Upepo mkali waacha majanga Katavi

Baadhi ya nyumba zilizoezuliwa mapaa katika Kitongoji cha Kasekese A wilayani Tanganyika.Picha na Mary Clemence

Muktasari:

Wataalamu wa majenzi wasisitiza wananchi kuzingatia ujenzi bora.

Katavi. Upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa umeezua mapaa ya nyumba 18 na zingine kubomoka, maafa yaliyosababisha kaya 10 kukosa makazi katika  kitongoji cha Kasekese A, kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Februari 12, 2024, Sclolastica Budeba aliyeathiriwa katika tukio hilo amesema mvua ilinyesha Februari 10, 2024 saa 11 jioni.

“Nilikuwa nimekaa nje na watoto wangu saba ilipoanza kunyesha nikaingia ndani, ukaja upepo mkali nikatoka kwenda nyumba nyingine niliyodhani ni imara,” amesema Scolastica na kuongeza:

“Nikachungulia nje nikaona mabati yametoka, nikarudi ndani upepo ukazidi nikawakumbatia watoto wangu, mabati yakaezuliwa nikaenda kwenye mti wa mwembe kujikinga na wanangu, tuliteseka sana.”

Amesema kwa sasa yeye na familia yake wamehifadhiwa kwa majirani. Ameiomba Serikali imsaidie apate mahitaji ya chakula na mengine ili kuwanusuru wanawe.

Joseph Mabumba, yeye amesema mvua imesababisha kupoteza wapangaji wake 10 baada ya nyumba yake kuezuliwa paa.

“Nasikitika, nilikuwa najipatia kipato kutoka kwenye kodi, sijui nitaishije nimebaki mwenyewe, wapangaji wameondoka, Serikali itusaidie,” amesema Mabumba.

Mhandisi ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Elias Urio amesema athari iliyotokana na mvua na upepo huo imechangiwa na nyumba  kujengwa pasipo kufungwa linta, akisisitiza kujenga nyumba kitaalamu.

“Ni aina ya ujenzi, yule pale amejenga kwa tope lakini amefunga linta na kuna waya za kushikilia paa la nyumba, jengeeni kwa saruji pia itasaidia,” ameshauri.

Urio amesema upepo ulivuma hadi kwake hadi mti ukang’oka na kuanguka lakini nyumba ipo salama kwa sababu ya kufuata taratibu za ujenzi.

Mwenyekiti wa kamati ya maafa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu ametoa pole kwa waathirika akiwahimiza kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kujenga nyumba bora.

“Tumekuja kuwaona kwa ajili ya kuwashika mkono, tumewaletea kilo 300 za mahindi mtageuza kuwa unga, najua hazitoshi japokuwa zitawasaidia kupata chakula cha watoto wenu shuleni,” amesema Buswelu.

Katika tukio hilo hakuna madhara kwa binadamu yaliyoripotiwa kutokea.