Usimamizi mapato mjadala mkali bungeni

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole-Sendeka akizungumza wakati alipoomba mwongozo kuhusu taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati alipokuwa akichangia maoni yake kwenye mpango wa mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Dodoma. Wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likianza vikao vyake vya bajeti ya mwaka 2023/24, baadhi ya wasomi na wanasiasa wameeleza matarajio yao, ikiwamo kusimamia matumizi ya Serikali.
Bunge hilo lilianza vikao vyake jijini Dodoma kwa kuibua hoja tatu za wabunge kutaka waliotajwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ubadhirifu wachukuliwe hatua.
Hoja nyingine ni kutoridhishwa na upelekaji wa fedha zilizoidhinishwa na Bunge na uuzwaji wa Kiwanda cha Saruji cha Twiga.
Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 ambayo iliibua ubadhirifu na kasoro mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali Serikali kuu, taasisi za umma na miradi ya maendeleo, iliwasilishwa bungeni Aprili 5, 2023.
Baadhi ya wabunge waliwataka wale waliopewa dhamana ya kusimamia fedha hizo, kuchukuliwa hatua ambazo Watanzania wataziona.
Wakichangia azimio la kumpongeza Rais Samia Samia Suluhu Hassan, wabunge walitaka waliohusika na ubadhirifu huo kupisha katika nafasi zao kama walivyotakiwa kufanya hivyo na Rais.
Wabunge walisema Watanzania hawana utamaduni wa kupisha inapotokea kushindwa kuwajibika, hivyo ni kazi yao kuwaonyesha mlango wa kutoka.
“Ambao hawajaona mlango, katika hii miezi mitatu (muda wa vikao vya Bunge la Bajeti) tuwaonyeshe mlango. Hili ni jukumu la msingi la Bunge hili,” alisema Mbunge wa Ubungo (CCM) Profesa Kitila Mkumbo.
Kauli ya Profesa Mkumbo iliungwa mkono na Mbunge Christopher Ole Sendeka (Simanjiro-CCM) na Joseph Musukuma (Geita Vijijini-CCM).
Kwa upande wa hoja ya kutopelekwa kwa fedha zilizopitishwa na Bunge kama inavyotakiwa, wabunge mara kadhaa wamekuwa wakiitaka Serikali kupeleka fedha kama zilivyopangwa.
Mbunge wa viti maalumu, Ester Matiko alisema mwaka 2022/23, Bunge lilitenga takribani Sh26.6 bilioni kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, lakini cha kusikitisha hadi Februari ni Sh5.5 bilioni pekee, kama asilimia 22 tu ndio zimepelekwa.
Kwa upande wa ununuzi wa kampuni ya kuzalisha saruji ya Twiga Cement, wabunge walisema kuruhusu mkataba huo kuendelea kutasababisha ukiritimba utakaoleta madhara makubwa katika bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa ujenzi.
Baadhi ya wabunge walisema ununuzi uliopangwa wenye thamani ya Sh137 bilioni utachochea kupanda kwa bei ya saruji, hasa pale mtengenezaji mkuu atakapofanya matengenezo ya kawaida ya viwanda vyake.
Hoja hiyo ilikuja baada ya Kampuni ya Scancem inayomiliki Twiga Cement kutangaza kuafikiana na Kampuni ya Afrisam kununua asilimia 68.33 ya hisa za Tanga Cement ifikapo Juni 2022.
Waliochangiwa hoja hiyo ni wabunge wa CCM, Kenneth Nollo (Bahi) na Elibariki Kingu (Singida Magharibi).
Wabunge hao walisema uamuzi huo utakaoziunganisha kampuni ya Twiga Cement na Tanga Cement, Serikali itakuwa haina uwezo wa kudhibiti ongezeko la bei.
Matarajio
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka alisema Watanzania wanatarajia wabunge watatoa maoni yao ya kusimamia matumizi ya umma.
“Kwa jumla wake ni usimamizi wa bajeti. Na kusaidia kuandaa nyenzo za kusimamia matumizi ya fedha ili kiwango kinachopangwa kitumike kwa usahihi. Kwa sehemu yao wapendekeze mambo ya kisera, kisheria yanayoweza kubana (matumizi ya fedha). Wakati mwingine bila kuwa na miongozo ya kubana inaweza kuwa ni wakati mgumu,” alisema.
Alisema ni wajibu wa wabunge kutunga sheria au kutafuta taratibu zinazoweza kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kuhusu kununuliwa kwa Kampuni ya Saruji Cement, Dk Mwinuka alisema ununuzi wa kampuni hujitokeza katika kampuni kutegemea ufanisi na mipango.
“Kama mnunuaji atakuja na mipango ya kuongeza ufanisi huwa sio changamoto. Kumekuwa na changamoto kubwa kwenye ufanisi wa viwanda na inapotokea mwekezaji ambaye atakuwa mbunifu, ataongeza ajira, atakuza uzalishaji inaweza kuleta maana,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Dar es Salaam) Dk Richard Mbunda alisema suala la wabunge kuzungumzia ripoti ya CAG, linaonyesha kuwa hawana mchezo katika matumizi mabaya ya fedha za umma.
Dk Mbunda alisema ni wajibu wa Bunge kupitisha bajeti na kuisimamia kwa kuhakikisha inatumika ipasavyo, jambo ambalo wanalifanya. Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche alisema kazi ya chombo hicho sio kuishauri Serikali, bali ni kusimamia fedha za umma kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.