Serikali ya Tanzania kuajiri watumishi 44,096

What you need to know:

  • Kada ya elimu wataajiri watumishi wapya 10,297, afya 11,215, kilimo 1,383, mifugo 1,250, uvuvi 733, Jeshi la Polisi 1,782, Magereza 843, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji 512  na watumishi wapya wa hospitali za mashirika ya kidini na hiari 1,240.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema katika mwaka wa fedha 2021/22 inatarajia kuajiri watumishi wa umma wapya 44,096.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi  Aprili 22,  2021 Waziri wa Nchi Ofisi  Menejimenti ya Utumishi wa Umma  na Utawala Bora,  Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilishwa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kada ya elimu wataajiri watumishi wapya 10,297, afya 11,215, kilimo 1,383, mifugo 1,250, uvuvi 733, Jeshi la Polisi 1,782, Magereza 843, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji 512  na watumishi wapya wa hospitali za mashirika ya kidini na hiari 1,240.

Amesema Serikali itaajiri watumishi 14,841 wa kada mbalimbali ikiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu vyote vya umma nchini pamoja na kada nyingine ambazo haziko kwenye sekta zilizoainishwa awali.

Hata hivyo, amesema watumishi 92,619 wa kada mbalimbali watapandishwa vyeo na watumishi 2,360 watabadilishwa kada katika utumishi.

Amebainisha kuwa  maelekezo yatakayotolewa wakati huo ni kuchambua na kuhakiki madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma 17,699 yenye thamani ya Sh37.47 bilioni na kuchukua hatua ipasavyo.

Aprili 15, 2021 Serikali ya Tanzania ilieleza matarajio yake ya kuajiri watumishi wapya 44,811 katika mwaka wa fedha 2020/21.

Hayo yalielezwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wakati akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka huo wa fedha.

Alitaja ajira hizo mpya kuwa ni kada ya elimu (13,529), afya (10,467), kilimo, mifugo na uvuvi (2,145) Jeshi la Polisi (2,725), magereza (685), Jeshi la Zimamoto (501), uhamiaji (495) na hospitali za mashirika ya kidini na hiyari (1,262).

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.