Sh167.6 bilioni zaombwa maandalizi ya uchaguzi mkuu


Muktasari:

 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeishauri Serikali ihakikishe ununuzi wa mashine za uchapaji na matengenezo ya zilizo chakavu unakamilika kwa wakati kabla ya kuanza maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu.

Dodoma. Serikali imeliomba Bunge kuidhinisha Sh167.6 bilioni kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hayo yamo kwenye taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Joseph Mhagama amesema hayo leo Jumatano Aprili 3, 2024 bungeni jijini Dodoma alipowasilisha taarifa hiyo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, bajeti ya maendeleo ya ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, imeongezeka kwa Sh161.65 bilioni kutoka bajeti ya mwaka unaomalizika.

Amesema hilo limechangiwa na ongezeko la bajeti ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Amesema kamati inatoa pongezi kwa jitihada za Serikali kuendelea kupanga bajeti ili kutekeleza miradi mingi zaidi kwa kutumia fedha za ndani.

“Kamati inaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi mahiri, hodari na shupavu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza kutenga fedha za maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa kutumia fedha za ndani bila utegemezi wowote wa fedha za nje,” amesema Dk Mhagama.

Hata hivyo, kamati imeishauri Serikali ihakikishe ununuzi wa mashine za uchapaji na matengenezo ya zilizo chakavu unakamilika kwa wakati kabla ya kuanza maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu.

Kamati imeshauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iweke mpango endelevu na mahususi wa matumizi ya jengo la ofisi hiyo unaoendana na vipaumbele vyake.