Viongozi wapya Chadema waahidi ushindi Serikali za mitaa

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, Henry Kilewo aliyeibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Wenyeviti wapya wa Chadema mikoa ya Kinondoni, Ilala na Ubungo wamesema wanajipanga kuhakikisha wananyakua mitaa mingi katika uchaguzi wa Serikali.

Dar es Salaam. Wenyeviti wapya wa mikoa ya kichama wa Chama cha Demokrasia na  Maendeleo (Chadema) Ubungo, Kinondoni na Ilala wamesema kipaumbele chao ni kuhakikisha chama hicho kinanyakua viti vingi vya Serikali za mitaa katika maeneo yao.

Wamesema hayo leo Jumamosi Aprili 6, 2024 wakizungumza na Mwananchi Digital baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi ulioanza kufanyika Aprili 2 hadi 5 katika mikoa hiyo ya chama hicho.

“Shabaha yangu ni kuhakikisha tunakwenda kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa Mkoa wa Kinondoni, sambamba na kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka kesho,” amesema Henry Kilewo ambaye ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kinondoni.

Kilewo amesema katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa viongozi wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, wataanza operesheni ya kushuka chini kwenye mitaa 106 kwa lengo la kuonana na wananchi na viongozi wa chama hicho.

“Mkakati wetu ni kufanya ziara ya kushuka chini kuonana na wananchi kuwaonyesha ili wawajue mapema wagombea wetu wa Serikali za mitaa ambao wameshatia nia ya kuwania nafasi hiyo,” amesema Kilewo.

Maelezo ya Kilewo hayakuwa mbali na mwenyekiti mpya wa Chadema Mkoa wa Ilala, Waziri Mwenyevyale amesema mkakati wao ni kuwaunganisha wanachama wa chama hicho kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Nikishirikiana na viongozi wenzangu tutafanya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mapema ili kuhakikisha tunapambana na kushinda katika uchaguzi huu.

“Tunajiandaa mapema ili tuwe tayari kwa uchaguzi huu utakaofanyika mwisho mwaka huu, kwa umoja wetu ili tutalifanikisha,” amesema Mwenyevyale.

Mwenyekiti wa Chadema Ubungo, Amos Maziku amesema malengo yake ni kuchukua majimbo mawili ya mkoa huo, udiwani wa kata 14 na viti vya Serikali za mitaa katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu.

“Uchaguzi wa Serikali za mitaa ni muhimu kwetu kwa sababu ndio unatuwekea msingi katika chaguzi zingine, tunataka tushinde kwa asilimia 90.

“Chama kipo kila sehemu kuanzia ngazi za mitaa, tutahakikisha tunawapelekea viongozi bora waliopikwa na watakaoleta ushindani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, naamini tutafanikiwa namuomba Mungu atusaidie,” amesema Maziku.

Katibu wa Kanda ya Pwani inayounda mikoa hiyo, Jerry Kerenge ameliambia Mwananchi kuwa Kileo na Maziku wamefanikiwa kutetea nafasi zao katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, Kerenge  amesema mikoa ya chama ya Temeke, Pwani Kusini (Mkuranga, Rufiji, Kibiti na Mafia) na Pwani Kaskazini (Chalinze, Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha), ndio imebaki kukamilisha mchakato huo.

“Mikoa iliyobaki ikikamilisha chaguzi tutaamia ngazi ya kanda,” amesema Kerenge.

Katika uchaguzi huo, Kerenge amesema wajumbe waliwachagua makatibu wa mikoa ya Ilala, Kinondoni na Ubungo wanaosubiri kuthibitishwa kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.

“Katika Mkoa wa Kinondoni, aliyeshinda ni Dani Mtanga, Ubungo (Pollyn Msofe) na Ilala Jerome Ulomi wanaosuburi mchakato wa kuthibitishwa,”amesema Kerenge.