Uwekezaji wa ghorofa za PSSF waendeshwa kwa hasara

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imeonyesha kuwepo kwa hasara katika uendeshaji wa majengo yaliyowekezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Miongoni mwa majengo hayo ni Jengo la Golden Jubilee lililopo jijini Dar es Salaam lililotumia Sh226.97 milioni kwa ajili ya uendeshaji, huku makusanyo ya ada ya huduma yakiwa Sh196.73 milioni.

Jengo jingine ni la Twin Tower pia la Dar es Salaam, ambalo pia limetumia Sh245.65 milioni kwa ajili ya kugharimia uendeshaji, huku makusanyo yatokanayo na ada ya huduma yakiwa Sh96.81 milioni.

PSSSF pia imepata hasa katika majengo yake ya Kaloleni apartments, Mikocheni appartments, huku ikipata faida kwenye majengo ya Masaki apartments na PSSF International House.

Hasara nyingine imeonekana katika jengo la Quality Plaza, Samora House, jengo la Sokoine Mtwara, Jacaranda, Haile Selassie, Millenium Tower II, Victoria house, PSSSF Comercial Complex, PSSSF Arusha House na PSSSF Victoria House.

“Ongezeko la gharama za uendeshaji wa majengo zilisababishwa na ukusanyaji usioridhisha wa ada za huduma na kupungua kwa idadi ya wapangaji katika majengo.

“Ukaguzi ulichambua katika mwaka wa fedha wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma kuanzia mwaka 2018/19 hadi 2020/21 na ulibaini kuwa uwekezaji wa majengo ulikuwa na wastani wa faida ya chini katika uwekezaji kwa asilimia 2.66, ikilinganishwa na asilimia 2.67 ya uwekezaji katika hisa na asilimia 9.28 ya Soko la Fedha,” imesema ripoti ya CAG.

Kwa upande mwingine, ripoti hiyo imebaini kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu haikufanya ukaguzi wa uchunguzi kwa PSSSF wala Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mwaka 2021/22, huku mwaka 2020/21 ikifanya ukaguzi na uchunguzi kwa PSSSF peke yake.

“Zaidi ya hapo, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu haikuweza kutekeleza shughuli za ufuatiliaji kama inavyopaswa kwa kipindi kilichokaguliwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 mpaka 2021/22,” imesema ripoti hiyo.

Mmoja wa maofisa ngazi za juu PSSSF ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kwa sasa anayeweza kuzungumzia suala hilo ni Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati wa kujibu ripoti hiyo bungeni.

Hata hivyo alidokeza, kuna jitihada mbalimbali zimefanyika kuhakikisha uwekezaji walioufanya unakuwa na tija kwa wanachama.

“Kuanzia mwaka jana hadi sasa kuna maendeleo makubwa tumepiga, uwekezaji tulioufanya unaanza kukua taratibu, tusubiri wakati wa kujibu hoja,” alisema.