CAG ataka Jaji Biswalo achunguzwe

Jaji Biswalo Mganga
Muktasari:
- Jinamizi la fedha za makubaliano ya kukiri makosa (plea bargaining) linazidi kumwandama aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Jaji Biswalo Mganga, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja na mapendekezo mazito.
Moshi. Jinamizi la fedha za makubaliano ya kukiri makosa (plea bargaining) linazidi kumwandama aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Jaji Biswalo Mganga, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja na mapendekezo mazito.
Ingawa CAG Charles Kichere katika ripoti yake ya ukaguzi maalumu wa fedha za utaratibu huo (plea bargaining) aliyoiwasilisha bungeni jijini Dodoma juzi hakumtaja kwa jina Jaji Biswalo, lakini ripoti inataja wadhifa aliokuwa akishikilia wakati wa utekelezaji wa mchakato huo.
CAG amebaini katika mchakato huo kulikuwa na matumizi ya nyaraka bandia, matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa maadili, kutokuwepo kwa usawa katika mchakato na watu watatu kuchukuliwa fedha zao katika masuala ya kikodi na si jinai.
“Napendekeza mamlaka za uteuzi za aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ziunde Tume huru ya kuchunguza uwezekano wa ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya ofisi ya umma katika mchakato wa makubaliano ya kukiri kosa,” anasema CAG Kichere hiyo.
“Tume hiyo inapaswa kuchunguza madai ya kulazimishwa kwa washtakiwa na ukiukwaji wa Kanuni za Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai (Makubaliano ya Kukiri Kosa) za Mwaka 2021 na kutoa mapendekezo ya uboreshaji wa mapungufu yote yaliyobainika”.
Hata hivyo, baada ya CAG kumkabidhi Rais Samia Suluhu ripoti hiyo, Machi 29 mwaka huu na CAG kupendekeza kuundwa kwa tume huru, Rais Samia alijibu kwa maelezo mafupi kuwa tayari alishaunda Tume ya kutizama mfumo wa Haki Jinai hivyo itashughulikia.
Pamoja na kauli hiyo, bado kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo waathirika wa plea bargaining, wakitaka suala hilo lishughulikiwe na Tume ya Kijaji na wakati ikifanya kazi yake, Jaji Mganga akae pembeni kusubiri matokeo.
Wanaona si sawa suala hilo lishughulikiwe na Tume iliyoundwa kuchunguza mfumo wa Haki Jinai, kwani mapendekezo ya CAG hayahusu mifumo ya Haki Jinai, bali madai ya ukiukwaji wa maadili unaodaiwa kufanywa na Biswalo akiwa DPP.
Biswalo alihudumu u-DPP kwa takribani miaka sita na miezi saba kuanzia Oktoba 6, 2014 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete hadi Mei 11, 2021 alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na nafasi yake akateuliwa, Sylvester Mwakitalu.
Jitihada za gazeti hili kumtafuta Jaji Biswalo jana kupitia simu yake ya mkononi kuhusu mapendekezo hayo ya CAG kumchunguza hazikuzaa matunda, kwani ilikuwa ikiita pasi na kupokewa.

Sababu za kutaka Tume Huru
Katika ripoti yake hiyo, CAG ameeleza wakati wa ukaguzi, alibaini masuala muhimu yanayohusiana na usimamizi wa makubaliano na taratibu za kukiri kosa.
CAG alibaini kulikuwa hakuna uwazi kutokana na upungufu wa nyaraka katika majalada ya kesi 92 kati ya 352 aliyoyapitia ambako kulisababisha mashaka juu ya uadilifu katika mchakato na kwamba upungufu huo wa nyaraka umeathiri wigo wa ukaguzi.
Pia CAG alibaini kutokuwepo na usawa katika kushughulikia maombi ya kuongezwa muda wa mwisho wa malipo ya fidia, huku baadhi ya maombi yakichukua hadi siku 621 kukamilika badala ya siku 30, kama ilivyoelezwa katika mikataba ya kukiri kosa.
“Pia hapakuwa na miongozo au masharti yaliyowekwa ya kuahidi dhamana katika mikataba ya kukiri kosa. Hali hii ilisababisha uwepo wa utofauti katika masharti ya mikataba ya kukiri kosa,” anasema CAG katika ripoti yake hiyo.
CAG amesema aligundua uwezekano wa ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa ni pamoja na kuchukua Sh1.5 bilioni katika malipo ya fidia bila idhini na kufungua mashitaka na kuwashikilia kinyume cha sheria washitakiwa watatu.
Hao walikabiliwa na makosa ya kodi ambayo yalikuwa nje ya majukumu ya ofisi ya DPP.
Halikadhalika iligundulika uwepo wa nyaraka bandia katika mikataba ya kukiri kosa, huku washitakiwa wakidai kulazimishwa kusaini makubaliano hayo na hiyo inaonyesha uwepo wa ukiukwaji wa kanuni zinazosimamia makubaliano ya kukiri kosa.
“Hali hii inaonesha uwepo wa ukiukwaji wa Kanuni namba 12 na 14 za Kanuni za Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Makubaliano ya Kukiri Kosa) za Mwaka 2021, ambao unaleta shaka juu ya uwazi na uadilifu katika mchakato wa kukiri makosa,” anasema.
Pia, uwepo wa ukiukwaji wa haki za washitakiwa wakati wa kukamatwa, kufunguliwa mashtaka, na usimamizi wa kesi zilizoamuliwa kupitia makubaliano ya kukiri kosa.
Aliyoyabaini CAG
Katika ukaguzi huo, CAG aligundua kesi 352 za Kukiri Kosa na Kupunguza Adhabu zilitokea katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo washtakiwa 893 walitia saini makubaliano 380 na kukubaliana kulipa Sh219.13 bilioni.
Kiasi hicho kinajumuisha Sh45.51 bilioni kama fidia kwa makosa ya washtakiwa waliokiri kosa, Sh2.11 bilioni kama faini za mahakama na Sh8.26 bilioni ni malipo yaliyofanywa bila kuwepo makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining).
CAG aligundua Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ilipokea Sh55.87 bilioni na Sh42.68 bilioni zilihamishwa kutoka katika akaunti ya kukiri kosa na kupunguza adhabu.
Uhamisho huu ulijumuisha Sh38.80 bilioni zilizohamishwa kwenda Mfuko Mkuu, Sh3.43 bilioni zilizohamishwa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Sh450.56 milioni zilizorejeshwa kwa waathirika na kati ya majalada 352 yaliyopitiwa, majalada 297 yalikuwa na ahadi za Sh219.13 bilioni, ingawa hata hivyo ni Sh48.52 bilioni pekee ndizo zilizolipwa na washtakiwa katika majalada 195 ya kesi, na kuacha majalada 102 yakiwa na ahadi ambazo hazijalipwa zenye thamani ya Sh170.61 bilioni.