Ole Sendeka atoa kauli kushambuliwa, akumbuka tukio la Tundu Lissu

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka

Muktasari:

  • Mbunge huyo wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amezungumzia tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi akiwa ndani ya gari huku akikumbuka tukio lililomtokea Tundu Lissu kama hilo Septemba 7, 2017.

Simanjiro. Mbunge wa Simanjiro (CCM), mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema anamshukuru Mungu amenusurika baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana wilayani Kiteto akienda jimboni kwake.

Ole Sendeka na dereva wake,  walishambuliwa kwa risasi wakiwa kwenye gari lakini hawakudhurika wakiwa eneo la Ndaleta wilayani Kiteto  jana Ijumaa Machi 29, 2024.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Machi 30, Ole Sendeka amesema anamshukuru Mungu kwa kumnusuru na tukio hilo kwani risasi zilizopigwa kwenye gari hazikuwapata.

"Hakuna zaidi ya kushambuliwa na kupigwa risasi za kutosha ila tunamshukuru Mungu tumenusurika hazikutupata," amesema Ole Sendeka.

Amesema baada ya kutoka eneo la tukio hilo wamerudi kituo cha polisi Kibaya wilaya ya Kiteto na akitoka hapo atakuwa na namna nzuri zaidi ya kuzungumza juu ya tukio hilo.

"Ninachoweza kuzungumza kwa sasa namshukuru Mungu tumenusurika kwani wamenipiga karibu na zile walizompiga Tundu Lissu ila Mungu amenisaidia hazikunilenga," amesema Ole Sendeka.

Tukio ambalo Ole Sendeka analizungumzia la Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara lilitokea mchana wa Septemba 7, 2017, eneo la Area D, jijini Dodoma akiwa ndani ya gari lake pamoja na dereva wake.

Lissu alikutwa na mkasa huo muda mchache akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Kipindi hicho alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki. Zaidi ya risasi 30 zilishambulia gari hilo na kumsababishia majeraha mbalimbali mwili.

Lissu aliepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali. Usiku wa siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na Januari, 2018 akapelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Wakati Ole Sendeka akieleza hayo, Polisi wanaendelea kuwasaka watu waliomshambuilia. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu amesema japokuwa waliofanya tukio hilo wamekimbia ila wana uhakika kuwakamata wahusika hao.

"Bahati mbaya mbunge na dereva wake hawakuweza kusoma namba za gari hilo ila polisi tutahakikisha tutawakamata kwani jamii ya eneo hili itatupa ushirikiano wa kutosha," amesema Kamanda Mwakatundu.

Amesema ana amini watuhumiwa hao watatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo husika.

Pia, Msemaji wa Polisi, David Misime amesema timu ya watalaamu wa uchunguzi inayohusisha matumizi ya risasi kutoka makao makuu ya Polisi Dodoma,  imetumwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Manyara kuchunguza kwa kina tukio hilo ili kubaini waliohusika kina nani au kusudio lao ni nini.

Walaani tukio hilo

Mgombea ubunge wa Chadema mwaka 2020, aliyegombea na Ole Sendeka uchaguzi mkuu wa mwaka huo, Emmanuel Ole Landey ametoe pole kwa mbunge huyo na dereva wake kwa tukio baya na la kukemewa lililowapata.

"Mbegu tuliyoipanda ya wasiojulikana inapaswa kung'olewa sasa na kuiangamiza, kwani matunda yake ni sumu kwa Taifa na hayakubariki kwa namna yoyote ile," amesema Ole Landey.

Diwani wa Terrat, Jackson Ole Materi ametoa pole kwa mbunge huyo kwani ni habari mbaya kwa wana Simanjiro huku Diwani wa Emboreet, Yohana Shinini naye akitoa pole kwa tukio hilo.

Mkazi wa kata ya Naberera, Aloyce Loishiye amelaani vikali kitendo hicho na kuomba vyombo husika kuwachukulia hatua kali wote waliofanya tukio hilo.