Raia watatu wa Burundi wakamatwa na simu 61 za wizi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, akionyesha simu zilizokamatwa na jeshi hilo mkoani Shinyanga. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

  • Wasichana watatu watuhumiwa kuwaibia simu wanaume wanaokutana nao nyumba za kulala wageni.

Shinyanga. Wasichana watatu raia wa Burundi wanashikiliwa na Polisi mkoani Shinyanga, kwa kosa la kupora simu 61 na kuwaibia wanaume waliokuwa wanalala nao kwenye nyumba za wageni.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema hayo leo Desemba 20, 2023 alipozungumza na waandishi wa habari.

Amesema watuhumiwa wamekamatwa wakiwa na simu hizo wakati wa doria na misako iliyolenga kuimarisha usalama wa raia na mali zao, katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Magomi amesema watuhumiwa wameingia nchini bila kufuata utaratibu na kazi kubwa wanayoifanya ni kuwapora wanaume wanaokutana nao.

"Baada ya kuwahoji kwa hatua za kwanza wamesema kuna bosi wao anawatuma kutoka Uganda, hivyo wakiiba wanampelekea anaenda kuziuza. Niwaombe wananchi wote kuwa makini pale tunapoona wageni kama hawa na tutoe taarifa mapema kabla hawajafanya wizi mkubwa," amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi amesema wanaendelea kudhibiti wizi wa mafuta, nondo na saruji kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali na wadau wengine.

"Katika msako tuliofanya kwa mwezi mmoja tumekamata lita 260 za mafuta ya dizeli licha ya kwamba kwa sasa wizi huo umepungua," amesema.

Amesema watuhumiwa wa makosa 2,806 ya aina mbalimbali wamekamatwa mwaka huu.

Kati ya makosa hayo amesema matano ni ya kusababisha ajali za barabarani.

Kamanda amesema pia wamekamata lita 173 za pombe ya gongo, pikipiki saba, televisheni nne, goroli za karasha 106, bangi misokoto 15 na noti bandia tisa za Sh85,000.

"Niwaombe wananchi wawe makini na watu wanaotumia  fedha bandia. Fedha hizi mtu akikupa au akinunua kitu jaribu kuikunja, kwani ukiikunja haikunjuki inabaki vivyo hivyo. Fedha halali inakunjuka yenyewe, hivyo tuwe makini," amesema Magomi.