Prime
Safari ya watoto wenye uzito uliopitiliza kuanza matibabu

Imani, Gloria na mama yao wakipokelewa na muhudumu wa afya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) tayari kwa kuanza matibabu. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Imani (6) ana uzito wa kilo 76, mdogo wake Gloria (4) ana uzito wa kilo 62, uzito unaowafanya washindwe kucheza, kuanza shule.
Dodoma/Dar. Februari 4, 2024 ni siku ya furaha kwa familia yenye watoto wenye uzito kupita kiasi, Imani na Gloria Joseph waliowasili Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila kwa matibabu.
Imani (6) baada ya kupokewa hospitalini hapo leo Februari 4, 2024 alipimwa na kukutwa na uzito wa kilo 76, huku mdogo wake Gloria (4) akiwa na kilo 62.
Wawili hao walianza safari saa 11 alfajiri kutoka nyumbani kwao Mtaa wa Makole, jijini Dodoma wakiwa wenye furaha pamoja na wazazi wao.

Watoto Imani na Gloria wakipanda kwenye bajaji pamoja na wazazi wao kwa ajili ya kuelekea stendi ya mabasi Dodoma, tayari kuanza safari kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu. Picha na Merciful Munuo
Katika safari walisindikizwa na baba yao mzazi, Joseph Kalenga aliyetoa shukrani kwa Gazeti la Mwananchi kwa kutoa taarifa za watoto wake na kisha kupata msaada wa matibabu yaliyokuwa yanawaumiza kichwa.
Safari ilianza kwenye bajaji mbili alizoagiza baba yao, ili kuwapeleka kituo cha basi.
Changamoto ya kwanza ni namna ya kuingia katika usafiri wa bajaji kutokana na uzito walionao na ufinyu wa nafasi ndani ya chombo hicho cha usafiri, hivyo walilazimika kusaidiwa kwa kusukumwa.
Gloria na Imani wameondoka nyumbani wakikatiza mitaa ya Makole kuelekea kituo cha Shabiby kilichopo jirani na chuo cha CBE, jijini Dodoma.
Muda wote njiani, watoto na wazazi wao walikuwa wenye furaha na kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wanafika stendi kwa wakati.
Wakiwa kwenye bajaji mara kadhaa waliuliza iwapo wameshafika Dar es Salaam, baadhi ya watu wanawashangaa kwa uzito walionao wanaposhuka kutoka kwenye bajaji kwa msaada wa wazazi wao.
Wakiwa kituoni Shabiby kabla ya kupanda kwenye basi, baba yao Kalenga ameeleza furaha yake na matarajio yake kwa afya za watoto wake.

Imani, Gloria pamoja na wazazi wao wakiwasili katika stendi ya mabasi Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Amesema ana matumaini makubwa na safari ya watoto wake kuwa itakuwa ya mafanikio makubwa na uzito wao utapungua baada ya matibabu.
“Nitashukuru nikiona watoto wangu wamepata nafuu na wamepona vizuri. Nitashukuru nikiona afya yao imetengamaa tofauti na sasa,” amesema na kuongeza;
“Kwa heshima kubwa nalishukuru Gazeti la Mwananchi, baada ya wao kutazama hali ya watoto ilivyo wamepaza sauti, msaada ukapatikana na wao wamekamilisha kusafirishwa kwa watoto wangu. Najihisi faraja, pia naona mkono wa Mungu unafanya kazi kwa kuwa yote ni mipango yake.
“Nawatanguliza kwa sala, Mungu ndiye kila kitu waende salama, wafike salama na mambo mengine yakienda vizuri nitashukuru,” amesema.
Baada ya mazungumzo wanapata nafasi ya kuagana na baba yao na kazi ngumu zaidi inakuwa kumpandisha Gloria kwenye gari, ambaye uzito mkubwa umemuathiri zaidi kulingana na umri wake.
Safari ya kuelekea Dar es Salaam inaanza saa 12 asubuhi kwa Gloria, Imani na mama yao, Vumilia Elisha.

Imani, Gloria, mama yao pamoja na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Rachael Chibwete wakiwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Picha na Merciful Munuo
Ndani ya basi watoto walikuwa watulivu, usingizi ukiwachukua kwa muda mrefu.
Hata hivyo, hali ilibadilika kidogo kwa Imani. Alipozinduka kutoka usingizini alihisi kichefuchefu na kuanza kutapika.
Mama yake alimpa huduma na baada ya muda alirejea katika hali ya kawaida.
Baada ya dakika 30, Imani akaanza kumwambia mama yake anahisi njaa, hali iliyomfanya mama yake achanganyikiwe na kutaka kumpa zabibu, ili apunguze njaa.
Hata hivyo, baadhi ya abiria walimshauri avute subira kidogo ili afike kwenye kituo atakapopata chakula na huduma nyingine, badala ya zabibu ambazo haijulikani kama zingepunguza njaa au zingeongeza kichefuchefu kwa sababu walikuwa hawajala chochote tangu walipoanza safari.
Muda mwingi wa safari Gloria alikuwa amelala.
Saa 4.20 asubuhi tunapowasili Morogoro kwenye kituo cha mapumziko, mama yao kwa kuhofia safari, amesema ni vyema wakapata chai na andazi moja pekee.
"Natamani wasile kitu chochote mpaka tufike ili wasisumbue njiani, maana wakila wataanza kusumbua," amesema Vumilia.
Hata hivyo, baada ya kuletewa chai, Imani alishindwa kunywa kutokana na basi kuanza kuondoka hivyo ilimwagika. Gloria alikunywa chai kusaidiwa na mama yake waliyekuwa wamekaa pamoja.
Wawasili Dar
Safari iliendelea mpaka saa 8.10 mchana walipowasili kituo cha mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Kutokana na uzito walio nao, walitumia dakika 15 kushuka ndani ya basi wakisaidiwa na wahudumu wa Shabiby.

Imani, Gloria, mama yao pamoja na Mhariri wa jarida la afya gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta aliyekwenda kuwapokea stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam. Picha na Merciful Munuo
Wakiwa kituoni hapo, baadhi ya watu waliacha shughuli zao na kukusanyika kuwaangalia.
Saa 8.35 mchana safari ya kutoka stendi ya Magufuli ilianza kuelekea Hospitali ya Mloganzila iliyopo umbali wa kilomita tano.
Mapokezi Mloganzila
Akizungumza baada ya kuwapokea watoto hao, daktari bingwa wa magonjwa ya dharura hospitalini hapo, Asha Iyullu amesema wanaendelea na vipimo vya awali.

Imani, Gloria, mama yao pamoja na mhudumu wa afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzira) wakipokelewa tayari kwa kuanza matibabu. Picha na Merciful Munuo
"Wamekuja kwa changamoto ya uzito mkubwa. Leo tumeanza na vipimo vya awali, kuanzia kesho wataanza vipimo zaidi na jopo la madaktari kujua changamoto ya mafuta yaliyopo mwilini na kwenye damu,” amesema.
Amesema, "Hospitali yetu tuna ushirikiano na King's college, tulianza kutoa huduma hii mwaka jana. Tumewafanyia vipimo, mpaka leo Gloria ana kilo 62 na Imani ana uzito wa kilo 76."
Mama wa watoto hao, Vumilia Elisha amesema: "Wamepokewa vizuri, nimefurahi wameanzishiwa matibabu. Nimewasilisha nyaraka zote za rufaa."
Watoto hao waliopokewa saa 8.50 mchana, walianza kwa kufunguliwa jalada kwa ajili ya uchunguzi wa awali na matibabu.

Mtoto Imani akichukuliwa vipimo vya awali na wahudumu wa afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila). Picha na Merciful Munuo
Kwa mujibu wa muuguzi aliyewahudumia, Mathayo Nyuma, vipimo vya awali walivyochukuliwa ni vya presha, mapigo ya moyo na kiwango cha oksjeni, wingi wa damu na vingine ambavyo vitahitajika baadaye.

Mtoto Gloria akichukuliwa vipimo vya awali na wahudumu wa afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila). Picha na Merciful Munuo
Mama aeleza furaha yake
Mama wa watoto hao, Vumilia amesema ameridhishwa na huduma waliyopewa baada ya kuwasili Mloganzila na kwamba ana imani watapata matibabu mazuri yanayowastahili.
Akizungumzia tukio la watu kuwashangaa watoto wake baada ya kushuka kituo cha mabasi, amesema hali hiyo ameizoea japokuwa kuna wakati huwa inampa huzuni.
"Hii hali nimeshaizoea na wakati mwingine huwa inanipa huzuni kwa sababu wengine huwa waaniuliza maswali magumu ambayo siwezi kuyajibu naishia tu kukaa kimya, hata hivyo nawashukuru kwa sababu walinisaidia kuwashusha wanangu kwenye basi," amesema Vumilia.
Februari mosi, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi alitoa nafasi ya matibabu bure kwa watoto hao kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu.
Hatua hiyo imekuja siku 18 tangu Gazeti la Mwananchi liliporipoti kuhusu uwepo wa watoto hao wanaoishi mtaa wa Makole, Kata ya Makole, jijini Dodoma.