Watoto wenye uzito kupindukia kutibiwa bure Mloganzila
Muktasari:
- Mpaka sasa Imani Joseph (6) ana uzito wa zaidi ya kilo 70 huku mdogo wake, Gloria Joseph (4) akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 50 unaowafanya washindwe kucheza, kuanza shule na kujumuika na wenzao pamoja na kula kupita kiasi.
Dar/Dodoma. Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imetoa nafasi ya matibabu bure kwa watoto wenye uzito kupita kiasi, Imani (6) na Gloria Joseph (4) kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu (Lipid clinic).
Hatua hiyo imekuja siku 18 tangu Mwananchi liliporipoti kuhusu uwepo wa watoto hao wanaoishi katika Mtaa wa Makole, Kata ya Makole jijini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Februari mosi, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema wameona picha za watoto hao na wazazi wao (Joseph Kalenga na mkewe, Vumilia Elisha) wakiomba msaada.
“Uzito wao ni mkubwa si wa kawaida. Muhimbili tumesikia rai ya mama kuomba msaada, tutakachoomba kikubwa wapewe rufaa ya kuja Dar es Salaam.
“Kwa kuwa mwaka moja uliopita Hospitali ya Taifa Muhimbili ilichaguliwa moja ya zile nne barani Afrika kushungulikia mambo ya uzito mkubwa ‘lipid clinic’ zinazoshughulikia tatizo la mafuta na tunafanya kazi na wenzetu wa Uingereza, sisi ni moja ya kituo cha hizi kliniki barani Afrika,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu rufaa hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Hospitali, Dk Ernest Ibenzi amewataka wazazi wa watoto hao kufika hospitalini kushughulikiwa rufaa ya matibabu.
Mama wa watoto hao, Vumilia Elisha ameishukuru Hospitali ya Muhimbili kutoa msamaha huo wa matibabu.
“Nimefurahi nilivyopata hizi taarifa kuambiwa nimefanikiwa watoto wangu kupata huduma, lakini changamoto sina uwezo wa kufika Muhimbili ingawa nimejiandaa kwenda, niko tayari. Nawashkuru Mwananchi na wote walioshiriki asanteni,” amesema Vumilia.
Matibabu yatakavyokua
Profesa Janabi amesema jopo la wataalamu wanaoendesha kliniki hiyo litaendesha uchunguzi wa kina kubaini chanzo kama ni vinasaba vya kuzaliwa navyo au kuna matezi mengi yanayoshughulika na chakula hayapo sawasawa.
“Kuna vipimo vingi tutawafanyia, ni mapema kusema mpaka pale watakapokuwa wamefika. Kubwa kwetu ni lazima tuanze uchunguzi na kama ni tiba tuanze mapema kwa kuwa uzito unakuja na magonjwa mengi ya moyo, figo, kisukari, kiharusi itakuwa ni muhimu sana kuwasaidia,” amesema.
Profesa Janabi ametaja athari za uzito kupita kiasi unaweza kuleta athari katika kutembea, kushiriki michezo, kusoma vizuri na wao wenyewe kuwaletea msongo kutokana na majina kadhaa wanayoitwa ikiwemo ‘bonge’.
“Wenyewe kwa wenyewe wanaitana bonge inaweza kuwaathiri kisaikolojia,” amesema Profesa Janabin na kueleza kutokana na hilo watahakikisha wanapata tiba ya kisaikolojia wao na wazazi wao kwa kipindi watakachokuwa wakiendelea na matibabu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Mloganzila, Rosemary Minja anayehusika na matibabu ya magonjwa ya matatizo ya mafuta kwenye damu na uzito mkubwa unaoambatana na mafuta mengi kwenye damu amesema; “Matatizo haya yanaweza kuwa tofauti, tutawachunguza na tukipata majibu tutaanza tiba. Mara nyingi husababishwa na homoni za madini joto, ukuaji mara nyingi inasababisha uzito unakua mkubwa.
“Pia inaweza kuwa matatizo ya kurithi ya vinasaba ni muhimu wakafika mapema kwa ajili ya uchunguzi kwa kuwa wanaweza kuwa na shida ya homoni au vichocheo ambavyo vinaweza kusababisha changamoto nyingine zikaleta madhara kwenye moyo na mishipa ya damu.”
Dk Minja amesema uzito mkubwa si moyo na mishipa ya damu pekee itaathirika, pia huathiri mifupa kwa kuwa miili itabeba uzito mkubwa kwa muda mrefu.
Amesema mtoto anavyokuwa uzito utaathiri mifupa na viungo vya mwili, hivyo wataangalia nini sababu na matibabu yatategemea wamebaini nini kwenye vipimo vya uchunguzi.
“Tutashirikiana na madaktari wa watoto wanaohusika na homoni za watoto kufanya uchunguzi wa uhakika,” amesema.
Kwa mujibu wa Kapinga, watoto wao wanakula chakula kingi kuliko kawaida, kwani wakitengewa kilo tano za wali na hata za ugali wanakula wanamaliza peke yao.
Wazazi wa watoto hao wamesema uzito unawafanya washindwe kucheza na kujumuika na wenzao.