Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Waliopata ujauzito kurejea shule itoe ufafanuzi’

Muktasari:

  • Novemba 24, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na miezi minane tangu aingie madarakani alitangaza uamuzi wa Serikali kuruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito.

Dar es Salaam. Baada ya kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu mpango wa Serikali kuuweka kisheria uamuzi wa kuwarejesha shuleni wasichana wanaopata ujauzito, wadau wa elimu wametaka sheria itakayoandaliwa itoe ufafanuzi wa kina wa mambo muhimu yanayoonekana kuwa kikwazo tangu kuanza utekelezaji wa sera hiyo.

Novemba 24, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na miezi minane tangu aingie madarakani alitangaza uamuzi wa Serikali kuruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito.

Uamuzi huo ulifuatiwa na Wizara ya Elimu kupitia Kamishna wa Elimu, Dk Lwayebe Mutahabwa kutoa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, bado kuna kundi kubwa la wasichana waliojifungua wanashindwa kurejea shuleni kutokana na vikwazo vya kimazingira ikiwamo kuzuiwa na wazazi, kukataliwa shuleni, unyanyapaa na umasikini.

Mei 23, 2024 akizungumza bungeni Majaliwa amesema miongoni mwa maeneo watakayoyafanyia kazi katika mapitio ya sera ya elimu ni kuimarisha maelekezo yatakayokwenda kutunga sheria na kanuni ya namna wanafunzi wanaokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito wanavyoweza kurudi shuleni.

“Suala hili halitakuwa ni matakwa ya mtu, litakuwa matakwa ya kisheria na kanuni. Japo mamlaka za mikoa, wilaya zinaendelea kufuatilia kuhakikisha wanarudi shuleni, muhimu zaidi ni pale wanapokwenda kuliwekea kisheria lisiwe hiari ya mtu yeyote katika kulitekeleza,” amesema Majaliwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 24, 2024 aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dk Avemaria Semakafu amepongeza hatua ya Serikali kuliweka suala hilo kisheria, hata hivyo amesema limechelewa.

“Uamuzi ulitolewa na Rais na pindi kiongozi mkuu wa nchi anapotoa uamuzi wa aina hii ilitakiwa utekelezaji wake uanze mara moja, wizara husika ilipaswa kufanyia marekebisho sheria iliyokuwa ikizuia,” amesema.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Martha Makala amesema uamuzi wa kutengeneza sheria umekuja wakati muafaka, ikizingatiwa kuna wakuu wa shule wanawazuia wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni.

“Kwa sababu hili ni jambo la kisera ni muhimu kuwa na sheria na wito wetu kwa wizara, mchakato wa kutengeneza sheria uanze mara moja na ushirikishe wadau kwa pamoja tukae tuje na sheria na kanuni itakayowaondolea vikwazo wanaokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito,” amesema.

“Uwepo wa sheria utarahisisha mchakato uliowekwa kwenye mwongozo wa kuwarejesha shuleni, kwa kuwa sasa bado kuna watu wanaokwamisha. Kuna viongozi, wakuu wa shule, walimu wanaotoa kauli za udhalilishaji kwa mabinti hawa,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema sheria iweke hatua za kuchukua kwa mzazi anayekwamisha mtoto kurejea shuleni.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema hatua hiyo itahakikisha uamuzi huo siyo utashi wa kiongozi aliye madarakani bali ni suala la kisheria na utekelezaji wake unapaswa kusimamiwa kikamilifu.

Mkurugenzi huyo ambaye pia ni mwanasheria amesema ni muhimu sheria ikabainisha vipaumbele vya kibajeti ili kuwezesha mambo yanayoendana na utekelezaji wa mpango huo wenye lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.

“Ni muhimu kwenye sheria ionekane utaratibu wa kumuondoa na kumrejesha shuleni aliyepata ujauzito, isiwe amegundulika leo halafu anafukuzwa shuleni. Kama ujauzito wake ni mdogo aachwe hadi pale atakapokaribia kujifungua ndiyo aondoke,” amesema.

“Sheria ionyeshe huduma atakazopata aliyejifungua na kurejea shuleni, katika hali ya kawaida ni lazima apate huduma za unasihi ili kumuweka sawa. Pia, ionyeshe mtoto atakayezaliwa atapata huduma zipi, hapa tunazungumzia vituo vya kulelea ili mama apate muda wa kumnyonyesha akiendelea na masomo,” amesema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema sheria ielekeze kutengwa bajeti ya maeneo maalumu kwa ajili ya kunyonyeshea shuleni.

Pia, iweke ujinai kwa watakaowanyanyapaa wasichana hao kwa kuwa taarifa zinaonyesha wengi wanakwepa kurudi shuleni kutokana na vitendo vya unyanyapaa.

Ripoti ya utafiti iliyofanywa na Shirika la Hakielimu katika mikoa 12 inaonyesha kwa kiasi kikubwa unyanyapaa unafanywa na walimu wakuu wa baadhi ya shule huku kukiwa na vitendo vya udhalilishaji wa mabinti wanaojaribu kurejea shuleni.

Katika utafiti huo asilimia 61.2 ya wahojiwa walieleza wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya udhalilishaji wanaokutana nao wakiitwa majina yasiyofaa na yanayokatisha tamaa.

Asilimia 53.2 walieleza licha ya shauku waliyonayo ya kurejea shuleni wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutolewa mfano kila wakati.