenzake, raia wa Nigeria, Nafise Quaye, (47) walipokea Dola za Marekani 3.2 milioni (zaidi ya Sh8 bilioni) kutoka kwa mwathirika wa ulaghai huko Texas.
Dar es Salaam. Mtanzania Sunna Sepetu (37) ametiwa mbaroni kwa kosa la utakatishaji fedha nchini Marekani.
Imeelezwa, kati ya mwaka 2013 na 2019, Sunna na mwenzake, raia wa Nigeria, Nafise Quaye, (47) walipokea Dola za Marekani 3.2 milioni (zaidi ya Sh8 bilioni) kutoka kwa mwathirika wa ulaghai huko Texas.
Taarifa kutoka nchini humo inasema, fedha hizo zilihamishiwa kwenye akaunti za benki zilizoanzishwa na washtakiwa kwa majina ya kampuni mbalimbali za ukandarasi.
Wote kwa pamoja wametiwa mbaroni mjini Worcester, Massachusetts, baada ya kushtakiwa kwa kula njama ya utakatishaji fedha zilizotokana na utapeli.
Kesi yao iliendeshwa kwa siku nane kwenye mahakama moja ya shirikisho mjini humo.
Uamuzi huo ulitangazwa na wakili wa serikali, Jane Young, ambaye alisisitiza dhamira ya idara ya sheria ya kuwashtaki wale wanaofanya ulaghai wa mtandao.