Wakusanya ushuru wa maegesho Dar wagoma

Dar es Salaam. Makusanyo ya maegesho ya magari jijini Dar es Salaam yanayokadiriwa kufikia Sh 25 milioni kwa siku huenda yakatoweka kutokana na mgomo wa wakusanya ushuru huo kutoka kampuni ya Excel Parking Service (EPS).

Wakusanya ushuru hao wamegoma wakidai kutolipwa mishahara yao miezi miwili.

Tofauti na ilivyozoeleka katika maeneo ya jiji hilo ambayo awali watu walikuwa wakitozwa Sh500 kwa saa kwa ajili ya maegesho, tangu juzi wakusanyaji walikuwa hawafanyi kazi yao, badala yake walikusanyika katika baadhi ya mitaa na kukaa pamoja.

“Tangu jana hatujafanya kazi, tupo hapa tunakusanyika kusubiri hatima yetu, tuna madai yetu lakini pia na kazi yenyewe kama inaelekea ukingoni,” alisema mmoja wa watoza ushuru aliyekuwa amekusanyika na wenzake ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mathayo Nungu alisema kusimama kwa shughuli hizo za ukusanyaji wa ushuru ni hasara kwa kampuni yake, Serikali na hata wafanyakazi waliokuwa wakitoza ushuru huo.

“Mimi sijalipwa na mwajiri wangu kwa miezi minne, nami sijawalipa wafanyakazi wangu kwa miezi zaidi ya miwili, ndiyo maana wamegoma kufanya kazi kwa siku hizi, lakini natumai nitafikia mwafaka na mwajiri wangu na kazi zitaendelea,” alisema Nungu, na kuongeza kwa wastani kampuni yake hukusanya Sh25 milioni kwa siku.

Alisema kampuni hiyo hulipwa kamisheni kutoka kwenye kiwango ilichokusanya ambayo nayo huitumia kulipa wafanyakazi wake na kugharimia gharama nyingine za undeshaji wa ofisi. Alipotafutwa na gazeti hili ili kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri alisema mtoa huduma huyo hana mkataba nao, hata hivyo alisema yupo kikaoni hivyo atafutwe mwanasheria wa halmashauri.

Kwa upande wake, mwanasheria huyo, Florah Luhala alisema mpaka jana kati ya mashine 122 zilizokuwa zikitumiwa na kampuni hiyo kukusanya tozo ya maegesho, halmashauri imezipata 11 tu na zenyewe zimeshaanza kazi.

“Mkataba wake uliisha tangu Desemba mwaka jana, lakini hajakabidhi mashine zetu licha ya kumjulisha kwa barua na kutakiwa kufanya hivyo. Miongoni mwa barua tulizomwandikia ni kumfahamisha kuwa hatuna nia ya kumuongeza mkataba lakini bado ameng’ang’ania, ndiyo maana leo (jana) tumeamua kuifungulia kesi kampuni hiyo,” alisema Luhala.

Alisema tayari jiji limeshafanya usaili na kupitisha watu 65 wa kufanya kazi hiyo na kinachosubiriwa sasa ni mashine tu lakini hata hizo 11 zilizopo tayari zimeanza kazi.