TLS yaipiga chenga Mahakama Kuu
Muktasari:
- TLS imetafuta njia mbadala ya kujadili ajenda za mkutano mkuu uliozuiliwa na Mahakama.
Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), imewaelekeza viongozi wake wa Kanda na mikoa kufanya mikutano hiyo kujadili ajenda zilizopaswa kujadiliwa katika mkutano uliozuiwa.
TLS imetoa maelekezo hayo baada ya Mahakama Kuu kuzuia mkutano mkuu wa dharua wa chama hicho.
Kupitia baraza la uongozi chama hicho kimewaelekeza wanachama kuwasilisha katika baraza hilo mapendekezo yatakayofikiwa katika mikutano hiyo.
Hilo ni moja ya maelekezo ya namna ya kwenda mbele kutimiza wajibu wa utekelezaji wa majukumu ya TLS, kwa ajenda zilizopaswa kujadiliwa na kuazimiwa katika mkutano mkuu uliozuiwa na Mahakama.
TLS ilipanga kufanya mkutano mkuu wa dharura Desemba 16, 2023, ukiwa na ajenda kuu mbili, ambazo ni muundo na mamlaka ya kamati ya kitaifa ya mawakili na kamati ya mawakili ya mikoa, huku ya pili ikiwa ni kuhusu matokeo ya marekebisho ya Sheria ya TLS yaliyopitishwa Novemba, 2023.
Ijumaa jioni, Desemba 15,2023 chama hicho kilipokea amri ya Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam ya zuio la mkutano huo, kutokana na shauri dogo la maombi lililofunguliwa na mmoja wa wanachama wake, Wakili Baltazary Mahia dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Amri ya Mahakama ilitolewa siku hiyo baada ya kusikiliza shauri hilo upande mmoja ili kusubiri kulisikiliza pande zote hapo Februari 8, 2024.
Baraza la uongozi la TLS lilitii amri hiyo na kuwaarifu wanachama wake kuhusu kusitishwa kwa mkutano huo hadi watakapopewa maelekezo mengine.
Jumatatu, Desemba 18, 2023 baraza hilo lilitoa taarifa nyingine kwa wanachama likitoa maelekezo kadhaa yakiwemo ya kuendesha mikutano na kujadili ajenda hizo katika kanda na mikoa.
Baraza limeeleza halijaridhishwa na amri ya Mahakama ya upande mmoja kuzuia mkutano wake halali kwa mujibu wa sheria, hivyo litafanya jitihada za kiutawala kuelezea manung’uniko yake.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Rais wa TLS, Wakili Harold Sungusia imeeleza imewateua mawakili Francis Stolla na John Seka (wote marais wastaafu wa TLS) kwa kushirikiana na kamati ya masuala ya sheria na jinsia, kufuatilia kesi hiyo na kujiandaa kukiwakilisha chama hicho mahakamani.
“TLS kitatetea haki yake mahakamani wakati wa usikilizwaji wa pande zote Februari 2024, na kupinga kwa nguvu shauri hilo ili kulinda utawala wa sheria na kuhamasisha haki. Kitahakikisha kuwa gharama zote ambazo chama hicho pamoja na wanachama wameingia zinarejeshwa,” inasisitiza taarifa hiyo.
Kuhusu amri ya kusitisha mkutano, taarifa inaeleza baraza halihoji haki ya wanachama kukishtaki chama chao, bali utolewaji wa amri ya upande mmoja dhidi yake wakati ofisi zake ziko umbali wa mwendo wa chini ya dakika 20 kutoka Mahakama Kuu.
Pia inaeleza uhalali wa hati ya kiapo kinachounga mkono shauri hilo la maombi lililofunguliwa na mwanachama wake inatia shaka.
TLS imesema inafuatilia kwa ukaribu shauri hilo kwa masilahi ya haki.
“Baraza la uongozi linatambua umuhimu wa uhuru wa Mahakama katika mfumo wa usimamiaji haki,” imesema taarifa hiyo na kuongeza, ilishangazwa na utolewaji wa amri hiyo ya upande mmoja dhidi yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Imeeleza taarifa kuhusu mkutano mkuu wa dharura ilitolewa hadharani Desemba mosi, 2023; siku 14 kabla ya kutolewa kwa amri ya Mahakama ya zuio.
Imeleeza kwa nia njema kwa mwanachama wa TLS ambaye hakuridhishwa na taarifa ya mkutano huo akitaarifu chama hicho au hata kufungua shauri hilo mahakamani mapema, ili kutoa fursa kwa pande zote kufika mahakamani au kuruhusu marekebisho ya kasoro zinazolalamikiwa.
TLS katika taarifa imesema kwa kusoma nyaraka za shauri hilo inaonekana lilifunguliwa Desemba 15, 2023 na siku hiyohiyo lilisikilizwa upande mmoja na chama hicho kilicho mtaa wa Chato umbali wa kilomita 6.5 kutoka Mahakama Kuu hakikupewa haki ya kusikilizwa.
“Inaonekana rahisi zaidi mwombaji kupeleka TLS amri ya upande mmoja saa 12.30 jioni baada ya saa za kazi kuliko kufanya jitihada kukipatia hati ya wito kufika mahakamani kujitetea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
TLS imebainisha kuwa shauri limepangwa kusikilizwa Februari 8, 2024 lakini Bunge limekitaarifu kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mawakili na Sheria ya TLS kati ya Januari 8 na 10,2024.
Imeeleza ndiyo maana imechukua hatua za haraka vingingevyo hakitapata fursa hiyo.
Shauri lililopo
Wakili Mahia katika shauri la maombi namba 27673/2023, anapinga uamuzi wa TLS kupitia baraza la uongozi kuitisha mkutano huo kwa madai hauna maana, si halali na umekiuka taratibu.
Hata hivyo jitihada za Mwananchi Digital kumtafuta Mahia, hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.