Usajili laini za simu waponza kampuni, TCRA yashusha rungu

Muktasari:

  • Habari za ndani zinasema Airtel iliruhusu jumla ya laini 26,009 kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa 6,165 pekee, hivyo faini yake ni Sh1.541 bilioni, Tigo imetozwa Sh473 milioni kwa kutumia jumla ya vitambulisho 1,892 kusajili laini za simu nyingi kuliko inavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.

Dar es Salaam. Kampuni za huduma za simu nchini zimetozwa faini ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa kukiuka kanuni za usajili wa laini ikiwa ni hatua iliyochukuliwa na mdhibiti wa sekta hiyo katika kushughulikia ulaghai wa mtandaoni.

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu ripoti ya robo ya nne ya mwaka 2023 ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), iliyoeleza katika kipindi husika kulikuwa na matukio ya ulaghai 21,788 yakiongezeka kwa asilimia 73 kulinganisha na matukio 12,603 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Chanzo kimoja ndani ya TCRA kimeliambia gazeti dada la The Citizen kuwa katika harakati za kudhibiti ulaghai unaoendelea mtandaoni kampuni zinazotoa huduma za simu zimetozwa faini ya jumla ya Sh2.08 bilioni, kwa kushindwa kutii kifungu kinachowataka kutotumia Kitambulisho cha Taifa kimoja kusajili zaidi ya laini tano kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 37 cha kanuni za usajili wa laini za simu cha mwaka 2023.

Kampuni zilizotozwa faini ni Airtel Tanzania Plc, Honora Tanzania Limited (Tigo), Viettel Tanzania Plc (Halotel), Vodacom Tanzania Plc na Shirika la Simu Tanzania (TTCL), wote hao walibainika kukiuka kanuni hizo katika kipindi cha kuanzia Septemba hadi Novemba, 2023 kama ilivyogunduliwa katika ukaguzi uliofanywa na mdhibiti Novemba, 2023.

Habari za ndani zinasema Airtel iliruhusu jumla ya laini 26,009 kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa 6,165 pekee, hivyo faini yake ni Sh1.541 bilioni, Tigo imetozwa Sh473 milioni kwa kutumia jumla ya vitambulisho 1,892 kusajili laini za simu nyingi kuliko inavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.

Vilevile, vitambulisho 202 tu viligunduliwa kutumika kusajili laini nyingi zaidi ya inavyotakiwa na kanuni, hivyo kampuni ya mawasiliano ya Halotel italazimika kulipa faini ya Sh50.5 milioni.

Upande wa Vodacom vitambulisho 59 vilitumika kusajili idadi ya laini zinazovuka kiwango cha udhibiti. Hivyo kampuni hiyo ambayo ndiyo pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), italazimika kulipa faini ya Sh14.75 milioni.

Kwa TTCL, vitambulisho 12 vilitumika kusajili laini kinyume na kanuni na imetozwa faini ya Sh5 milioni.

Inaelezwa hatua hizo zilichukuliwa makusudi ili kuimarisha usimamizi thabiti wa usajili wa laini za simu, ambao ndiyo msingi wa kukomesha matukio ya ulaghai mtandaoni.

Kampuni za simu hazikupatikana kujibu hicho kinachoelezwa, hata Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo isipokuwa alisema wao huchukua hatua za kiudhibiti kulingana na kila kinachofanyika ili kuhakikisha matukio hayo yanakoma.

“Pamoja na hatua za kiudhibiti (ambazo hakuzidadavua) pia tunaendelea kutoa elimu kwa umma kuelewa kwa kina matumizi salama ya huduma za mtandao,” amesema Dk Bakari.

Kuhusu kuendelea kuwapo kwa vitendo vya ulaghai mtandaoni, Mhadhiri msaidizi wa benki na fedha katika Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Aziz Rashid amesema matukio hayo yasipodhibitiwa yataathiri uchumi wa mtu mmojammoja, lakini pia huenda vikakua na kuathiri uchumi wa nchi.

“Uchumi wa kidijitali miongoni mwa changamoto zake ni ulaghai na uhalifu wa kimtandao. Ulaghai husababisha watu kupoteza pesa, hivyo uchumi wao kuathirika lakini uhalifu wa kimtandao unaweza kutikisa hadi uchumi wa nchi,” amesema Rashid.

Amesema ulaghai wa ‘tuma kwa namba hii’ unapoteza fedha ndogondogo kwa kuwa walio wengi hawatumi nyingi, lakini isipodhibitiwa ikahamia kwenye uhalifu wa kuhamisha mabilioni kutoka benki au kwenye hifadhi ya hiyo mitandao itakuwa hatari kwa uchumi wa nchi.


Kufungiwa laini

Ukiachilia mbali faini zilizotozwa, wiki kadhaa zilizopita TCRA ilitoa taarifa kuwa imezifungia laini 30,309 katika kipindi za miezi mitatu (Oktoba, Novemba na Desemba, 2023) na katika robo ya tatu (Julai, Agosti na Septemba) ilifungia laini 34,848.

Katika taarifa hiyo Dk Bakari alieleza kuwa kufungiwa kwa laini hizo kunasaidia kupunguza matukio ya wizi.

Alisema juhudi za kukabiliana na simu za ulaghai na zinazotumika kwa utapeli zinaelekea kuzaa matunda kutokana na kupungua kwa matukio yaliyoripotiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matukio ya ulaghai yameshuka kutoka asilimia mbili ya idadi ya laini za simu zilizokuwa zimesajiliwa hadi Septemba 2022 kufikia asilimia 0.01 Desemba 2023.

"Simu za ulaghai zilianza kupungua Novemba 2022. Pia simu zilizofungiwa baada ya kuripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu. Zilipungua kwa asilimia 13.03 kati ya Septemba na Desemba 2023," ilieleza taarifa hiyo.