Prime
Utata taarifa za watuhumiwa ‘waliotumwa na afande’
Muktasari:
- Wakati Waziri wa Mambo ya Ndani akisema watuhumiwa wamekamatwa, Jeshi la Polisi lakwepa kutoa taarifa.
Dar es Salaam. Licha ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuthibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa tukio la ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Mkoa wa Dar es Salaam, bado kuna utata wa taarifa kuhusu mwenendo wa hatua zinazochukuliwa katika tukio hilo.
Bila kuelekeza idadi ya waliokamatwa au ni kina nani, Waziri Masauni kupitia ujumbe wa WhatsApp alijibu swali aliloulizwa na Mwananchi akisema: “Tayari.”
Jibu hilo lilimaanisha kwamba kuna watuhumiwa wamekamatwa.
Wakati Waziri Masauni akieleza hayo, taarifa ya Jeshi la Polisi ya leo jioni Agosti 6, 2024 haikueleza kuhusu waliokamatwa zaidi ya kueleza uchunguzi wa tukio hilo unaendelea vema.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax akizungumza na Mwananchi ametaka watafutwe polisi alipoulizwa kuhusu uwepo wa madai kwamba wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Amesema polisi ndio wenye mamlaka ya kuchunguza na hatimaye kugundua muhusika.
Picha jongefu (video) kuhusu tukio hilo zilisambaa Jumapili ya Agosti 4, mwaka huu kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha vijana watano wakimbaka na kumwingilia msichana huyo kinyume cha maumbile.
Katika video nyingine watuhumiwa hao wanasikika wakimhoji binti huyo na kumshurutisha amwombe radhi mtu aliyetajwa kwa jina la afande, naye alifanya hivyo.
Tangu kusambaa kwa video hizo, jamii kupitia mitandao pamoja na wanaharakati wamelaani tukio hilo wakitaka Serikali ichukue hatua za haraka dhidi ya watuhumiwa waliohusika na ukatili huo.
Majibu ya Masauni, Tax
Alipoulizwa na Mwananchi leo iwapo watuhumiwa hao wameshakamatwa, Masauni alijibu kwa kuandika, “tayari” kupitia ujumbe wa WhatsApp.
Hata hivyo, amesema yupo kwenye mkutano kwa wakati huo.
Akijibu swali iwapo watuhumiwa hao ni askari wa JWTZ, Waziri Tax amesema Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na kutoa jawabu la nani, wa namna gani aliyehusika.
Kwa sababu jeshi hilo limeshaeleza linaendelea kufanya kazi yake, amesema maswali yote kuhusu nani anahusika yaelekezwe huko.
“Unaponiuliza mimi ni kama unamuuliza mtuhumiwa, anayehusika na uchunguzi wa kubaini mhalifu ni Jeshi la Polisi, uliza Jeshi la Polisi kujua hayo.
“Ukimtaja huyo askari wangu nitasema umetaja mtu, lakini sijathibitisha kwa sababu anayefanya uchunguzi ni mtu mwingine,” amesema.
Hata hivyo, amesema Serikali haitavumilia uvunjwaji wa aina yoyote wa sheria na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua stahiki.
Majibu ya Polisi
Wakati mawaziri wakijibu hivyo, taarifa iliyotolewa na Polisi leo kupitia msemaji wake, David Misime imeeleza uchunguzi unaendelea vizuri na wananchi waendelee kuwa na subira.
Katika taarifa hiyo, Misime amesema, “Taarifa itatolewa baada ya kukamilisha yale ambayo sheria za nchi zinaelekeza.”
“Jeshi la Polisi linatoa wito sote kwa pamoja tuendelee kutafakari namna tunavyoendelea kujadili jambo hili na tunavyotoa maoni kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari je, hatuendelei kumtonesha huyu binti majeraha aliyonayo moyoni? Je, kwa kuendeleza hayo, familia yake hatuendelei kuijeruhi kisaikolojia?” amehoji Misime.
Amesisitiza mwenye taarifa ya ziada aziwasilishe kwa njia sahihi kwa kutumia mifumo iliyopo, bila kuendelea kumuumiza muathirika.
Tangu kusambaa kwa video hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kililaani tukio hilo, kikimtaka Rais Samia Suluhu Hassan atoke hadharani kukemea ukatili huo na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camilius Wambura achukue hatua za haraka hadi kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kupitia taarifa iliyotolewa na rais wake, Boniface Mwabukusi kililaani tukio hilo kikieleza kinaendelea kufuatilia kwa karibu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha hatua stahiki kwa waliohusika zinachukuliwa.
Pia wakili Peter Madeleka kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani twitter), aliahidi kuingilia tukio hilo na kuchukua hatua za kisheria, iwapo mamlaka hazitafanya hivyo ndani ya saa 24 tangu lilipotokea.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesisitiza aliyewatuma pia anapaswa akamatwe.
Kwa mujibu wa Henga, kilichofanyika ni kosa la jina na katika jinai, aliyewaza na aliyetenda wote wanakuwa na kosa linalofanana.
“Kiu yetu ni kuona aliyewatuma, huyo aliyemuita afande naye anakamatwa kwa sababu amefanya kosa lilelile kama walilofanya hao vijana walioonekana kwenye video,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa sababu jamii inaonyesha kukerwa zaidi na tukio hilo, isiwe shinikizo la watuhumiwa hao kufanyiwa ukatili wakati wa mahojiano.
“Wanapaswa kuhojiwa kawaida kama inavyofanyika kwa watuhumiwa wengine na isitokee tena na wao wakafanyiwa ukatili kama ambavyo wao wamefanya ukatili.
“Kuna watu wanasema wanyimwe dhamana, hiyo ni haki yao kwa sababu kosa lao linadhaminika, isipokuwa wafanyiwe hivyo kama itaonekana kuna hatari ya usalama wao,” amesema.
Amesisitiza jambo muhimu ni kuhakikisha hatua za kisheria zinafanyika na wahukumiwe kama inavyopaswa kwa mujibu wa sheria.
Juhudi za kumtafuta msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) zimeshindikana baada ya simu yake kuita mara kadhaa bila kupokewa.
Jumapili ya Agosti 4, 2024, Meya wa zamani wa Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob katika ukurasa wake wa X alielezea tukio hilo na kuwaomba viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuchukua hatua.
Pia alimuomba Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax kuingilia kati suala hilo.
“Kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ni mama, Waziri wa Ulinzi ni mama, Waziri wa Wanawake ni mama tunatarajia kuona wakichukizwa zaidi juu ya udhalilishaji na ukatili juu ya mtoto wa kike, wao wakiwa kama wazazi na viongozi wenye dhamana ya kulinda raia wa Tanzania,” aliandika Jacob.
Akitoa maoni katika andiko hilo la Jacob, Waziri Gwajima aliandika: “Salaam. Ahsante sana kuniTag. Nimesoma na kuwasilisha kwenye mamlaka yenye dhamana ya kuchunguza na kukamata ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Watatoa taarifa kwa nafasi yao.”
“Aidha, kwa namna yoyote ile, taarifa hii inasikitisha na jambo kama hili halifai, ni la kulaaniwa na haliwezi kufumbiwa macho. Iwapo manusura au aliye karibu naye atasoma hizi taarifa wasiogope, watoe taarifa ili manusura apate msaada haraka, ikiwamo huduma za afya, kisaikolojia na usalama.”
Muda mfupi baadaye, Misime alitoa taarifa kwa umma kuzungumzia tukio hilo, akisema wameanza kulifanyia kazi na kulaaniwa, kwa kuwa halikubaliki na ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na haki za binadamu.