Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ruwasa yatenga Sh600 milioni kupunguza changamoto ya maji Lindi

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva akimuelekeza jamba Kaimu Meneja wa Ruwasa  Manispaa ya Lindi Mhandisi Athanas Lume wapili kulia alipotembelea Kijiji cha Dimba Kata ya Kilolambwani  kwa ajili ya kukagua miradi ya maji. Picha na Bahati Mwatesa.

Muktasari:

  • Wananchi wasema visima vitaondoa changamoto ya maji wanayoshirikiana na wanyama.

Lindi. Wakati wananchi wa Kata ya Kilolambwani Manispaa ya Lindi wakilalamika kupata changamoto ya upatikanaji wa maji, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Lindi, umesema Serikali imetenga Sh600 milioni kwa ajili ya kuchimba visima 10 katika Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Mtama

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Januari 21, 2025 na Kaimu Meneja wa Ruwasa,Wilaya ya Lindi, Mhandisi Athanas Lume na kwamba visima hivyo vitafanikisha juhudi za Serikali kuboresha upatikanaji wa maji vijijini.

"Hadi sasa, usambazaji wa maji vijijini umefikia asilimia 77 kwa jimbo la Mchinga na asilimia 74 kwa Halmashauri ya Mtama. Lengo ni kufikia asilimia 85 ifikapo Oktoba 2025," amesema Mhandisi Lume.

Amesema visima vinavyochimbwa vitanufaisha wakazi 71,174 wa Mchinga na wakazi 166,493 wa Halmashauri ya Mtama.


Kilio cha wananchi

Mkazi wa Kilolambwani, Fatuma Hassan, amesema wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye visima vya asili wanavyoshirikiana na wanyama.

"Ukisema uondoke alfajiri ukimuacha mume kitandani, anakasirika. Ukibaki kulinda ndoa, unakaa bila maji. Hali hii imeathiri ndoa za wanawake wengi,” amesema Fatuma.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuleta maendeleo na kutenga fedha kwa ajili ya kuchimba visima hiyo, ili kuondoa adha hiyo.

Mwananchi mwingine ameeleza kuwa maji wanayotumia sasa wanakunywa tumbili na  mifugo, lakini wanalazimika kuyachota hivyo hivyo na kisha kuyaacha yatulie kabla ya kuyatumia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Dimba, Kata ya Kilolambwani, Saidi Kilunjila, amesema:"Tulikuwa tunakunywa maji wanayokunywa na tumbiri, lakini ujio wa visima vya Ruwasa unatupa matumaini mapya."


DC atoa maagizo

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amewataka Ruwasa kuhakikisha visima hivyo vinakamilika kwa wakati ili wananchi wapate maji.

"Niwaombe Ruwasa kuhakikisha wananchi wa Mchinga na Halmashauri ya Mtama wanapata maji kwa wakati. Hii itasaidia kufikia malengo ya Rais Samia ya kutua ndoo kichwani kwa mama wa kijijini," amesema Mwanziva.