Kigogo wa zamani CWT ashinda uenyekiti Chadema
Muktasari:
Rais wa zamani wa Chama wa Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba ameshinda uenyekiti wa Chadema mkoani wa Kagera huku akianisha mambo sita atakayosimamia katika utekelezaji wa majukumu yake
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuchaguliwa uenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kagera, bosi wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba amesema ataanza na mambo sita ikiwamo kuamsha ari ya wanachama wa chama hicho.
Mengine amesema ni masuala ya kikokotoo, Katiba mpya, Tume huru, bima ya afya na elimu atakayoyatekeleza kwa ushirikiano na viongozi wenzake wa mkoa na Taifa wa Chadema.
Jana, Jumapili Machi 24, 2024 Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alimtangaza Mkoba kushinda nafasi hiyo, baada ya kupata kura za ndio 50 kati ya 55 za wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
Katika uchaguzi huo uliowachagua pia viongozi wa mabaraza ya wazee, vijana na wanawake wa chama hicho pamoja na katibu mkuu wa mkoa, Mkoba alikuwa mgombea pekee wa uenyekiti baada ya mshindani wake Justus Basheka kuenguliwa na kamati ya usahili kwa sababu mbalimbali.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Machi 25, 2024 Mkoba aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), amedai kuwa demokrasia ilipominywa miaka kadhaa iliyopita ilishusha morali ya wanachama wa chama hicho mkoani humo sasa anakwenda kuirejesha.
“Nataka wanachama wa Chadema wa Mkoa wa Kagera wakipende chama hiki kwa moyo wote kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita, nitakwenda kuifanya kazi hiyo,” amesema Mkoba.
Mkoba amesema ataisimamia vema ajenda ya Chadema ya kupata Katiba mpya, akipingana na Serikali iliyotaka mchakato huo ufanyike baada ya kufanya utafiti ulionekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu Katiba hata wengine hawajahi kuiona.
Hatua hiyo, ya Serikali ilipingwa na wadau wa demokrasia ya vyama vingine waliosema kitendo cha Katiba mpya kupatikana baada ya miaka mitatu ni kupoteza muda.
“Hatuhitaji watu kufundishwa kuhusu Katiba mpya kwa miaka mitatu, hii sio sahihi naungana na Chadema kuwa mchakato huo ufanyike sasa, nitasimamia upatikanaji wa Tume huru ya uchaguzi,” amesema Mkoba.
Mbali na hilo, Mkoba amesema suala la kikokotoo bado ni changamoto kwa watumishi wa umeme, akisema kinawanyima mafao yao na kuitaka Serikali iangalie upya mchakato kazi ataisimamia kwa kusuka ajenda hiyo.
Mkoba amesema atasukuma ajenda ya elimu na bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kunakuwa na uboreshaji katika sekta hizo kwa lengo la kuwahudumia Watanzania.