Simbachawene amjibu Mpina

Muktasari:

  • Amesema anadhani pengine kuna ajenda iliyojificha kusema nchi imefeli wakati inatekeleza miradi ya maendeleo.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amemshukia mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akimtaka kutodharauliana.

Simbachawene amesema hayo leo Aprili 19, 2024 alipojibu hoja za wabunge walizotoa walipochangia bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema nchi ambayo Mpina anasema imefeli inawezaje kutekeleza miradi mikubwa mingi ambayo kama nchi nyingine zikitekeleza zinafilisika.

Amesema nchi ambayo imefeli inaweza kukusanya kodi kati ya Sh1 trilioni hadi Sh3 trilioni kwa mwezi.

“Ninachotaka kusema Naibu Spika, hapa tusijidharau namna hii, kama mtu una mambo yako ni vyema ukayazungumza kwa namna nyingine lakini si mambo ya kitaalamu kama hayo.”

“Nchi yetu inaheshimika, Rais wetu anaheshimika ndiyo maana kila mahali anapoenda duniani wanampa Shahada ya udaktari. Ni heshima wanampa zawadi zote za kubeba wanaona hazifai hadi wanaamua kumpa zawadi ya kichwani,” amesema.

Amesema kwa heshima hiyo anayopewa Rais Samia (Suluhu Hassan) duniani, haiwezekani kudharaulika ndani ya nchi, na lazima watu wajenge tabia ya kujiamini na kuheshimiana.

Simbachawene amesema mtu hawezi akasema ni nchi iliyofeli halafu papo hapo akasema anamheshimu Rais anayeiongoza nchi hiyo na kwamba hiyo ni hujuma.

Amesema katika kipindi ambacho kuna changamoto mbalimbali za ugonjwa wa Uviko-19 na kudorora uchumi duniani, Tanzania imekuwa ikitekeleza miradi kila mahala nchini.

“Kule Meatu kwake tu (Mpina), Tarura (Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini) amepelekewa fedha lakini Sequip (Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari) amepelekewa shule mbili na Boost (Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji wa Shule za Awali na Msingi), amepelekewa madarasa chungu nzima,” amesema.

Amesema pia katika jimbo lake amepelekewa gari la wagonjwa moja lakini pia kituo cha afya kimoja kimejengwa, akahoji anawezaje kusema kuwa nchi imefeli.

Simbachawene akisikilizwa na Mpina amesema anadhani pengine kuna ajenda iliyojificha.