Simu za wizi pasua kichwa

Muktasari:

  • Simu za wizi zinazoingizwa kama mtumba hata mpya zinazopitishwa njia za panya kutoka Kenya zinatajwa kuwa biashara kubwa katika baadhi ya mikoa nchini.


Mikoani. Simu za wizi zinazoingizwa kama mtumba hata mpya zinazopitishwa njia za panya kutoka Kenya zinatajwa kuwa biashara kubwa katika baadhi ya mikoa nchini.

Ukiacha simu za wizi na za magendo, taarifa zinaonyesha uwapo wa mafundi wenye uwezo wa kuchezea namba za utambulisho (IMEI) ili kufanikisha matumizi yake.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara na kanda ya ziwa, umebaini simu zinazoibwa Kenya huingizwa na kuuzwa kwenye mikoa hiyo kama mtumba, huku zinazoibwa Tanzania zikipelekwa kuuzwa Kenya.

Vyanzo mbalimbali vimelidokeza gazeti hili kuwa mchezo huo umefanya simu za gharama kubwa zinazoibwa Kenya zisionekane kwenye mifumo ya mawasiliano nchini humo, vivyo hivyo kwa zile zinazoibwa nchini.

Kwa Mkoa wa Kilimanjaro mathalan, inaelezwa soko kubwa la simu za wizi zinazoingizwa kwa njia za panya katika wilaya za Rombo na Moshi, zinauzwa kituo kikuu cha mabasi cha Moshi mjini.

“Hizo simu zinaingizwa kwa magari na pikipiki zikiwa kwenye mifuko ya sulphate na ni mtandao mkubwa. Huwezi kupewa risiti hata siku moja ukizinunua, zinauzwa bei rahisi sana. Simu ya Sh700,000 utauziwa Sh400, 000,” kilidokeza chanzo chetu.

“Simu zinazoibwa Tanzania sio zote zinapelekwa Kenya, zinazopelekwa huko ni Samsung Galaxy na iPhone ambazo hazina password (namba ya siri) maana hizo iPhone kama ina Password huifungui mzee,” kilidai chanzo hicho.

Chanzo hicho kutoka ndani ya Jeshi la Polisi kilisema kama mifumo ya mamlaka za mawasiliano ya Kenya na Tanzania zingekuwa zinasomana na kubadilishana taarifa za simu zilizoibwa katika mataifa hayo, nchi ingetikisika.

Inaelezwa mkoani Kilimanjaro, simu hizo huingizwa kupitia mipaka ya Holili na Tarakea wilayani Rombo na Madarasani na Kitobo katika Wilaya ya Moshi na kusafirishwa kwa siri hadi Moshi na miji ya jirani.

Taarifa zaidi zinasema baadhi ya mafundi simu wa kituo hicho na maeneo jirani wana uwezo wa kuchezea namba ya IMEI kiasi kwamba zikitafutwa na polisi hazionekani kwenye mfumo.

Jijini Tanga, biashara ya magendo ya simu za mkononi imeshamiri huku ikielezwa nyingi zimekuwa zikiingizwa nchini kwa njia za panya zaidi ya 45 zilizopo katika mpaka wa Horohoro na bandari bubu kadhaa.

Mwananchi limeelezwa kuwa bodaboda hutumika zaidi kupitisha simu hizo za magendo kupitia mpaka wa Horohoro hususan katika Kata ya Mwakijembe wilayani Mkinga.

Dereva bodaboda ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema baadhi ya wafanyabiashara huzisafirisha kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Singida na Dodoma.

Jijini Arusha, biashara hiyo inaelezewa kuongezeka kwa sababu watu wengi huzikimbilia kwa kuwa zinauzwa kwa bei ndogo kwenye baadhi ya maduka ya watengeneza simu, vituo vya mabasi na vijana wanaozinadi kuwa ni za mtumba zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Taarifa nyingine zinadai kanda ya ziwa nao ni waathirika wa simu hizo za wizi ingawa wauzaji jijini Mwanza walijiweka kando wakisema ni vigumu kufahamu ipi ni ya wizi na simu ipi ni halali.

Mamlaka ya Mapato Tanzania

Oktoba 7 mwaka 2020, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na vyombo vingine ilikamata simu 2,845 zilizokuwa zikiingizwa kimagendo kutoka Kenya.

Simu hizo zenye thamani ya Sh700 milioni zilikamatwa eneo la Mashati wilayani Rombo, zikiwa zimepakiwa kwenye lori lililobeba ndizi zenyewe zikiwekwa chini.

Kati ya Januari 2020 hadi Agosti 2022, simu 3,236 zenye thamani ya Sh33.66 milioni zilikamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro zikiingizwa nchini.

Akizungumzia sula hilo, Meneja Msaidizi wa TRA, Idara ya Forodha, Ali Fum alisema kwa mwaka 2021/22, hakukuwa na magendo mengi ya simu za kisasa kwa kuwa kodi iliondolewa.

“Changamoto ya uingizaji simu za magendo ilikuwa huko nyuma, lakini mwaka jana haikuwa kubwa kwa kuwa Serikali iliondoa kodi kwenye simu kubwa na kuacha kwenye hizi simu ndogo za viswaswadu,” alisema Fum.

Alisema changamoto hiyo kwa sasa alisema inaweza kurejea kwa kuwa kodi imerejeshwa tena kwenye simu hizo.

Hata hivyo, alisema wataendelea na jitihada za kudhibiti kuhakikisha bidhaa zote zinapita katika njia rasmi mipakani.

Fum alisema mikakati waliyo nayo ni pamoja na kuimarisha doria na kushirikiana na askari polisi pamoja na raia wema kudhibiti maeneo yote ya mpakani na wanafikiria kutumia ndege zisizo na rubani kudhibiti magendo ya aina zote mipakani.

“Tunaendelea kufanya utafiti wa kutumia drones ambayo tunaweza kuirusha maeneo ya mpakani na mtu akakaa ofisini kuiongoza, hii itasaidia kupunguza tatizo hili,” alisema Fum.

Meneja huyo alisema changamoto kubwa katika kudhibiti magendo ni uwazi wa mpaka kwani kuna njia nyingi za panya.

Kuanzia Januari mpaka sasa, Fam alisema jumla ya simu 3,236 zenye thamani ya Sh33.66 milioni zilikamatwa mkoani Kilimanjaro zikiingizwa kutoka Kenya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo aliwataka wenye taarifa za magendo ya simu za mkononi kuzitoa kwake kwa sababu wanaikosesha Serikali mapato inayostahili.

“Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ikiwamo TRA tumekuwa tukikamata bidhaa za magendo zinazosafirishwa kwa njia za panya baharini na nchi kavu zikiwamo simu,”alisema Kamanda Safia na kuongeza:

“Ningependa kuwaarifu kuwa tunawafuatilia na tutawaweka mikononi mwa dola kama hawataacha biashara hiyo. Tutatumia taarifa za kiintelijensia na zinazotolewambao kwa kweli wanaotoa ushirikiano mkubwa.”

Akizungumzia wizi huo, Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo alisema halifahamu suala hilo.

“Hilo la wizi wa simu unaovuka mipaka ni jambo jipya nisiloweza kulizungumzia, labda niwasiliane na wenzangu wanaohusika na masuala ya namna hiyo,” alisema.

Mafundi simu wanena

Akizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina, mmoja wa mafundi wa simu na vifaa vya kielektroniki jijini Mwanza alisema kutokana na kukua kwa teknolojia, upo uwezekano wa kuchezea utambulisho (IMEI) wa simu.

“Teknolojia inakua na kubadilika kila siku, inawezekana kuuharibu mfumo wa utambuzi kuzuia taarifa za simu zinazoibwa zisinaswe wala kuonekana kwenye mifumo ya mamlaka za mawasiliano,” alisema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na fundi mwingine wa simu wa kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi ambaye alidai japo haujihusishi kuchezea IMEI, lakini amesikia uwepo wa wenzake wenye utaalamu huo.

“Usije ukaninukuu huko sitaki matatizo, japo sijaona kwa macho ila kuna simu moja ya wizi alipelekewa fundi (anamtaja) ila sijui aliifanyaje kwa sababu hadi leo sijasikia kasheshe yoyote. Sijui alifanyaje,” alisema fundi huyo.

Fundi aliyejitambulisha kwa jina la Mathis John wa kituo mabasi ya abiria jijini Arusha, alisema simu hizo zinaingizwa nchini baadhi zikiwa chakavu na mpya.

John alisema huwezi kubaini kwa urahisi ipi ni simu ya wizi na ipi ni chakavu ambayo mtu ameamua kuuza.

Alisema nyingi huwa zimefutwa kumbukumbu na wakipata mteja wanaanza kwanza kurudisha program zake.

Fundi mwingine, Godi Malisa alisema simu kutoka nchi jirani ni nyingi na huwezi kujua ni za wizi ama mtumba kwa sababu zilizotumika hununuliwa kama ilivyo vifaa vingine.

“Kwa mfano simu kama iPhone kununua mpya kabisa ni ghali, inauzwa hadi zaidi ya Sh2 milioni lakini zipo nyingi mitaani na madukani ambazo zimetumika na zinauzwa bei nafuu hadi Sh200,000 na baadhi zinatoka Ulaya na Afrika Kusini,” alisema Malisa.

Wauzaji wa simu

Rahem Hassan, mfanyabiashara wa simu katika Mtaa wa Rwagasore jijini Mwanza alisema japo haufahamu mtandao unaonunua na kuuza simu za wizi, kuna uwezekano wa kuziingiza sokoni na kuziuza.

“Sifahamu chochote kuhusu simu za wizi kutoka nje kuingizwa na kuuzwa nchini kwa sababu naagiza simu na bidhaa mpya lakini huenda wapo wanaofanya hivyo japo mimi binafsi sijasikia,” alisema Hassan.

Dereva bodaboda aliyeomba asitajwe gazetini alisema wafanyabiashara wanaojihusisha na simu za wizi kutoka Kenya huzisafirisha kwa kuzifunga kwenye maboksi.

“Nyingi hupelekwa mikoani,” alisema dereva bodaboda huyo.