‘Wanawake wananyanyaswa kingono wakitafuta fedha za marejesho’

Muktasari:

Kwa mujibu wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Kamona Stanley wanawake wengi (bila kutaja idadi) wamekumbana na unyanyasaji wa kingono wakitafuta fedha za marejesho ya mikopo umiza, nyonya damu na mtoto wa shetani.

Mwanza. Wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagiza kurejeshwa kwa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Kamona Stanley amesema wanawake wengi (bila kutaja idadi) wamekumbana na unyanyasaji wa kingono wakati wakitafuta fedha za marejesho ya mikopo umiza, nyonya damu na mtoto wa shetani.

Jaji Stanley ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 25, 2023 kwenye uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili mkoani Mwanza uliofanyika Igoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali likiwemo Dawati la Jinsia, Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini na wakazi wa Mwanza.

Jaji huyo amewataka watunga Sera kuja na muongozo utakao rahisisha upatikanaji wa mkopo kwa wanawake na makundi maalum ili kuwaepusha kuwa sehemu ya ukatili kwa kisingizio cha utafutaji huku akiwataka wanawake kufuata mfumo rasmi wa kupata fedha ili kuepuka ukatili wa aina hiyo.

“Akina mama wengi wamekuwa na changamoto ya ukosefu wa nguvu ya kiuchumi matokeo yake wamekuwa wakinyanyaswa kijinsia. Nitoe wito kwa wadau kurekebisha na kutoa wepesi kwa wanawake katika utoaji wa mikopo ili kuwaepusha na mikopo umiza, kausha damu na mtoto wa shetani,” amesema Jaji Stanley

“Lazima tuseme ukweli dada zetu wamekuwa wakinyanyaswa kingono kwa sababu ya kutafuta marejesho ya mikopo kwa hiyo ni vema watunga sera wakaangalia namna bora ya kukomesha mikopo hiyo kwa kutoa mikopo inayolipika, litakapowezekana hili tutatokomeza ukatili wa kijinsia,”amesema

Kuhusu mapambano ya ukatili dhidi ya watoto, Jaji Stanley amesema miongoni mwa vikwazo vya mapambano dhidi ya ukatili ni pamoja na tabia ya baadhi ya watu katika jamii kuwa wepesi kusambaza umbeya na picha za ngono ‘connection’ kuliko kuripoti visa vya ukatili vinavyotokea katika maeneo yao.

“Tumekuwa watu wa kwanza kushabiki vitendo vya ukatili wa kijinsia, juzi kuna tukio moja la mtoto amerekodiwa kama msalabani anachapwa halafu kuna mjinga mmoja anarekodi halafu analisambaza sasa unajiuliza huyu jamaa kama anarekodi kisha anasambaza ameshindwa nini kwenda kuliripoti,” amesema Jaji Stanley

Amesema kutokana na mwitikio mdogo wa jamii kuripoti visa hivyo, jitihada za kuyatokomeza zimekuwa zikigonga mwamba na kusema endapo taarifa sahihi zikitolewa kwa wakati sahihi huenda ukatili ukatokomezwa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini, Yassin Ally amesema mwenendo unaonyesha kupungua kwa vitendo vya ukatili katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku akisisitiza kuwa jitihada za ziada zinahitajika kukomesha ukatili nchini.

“Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa Kivulini tumepita kutoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia tunashukuru takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa zinaonyesha kiwango cha mimba za utotoni na matukio ya ukatili kimepungua katika mikoa hii,” amesema Ally

Ametaja changamoto za kukomesha ukatili nchini ni pamoja na ufanikishaji mdogo wa mashauri ya ukatili, watu kutojitokeza kutoa ushahidi wao mahakamani huku akishauri mkakati mahsusi kuwekwa ili kukabiliana na changamoto hizo.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila amesema mkoa huo umetengeneza timu maalum itakayopita maeneo mbalimbali kutoa elimu ya msaada wa kisheria na kuongeza uelewa kwa Umma kwa siku 16 ili kuwezesha jamii kutokomeza ukatili wa kijinsia.

“Tuna ukatili wa kimtandao pengine hatujui athari zake napengine sisi ni wa kwanza kusambaza ukatili huo. Tutafika katika shule, taasisi za Umma na kutumia mahakama inayotembea kutoa elimu hiyo, pia tutakuwa SAUT kwa siku mbili kutoa elimu hii wote mnakaribishwa kujifunza,” amesema Shishinila