‘Tumuombee Mchungaji Kimaro arudi salama’

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Dk Eliona Kimaro.

Dar es Salaam. Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Anna Kuyonga amewaomba waumini wake kumuombea mchungaji kiongozi wa ushirika huo, Dk Eliona Kimaro amalize salama likizo yake.

Januari 16, Dk Kimaro aliwaaga waumini hao akiwaeleza kuwa aliitwa ofisi ya msaidizi wa askofu ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani na kupewa likizo ya siku 60 na atakapoimaliza akaripoti ofisi ya dayosisi hali iliyoibua mjadala huku baadhi ya waumini wakitaka kurejeshwa kwa mchungaji wao.

Katika ibada ya kwanza jana, Mchungaji Anna aliwataka waumini hao kuendelea kumwombea Mchungaji Kimaro aliye likizo maalum ili arejee akiwa salama.

“Mchungaji Kiongozi Dk Eliona Kimaro yuko kwenye likizo maalum, tunaomba muendelee kumuombea huko alipo ili aweze kumaliza likizo yake na kurudi kwenye majukumu yake,” alisema Mchungaji Anna.

Licha ya ibada hiyo kuhudhuriwa na waumini wachache, tamasha la vijana lililoitwa anza mwaka na bwana lililokuwa lifanyike jana kanisani hapo liliahirishwa bila kuelezwa sababu na Mchungaji Anna aliwaeleza waumini kuwa limesogezwa mbele hadi watakapotangaziwa tena.

Muumini mmoja alisema Dk Kimaro alikuwa mlezi wa vijana usharikani hapo hivyo kutokuwepo kwake kunaweza kuwa kumechangia kuahirishwa kwa tamasha hilo hali inayowavunja moyo vijana.

“Ukiangalia hata ibada ya leo washarika ni wachache, hata vijana wengi hawajashiriki ibada. Tamasha lisingeweza kufanikiwa, nadhani wameona hadi likizo itakapoisha ili na yeye ashiriki,” alisema kijana huyo.

Victoria Lekule, muumini wa kanisa hilo alisema kupungua kwa waumini kumetokana na kutokuwepo kwa Mchungaji Kimaro.

“Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao na vyombo vya habari zimewavunja moyo watu wengi hivyo kuna haja ya kanisa kutumia busara kumaliza jambo hili ili kuondoa mpasuko unaoweza kutokea,” alisema Lekule.

Levina Kimwaga, muumini mwingine alisema kumpa likizo Mchungji Kimaro akiwa amewaandalia semina kimewafadhaisha wengi.

Mpaka tunakwenda mitamboni, juhudi za kumtafuta Mkuu wa KKKT Dayosi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa na Mchungaji Dk Kimaro hazikuzaa matunda.

Wakati anawatangazia kuhusu likizo hiyo, Mchungaji Kimaro alizungumzia semina iliyokuwa ianze Januari 16 aliposema, “semina yetu ni ya wiki mbili (semina ya neno la Mungu) lakini leo nimepewa barua ya likizo ya siku 60.”