Sawe: Siku ya mtoto wa Afrika ni kuangalia changamoto za watoto na namna ya kuzitatua

Sunday June 13 2021
mtoto pic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Katika kuelekea maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mtoto wa Afrika, Jukwaa la vipaji kwa watoto limetoa msaada kwa watoto wanaougua saratani.

 Akikabidhi msaada huo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mratibu wa tamasha la siku ya mtoto wa Afrika, Ailinda Sawe amesema wameona ni vema watoe huo ili kuwafariji na wasijione kama jamii imewatenga.

Alitaja baadhi ya msaada waliopeleka kuwa ni nguo, viatu, sabuni, sare za shule, miswaki na dawa za meno.

“Tulifikiria ni vizuri kabla ya kwenda kwenye tamasha tuwatembelee watoto wenye uhitaji ambao wamelazwa kwenye wodi ya saratani ili kuwafariji, kuwaonesha upendo na kuona changamoto ambazo zinawakabili.

“Kwasababu siku ya mtoto wa Afrika ni kuangalia changamoto za watoto na namna ya kuzitatua, basi tukaona tuje hapa. Na sisi tumefanya hivyo ili kukumbusha jamii kwamba siku ya mtoto wa Afrika ni siku ambayo jamii iangalie kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa kwamba ni wajibu anatuzwa, anaangaliwa na haki zake zinafuatwa kila mahali,” amesema Sawe.

Ameongeza kuwa, pamoja na msaada huo pia wamechanga fedha kwaajili ya kuwezesha kuwapatia bima ya afya na hilo litakuwa zoezi endelevu.

Advertisement

Said Masudi ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye saratani ameshukuru kwa msaada huo na kuomba watu wengine wajitokeze kutoa msaada.

“Huduma zinaendelea vizuri na watoto wanapatiwa huduma nzuri hivyo natoa wito kwa jamii wanapoona watoto wao wana matatizo wawahi hospitali,” amesema Masudi.

Naye Muuguzi Kiongozi wa wodi inayohudumia watoto wenye saratani, Asteria Henjewele amesema wodi hiyo inahudumia watoto wenye saratani aina zote nchini, lakini kuna mpango wa huduma kuihamishia mikoani kwasababu kuna watoto wengi wanaofika hapo.

“Kilio changu kikubwa ambacho natamani kila mtanzania kimfikie tunatamani hawa watoto wafike mapema hospitali kwasababu saratani inatibika lakini kama umewahi. Tukiangalia takwimu tulizonazo watoto wengi wanafika hospitali wamechelewa kwahiyo tunapambana kupigania maisha yao lakini tunashindwa kwasababu wamechelewa,” amesema Asteria.

Advertisement