Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaopata ujauzito kutungiwa sheria kurejea shule

Muktasari:

 Leo Alhamisi, ilikuwa kipindi cha maswali na majibu papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, ambaye ameulizwa maswali mbalimbali juu ya sekta ya elimu ikiwemo mkakati wa Serikali kuhakikisha wanafunzi wanaopata ujauzito wanarejea shule kwa lazima na si hiari.

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatunga sheria na kanuni ili suala la kurejea shule kwa wanafunzi waliopata ujauzito lisiwe hiari ya mtu.

Juni 2017, Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli alipiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba shuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari.

Rais Magufuli alisisitiza ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shuleni, kauli iliyozua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi.

Hatua hiyo ilikuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wanaharakati na baadhi ya mashirika kutoka nje ya nchi, kuishauri Serikali kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni katika mfumo rasmi.

Hata hivyo, Novemba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni miezi takribani nane tangu alipoingia madarakani, alitangaza uamuzi wa Serikali kuruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni.

Samia, aliyekuwa Makamu wa Rais aliingia madarakani Machi 19, 2021 ikiwa ni siku mbili kupita tangu Dk Magufuli aliyekuwa Rais kufariki dunia Machi 17.

Alichosema Majaliwa

Lakini leo Alhamis Mei 23, 2024 wakati maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma, limeibuka swali hilo lililoulizwa  na Mbunge wa Viti Maalum, Asia Halamga.

Asia aliuliza: Rais Samia Suluhu Hassan aliamua watoto waliopata mimba warejee shuleni na kuendeleza programu za kuwaendeleza waliopata ujauzito.Lakini zoezi hilo linasuasa, je Serikali italeta lini bungeni hili jambo lisiwe hiyari na liwe la lazima?

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema Serikali inapitia eneo la uwepo wa tofauti ya idadi ya wanaoanza shule na wale wanaomaliza pamoja na wanaokwama kutokana na kupata ujauzito.

Amempongeza Rais Samia ambapo katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitatu kati ya mambo makubwa aliyoyafanya, ni kuelekeza ni lazima uratibu ufanyike kwa watoto wote waliopata ujauzito wakiwa shuleni ili warejee shuleni.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto walizonazo katika maisha yao.


Amesema sasa hivi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya mapitio ya sera yake.

Amesema miongoni mwa maeneo ambayo wataiweka na kuyafanyia kazi ni pamoja na kuimarisha maelekezo ambayo yatakwenda kutunga sheria yake na kanuni ya namna ya watoto waliopata ujauzito wakaacha shule,  wanavyoweza kurejea shuleni.

“Sasa suala hilo halitakuwa ni matakwa ya mtu, litakuwa ni matakwa ya kisheria na kanuni. Nataka nimhakikishie mheshimiwa mbunge, Serikali inaendelea kulifanyia kazi kwa mabadiliko ya sera ya elimu yanayoendelea na moja kati ya kipengele itakuwa ni hicho,” amesema.

Amesema japokuwa mamlaka za mikoa, wilaya zinaendelea kufuatilia kuhakikisha wanarudi shuleni,  muhimu zaidi ni pale ambapo wanakwenda kuliwekea sheria ili jambo hili lisiwe hiari ya mtu yeyote katika kulitekeleza.

“Niwahakikishie mabinti zetu wanaopata ujauzito watapata nafasi ya kuendelea na masomo ili watimize ndoto zao kuendelea na masimo,” amesema.

Ripoti ya HakiElimu

Wakati Majaliwa akieleza mkakati huo, ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Hakielimu katika mikoa 12 ulionesha wasichana wengi wanashindwa kurejea shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo unyanyapaa.

Ripoti hiyo inaonesha kwa kiasi kikubwa unyanyapaa huu unafanywa na walimu wakuu wa baadhi ya shule, huku kukiwa na vitendo vya udhalilishaji wa mabinti wanaojaribu kurejea shuleni.

Katika utafiti huo uliofanyika mwaka 2023 asilimia 61.2 ya wahojiwa,  walieleza wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya udhalilishaji wanaokutana nao wakiitwa majina yasiyofaa na yanayokatisha tamaa.

Asilimia 53.2 walieleza licha ya shauku waliyonayo ya kurejea shuleni, wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutolewa mfano kila wakati.

Walimu wakuu wametajwa pia katika utafiti huo kuchangia mabinti waliopata ujauzito wasirejee shuleni, kwa kile kilichoelezwa wanawakataa kwa hofu ya kuwaharibu wanafunzi wengine.

Kufuatia hali hiyo wito umetolewa kwa Serikali kuweka mkazo kwenye utekelezaji wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.

Mwongozo huo ulitolewa Februari 2022, ulilenga kuwezesha urejeshwaji wa wanafunzi waliokatiza masomo katika shule za msingi na sekondari, kushirikisha wadau kuhusu waibu wao katika kuwarejesha wanafunzi waliokatiza masomo baada ya Serikali kuruhusu kurejea shuleni.

Mtafiti Dk Joyce Mbepera amesema utafiti huo ulibaini kuwa wapo wakuu wa shule wanaokataa kuwapokea wanafunzi walijifungua,  licha ya mwongozo kuwapa jukumu la kuhamasisha wasichana waliopata ujauzito baada ya kujifungua.

Dk Joyce amesema utafiti huo ulibaini kuwa walimu wengi wakiwemo wakuu wa shule hawana uelewa wa kutosha kuhusu mwongozo huo.


Wanaokacha masomo

Katika swali lake kwa Majaliwa, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda,  amesema pamoja na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu, matokeo ya wanafunzi wanaosajiliwa darasa la kwanza na wale wanaomaliza la saba wachache na hali iko hivyo hivyo hata kwa wanaomaliza sekondari.

“Serikali ina mkakati gani angalau wale wanaoanza shule wote wamalize?”amehoji Kakunda.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema ni kweli kwenye sekta ya elimu Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa kujenga miundombinu kutoka ngazi ya awali hadi vyuo vikuu.

Amesema wameanza kushuhudia watoto wengi wa Kitanzania wakipata nafasi za kusoma kwenye ngazi za awali, shule ya msingi na sekondari.

“Nikiri idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kuanza masomo sio sawa na wanaomaliza  kuanzia msingi na hata sekondari na  hasa kidato cha kwanza hadi cha nne. Kwa kidato cha tano hadi cha sita kuna unafuu kidogo. Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio katika ngazi zote,”amesema.

Amesema wanaendelea kuzungumza na jamii hasa wazazi kuhakikisha kila mzazi anasimamia mahudhurio ya mtoto kwenda shule, kuingia darasani na anaporudi kufuatilia mwenendo wa mtoto shuleni.

Amesema hatua zinazochukuliwa ni kuimarisha mabweni ya wanafunzi na hivyo kupata usimamizi wa maadili.

Majaliwa amesema wanatambua kuna utoro na mimba kwa wanafunzi wao, lakini kujenga mabweni kuitasaidia zaidi kuhakikisha kuwa wanawalinda.

Hatua nyingine ni kuimarisha sheria za kudhibiti utoro hasa kwa wazazi ambao wana wajibu wa kuwalea watoto hao.

“Tumetoa maelekezo katika ngazi za wilaya ambako kuna shule za msingi na sekondari, tumetoa maelekezo kwa mkoa kufanya ufuatiliaji na tumeimarisha pia ukaguzi kupitia taasisi yetu ya uthibiti ubora,” amesema.

Amesema miongoni mwa kazi inayofanywa na  wathibiti ubora ni kuhoji wanafunzi waliosajiliwa ili wapate sababu za wanafunzi wengine kutokuwepo darasani kulinganisha na usajili uliofanyika.

Amesema wanaamini hatua hizo wanazozichukua, zitapunguza utoro na hivyo zaidi ya asilimia 95 hadi 98 watakaosajiliwa kuanza shule, watamaliza shule.

Mabasi ya shule

Mbunge wa Viti Maalum, Nancy Nyalusi yeye amemuuliza Majaliwa akisema ukuaji sekta ya elimu na ongezeko la shule binafsi limefanya ongezeko la mabasi ya shule kuwa mengi.

“Serikali haioni haja kutunga sheria ya usalama kwa magari yote yanayobeba wanafunzi?” amehoji Nancy.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema kuna sheria za usalama wa vyombo vya moto vyote na sheria zinazotakiwa kufuatwa kwa ajili ya usalama wa watoto.

“Kwenye school bus (mabasi ya shule), tumeongeza kanuni zinazobana wamiliki wa shule kuwa lazima kuwe na dereva mwenye sifa ya kubeba watoto. Basi lazima lipakwe rangi ya njano na liwe na maandishi ya school bus,”amesema.

Majaliwa amesema kila basi linapofanya safari ni lazima liwe na walezi wawili mwanamume na mwanamke.

“Kunapotokea dharura mtoto wa kike ahudumiwe na mwanamke na kiume hivyo hivyo. Tunafuatilia sheria zote tulizoweka kwa school bus hizi,” amesema.