Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanya wa upigaji halmashauri

Mwanza. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebaini upungufu katika mamlaka za halmashauri nchini, ikiwemo kutofanyika kwa malipo ya kazi kwenye miradi ya ujenzi, kuchelewesha malipo kwa siku 90 na baadhi ya makandarasi kulipwa bila kuonyesha matumizi ya fedha za awali walizolipwa.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni jana inaonyesha baadhi ya halmashauri zilikusanya fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato, lakini fedha hizo hazikuonekana kwenye akaunti za halmashauri husika, huku baadhi ya makusanyo hayakufanyika kabisa na hivyo kusababisha upotevu wa mapato.

Taarifa ya CAG Charles Kichere ambayo ilipokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 29, mwaka huu kabla ya kuwasilishwa bungeni jana, ilionyesha kuwa baadhi ya halmashauri hazikukusanya mapato kutoka kwa wadaiwa ambao tayari walikuwa wamepewa hati za madai.

Katika uchunguzi wake, CAG pia amebaini uwepo wa matumizi ya fedha bila nyaraka toshelevu, malipo kufanyika bila kudai risiti za kielektroniki (EFD) huku baadhi ya matumizi yakikosa maelezo wala viambatanisho.

Baadhi ya halmashauri pia zimebainika kufanya malipo kupitia akaunti ya amana kinyume na madhumuni bila idhini, huku ununuzi wa bidhaa na huduma ukifanyika kwa fedha taslimu kinyume cha kanuni za ununuzi.

Ripoti hiyo itakayojadiliwa na kamati za kisekta za Bunge kabla ya kufunguliwa kwa mjadala wa wazi bungeni pia imebaini matumizi ya Sh898.85 milioni kwa matumizi yasiyo na manufaa ambapo kati ya fedha hizo, Sh322.29 milioni zilitumika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Upungufu mwingine uliobainishwa katika ripoti hiyo ni ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambavyo havikuthibitishwa uwepo wake, malimbikizo ya mishahara na stahiki za wafanyakazi kwa kipindi cha mwaka mmoja katika halmashauri 113 zinazofikia Sh119.9 bilioni.

Baadhi ya halmashauri pia zimebainika kutolipa gharama za kusafirisha mizigo ya watumishi 233 waliostaafu huku halmashauri 106 zikibainika kutokuwa na vitengo, vingine vikiongozwa na watumishi 747 wasio na sifa.


Usimamizi wa manunuzi na mikataba

Katika usimamizi wa ununuzi na mikataba, CAG aligundua majaribio ya vifaa vya ujenzi yenye thamani ya Sh1.38 bilioni hayakufanyika kwa miradi ya ujenzi, na malipo ya kazi zilizotekelezwa yenye thamani ya Sh7.8 bilioni yalichelewa kwa zaidi ya siku 90 katika halmashauri.

“Nilifanya tathmini ya ununuzi na usimamizi wa mikataba na kubaini kasoro mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika halmashauri. Aidha, kulikuwa na dosari katika kiasi cha awali cha Sh4.13 bilioni kilicholipwa kwa makandarasi, ikiwa ni pamoja na malipo ya ziada....’’ alisema.


Usimamizi wa Mapato

Alisema kwenye tathmini ya taarifa za mfumo wa mapato (LGRCIS) alibaini mapato ya Sh11.07 bilioni yalikusanywa kutoka vyanzo vingine kupitia mashine za POS lakini hayakupelekwa kwenye akaunti za benki za Mamlaka za Serikali za Mitaa husika.

“Mapitio ya makusanyo ya mapato kupitia LGRCIS yalibaini mapato ya Sh76.59 bilioni hayakukusanywa, hususani yatokanayo na tozo za vizimba vya masoko, uuzaji wa viwanja, mazao ya kilimo,leseni za vileo, ushuru wa uchimbaji wa vifaa vya ujenzi, leseni ya biashara, ushuru wa huduma na ushuru wa kupangisha maduka na nyumba zilizopo katika stendi za mabasi na masoko ya Halmashauri,”alisema

CAG alisema alibaini Sh13.15 hazikukusanywa kutoka kwa wadaiwa mbalimbali waliopewa hati za madai za mfumo wa mapato (LGRCIS) bila kubainisha sababu huku Sh4.94 bilioni hazikuwasilishwa na mawakala wa ukusanyaji mapato kulingana na makubaliano ya mikataba.


Usimamizi wa matumizi

Alisema halmashauri 111 zilikuwa na matumizi ya jumla ya Sh11.78 bilioni ambayo hayakuwa na nyaraka toshelevu ambapo halmashauri 71 zililipa Sh10.08 bilioni bila kudai risiti za EFD, huku halmashauri 40 zikilipa Sh1.70 bilioni bila nyaraka husika.

“Kutumia pesa za umma bila maelezo au viambatisho vya kutosheleza kunatia shaka juu ya uhalali wa malipo hayo. Pia, halmashauri 71 zililipa Sh7.7 bilioni kutoka kwenye akaunti za amana kinyume na madhumuni ya fedha na bila idhini na halmashauri 14 zililipa Sh1.51 bilioni kwa fedha taslimu kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa na huduma kinyume na Kanuni za ununuzi,”alisema

Alisema alibaini halmashauri tisa zilitumiaSh898.85 milioni kwenye matumizi yasiyo na manufaa, kati ya kiasi hicho Sh322.29 milioni zilitumika na halmashauri ya Jiji la Arusha katika ujenzi na ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa barabara ambazo hazikuthibitishwa uwepo wake.


Usimamizi wa Rasilimali Watu na Mishahara

Alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa 113 hazikulipa malimbikizo ya mishaha na stahiki za watumishi yenye thamani ya Sh119.94 bilioni kwa zaidi ya mwaka mmoja huku halmashauri sita zikiacha kuwalipa watumisha 233 waliostaafu gharama ya kusafirisha mizigo baada ya kustaafu Sh309.67 bilioni.

“Vilevile nilibaini kuwa halmashauri 106 zilikuwa na idara na vitengo ambavyo vinaongozwa na watumishi 747 wasio na sifa. Hali hii ilitokana na changamoto zilizojitokeza za miingiliano ya majukumu ya wakuu wa idara na vitengo yaliyoainishwa kwenye muundo wa zamani kwenda kwenye muundo mpya,”alisema

Alisema pamoja na changamoto hizo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimefanya maboresho ya kitaasisi katika makusanyo ya mapato kutoka kwenye vyanzo vyake, ambapo jumla ya Sh891.84 bilioni zilikusanywa katika mwaka wa fedha 2021/22, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 kutoka makusanyo ya mwaka uliopita ya Sh760.95 bilioni.