‘Takataka fursa ya kujiimarisha kiuchumi’
Aaron Sanga Wa kwanza kulia akitoa Elimu namna ya kutengeneza Nishati ya Mkaa Mbadala kwa kutumia Karatasi zilizotumika, mafuu ya Nazi pamoja na Chenga za Mkaa eneo la Mazimbu Manispaa ya Morogoro. Picha na Johnson James
Muktasari:
- Ili kuendelea kutunza mazingira na kuepuka matumizi ya mkaa na kuni, imeelezwa kuwa hakuna budi kila mmoja kutumia mkaa mbadala.
Katika mazingira kuna changamoto mbalimbali lakini wananchi wanaweza kuzitumia kama fursa ya kujiingizia kipato ikiwamo kutumia taka kutengeneza mkaa mbadala.
Johnson James, Mwananchi
Morogoro. Mkurugenzi wa Taasisi ya My Birthday Tree yenye mlengo wa kutunza mazingira Morogoro, Festo Asegile amewataka Watanzania kutumia takataka zinazowazunguka maeneo yao kama fursa ya kujiingizia kipato.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Juni 23, 2024, Asegile amesema katika mazingira kuna changamoto mbalimbali lakini wananchi wanaweza kuzitumia kama fursa ya kujiingizia kipato ikiwamo kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia taka.
“Leo tumeshuhudia vijana na wanawake wameshiriki katika mafunzo ya utengenezaji mkaa mbadala unaotengenezwa kupitia karatasi ambazo zimekwishatumika, hivyo tunawaomba Watanzania waichukue hii kama fursa ya kuwaimarisha kiuchumi bila kuchafua mazingira,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema ili kuendelea kutunza mazingira na kuepuka matumizi ya mkaa na kuni, hakuna budi kila mmoja aanze kutumia mkaa mbadala utakaosaidia kuepuka ukataji wa miti.
Aron Sanga, mratibu kutoka taasisi ya kimazingira ya Climate hurb, amesema takwimu zilizopo zinaonyesha asilimia 26.6 ya Watanzania wanatumia nishati ya mkaa huku asilimia 63.2 wakitumia kuni.
“Malengo yetu ni kutatua matatizo ya kimazingira kwa kutumia vyanzo vilivyopo kwenye mazingira yetu, tunatumia takataka kuzalisha mkaa mbadala zikiwamo za vifuu, karatasi zilizotumika na chenga za mkaa, yote haya huwa tunaona ni uchafu tuzitumie kuzalisha mkaa mbadala ili tulinde mazingira yetu,” amesema Sanga.
Amesema takwimu zinaonesha mpaka sasa mahitaji ya mkaa ni tani milioni 2.3 na ifikapo mwaka 2030, mahitaji yatakuwa zaidi ya tani 4.6 milioni.
Hivyo, Sanga amesema ili kuondokana na ukataji miti kwa kiwango hicho, lazima jamii ijielekeze kwenye nishati safi na mbadala.
Victoria George ni mmoja wa waliopata mafunzo ya namna ya kutengeneza mkaa mbadala, anasema kwa mafunzo aliyopata yatamsaidia kutunza mazingira na kwamba, elimu ya utengenezaji mkaa huo inatakiwa kuwafikia Watanzania wengi.
Mshiriki mwingine, Nashitwa Hashimu amesema utengenezaji wa mkaa mbadala utasaidia kulinda mazingira kwa sababu soko la kuni na mkaa litaanza kufifia iwapo watu watapatiwa elimu sahihi ya matumizi ya mkaa huo mbadala samba na uchakataji wake.