Spika atoa angalizo kampuni za simu kuhusishwa mikopo ya kausha damu

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, akijibu maswali ya wabunge leo Jumatano, Aprili 24, 2024 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Ataka Naibu Waziri ajiridhishe kwanza, asema hataki malalamiko kutoka kampuni za simu.

Dodoma. Majibu kwa swali la nyongeza la mbunge yamemwibua Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyesema asingependa kupata barua za malalamiko kutoka kwa kampuni za simu nchini kwamba zinatoa mikopo maarufu kausha damu.

Katika swali la nyongeza bungeni leo Aprili 24, 2024 mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond, amesema baadhi ya kampuni za simu nchini zinaongoza kwa kukopesha haraka bila kujaza fomu yoyote.

"Vijana wengi na wanawake wanavutiwa lakini mikopo hiyo ni kausha damu, je ni lini Serikali itatoa elimu kwa wanawake, vijana na wajasiriamali," amehoji.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, akijibu swali hilo amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, taasisi za kifedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Baada ya majibu hayo, Spika Dk Tulia amemtaka Chande kufuatilia ili kujiridhisha kama kweli kampuni za simu zinahusika kutoa mikopo hiyo na kutoa mrejesho kwake.

"Kama ni kweli wanatoa mikopo hiyo mnatakiwa kuanza nayo, lakini kama si kweli kuwajadili bungeni ni kutowatendea haki," amesema.

Spika amesema asingependa kupata barua za malalamiko kutoka kwa kampuni hizo kwamba zinatoa mikopo kausha damu.

Awali, mbunge wa Viti Maalumu Felista Njau,  amehoji ni hatua gani zinazochukuliwa na Serikali kuwasaidia wanawake na vijana ambao wanapata matatizo ya akili na ndoa kuvunjika kutokana na mikopo hiyo.

Katika swali la nyongeza, Njau amesema kumekuwa na mikopo yenye athari kwa wanawake na vijana ambayo imesababisha kupata tatizo la akili na ndoa kuvunjika.

"Je, Serikali haioni ni wakati wa kukomesha mikopo hii ili kuwanusuru vijana na wanawake," amehoji.

Njau amesema pamoja na uwepo wa sheria na miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania  (BoT), bado mikopo imeendelea kuwepo na hasa ile ya kausha damu na kuhoji nini kauli ya Serikali.

Naibu Waziri, Chande amesema Serikali inatoa maagizo kwa taasisi hizo kuacha mara moja na kwamba itafuatilia.

Chande ameagiza BoT kufuatilia kwa karibu na kama kuna taasisi yoyote inayoenda kinyume cha sheria na miongozo zitachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuzifutia usajili.

Njau katika swali la msingi amehoji kuna mkakati gani wa kufuatilia na kuchukua hatua kwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye riba kubwa kinyume cha mwongozo wa BoT.

Chande amejibu akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na kisheria ili kudhibiti tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo kinyume cha miongozo iliyopo.

Amezitaja hatua hizo kuwa, kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kusimamia ukwasi katika mfumo wa kibenki ili kuendana na mahitaji halisi ya kiuchumi na kuweka mazingira rafiki ya utoaji mikopo.

Nyingine ni kuendelea kuhimiza benki kuwasilisha taarifa za wakopaji na kutumia kanzidata ya taarifa za wakopaji wakati wa uchambuzi wa maombi ya mikopo, ili kupunguza vihatarishi vya ongezeko la mikopo chechefu.

"Kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu fursa za mikopo zilizopo, viwango vya riba na athari zake, vigezo vya kuzingatia na umuhimu wa kurejesha mikopo," amesema.

Ametaja hatua nyingine ni kuitisha vikao vya majadiliano na wadau katika sekta ya fedha ili kutambua changamoto zilizopo na kushirikishana mikakati ya kukabiliana nazo.

Hatua nyingine amesema ni kufanya ukaguzi, ufuatiliaji na tathmini ya uzingatiaji wa sera, sheria na miongozo iliyopo ili kuboresha na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaobainika kukuika taratibu.