Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaeleza ilivyojipanga kukabiliana na athari za mvua

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

Wakati mvua zikiendelea kunyesha nchini na kuharibu miundombinu nchini, Serikali imeeleza jinsi ilivyojipanga kukabiliana na uharibifu wa  barabara

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha huduma zinaendelea wakati wa msimu wa mvua, huku akiwataka wanaoishi mabondeni kuhamia kwenye maeneo yenye miinuko.

Majaliwa amesema hayo katika kipindi cha maswali ya  papo kwa hapo leo Alhamis Februari 8, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo.

Butondo amesema kipindi hiki kimekuwa na wakati mgumu wa mvua hasa katika baadhi ya mikoa ya kanda ya ziwa, nyanda za juu kusini na pwani ya kaskazini ikisababisha uharibifu wa miundombinu.

 “Serikali ina mpango gani wa haraka na wakidharura na wa kibajeti ili kuhakikisha tunanusuru hali ya kimawasiliano kwa maana ya barabara ambazo hali sasa imekuwa mbaya sana katika maeneo ya mijini na vijijini?,” amehoji Butondo.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema jukumu hilo wamezipa taasisi za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha wakati wote wanafuatilia mwenendo wa barabara nchini na kama kuna eneo limeharibika kurudisha kwa haraka zaidi.

Amesema taasisi hizo kupitia Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zimejiweka vizuri kibajeti na kila mbunge aliyeuliza swali hili aliambiwa fedha zilizopelekwa kwenye jimbo lake.

“Kwa hiyo Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha tunarudisha miundombinu ili huduma za wananchi katika maeneo hayo ziendelee. Najua hatutarudisha kwa viwango vya awali lakini muhimu ni kuwafanya watu waendelee kupita kwenye miundombinu hiyo,” amesema Majaliwa.

Pia, ametoa tahadhari kwa watu walio katika maeneo hatarishi kuondoka kwenye maeneo hayo na kukaa kwenye maeneo yenye miinuko ili kupunguza maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

“Lakini niwahakikishie Watanzania taasisi zetu ziko macho, kupitia Tanroads na Tarura, tunaanza katika halmashauri yenyewe ambako Tarura ipo,” amesema Majaliwa.

Amesema wanazo ofisi za Tanroads kwenye kila mkoa zenye jukumu lai kupita maeneo mbalimbali na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kila mvua zinaponyesha ili kuangalia miundombinu iwapo imebaki salama au kama  kuna tatizo limejitokeza ili kurudisha huduma kwa haraka zaidi.