‘Wanywaji juisi ya miwa chukueni tahadahari’

Dar es Salaam. Biashara ya juisi ya miwa inazidi kushamiri katika maeneo ya mikusanyiko ya watu, kama vituo vya mabasi na masoko.

Licha ya juisi hiyo kutajwa kuwa na faida kwa mwili wa binadamu, watumiaji wanapaswa kuzingatia usalama wao kabla ya kuitumia.

Hii ni kutokana na watengenezaji wengi kutozingatia usafi katika maeneo yao ya biashara, mwili, mavazi au vifaa. Pia baadhi huhifadhi miwa sehemu ambayo si salama kwa afya.

“Kwa kweli napenda juisi ya miwa, lakini lazima nimkague kwanza mtengenezaji kama amevaa glovu, jinsi anavyoweka miwa na hata vyombo anavyotumia,” anasema Martha John, mkazi wa Tabata Kinyerezi.

“Baadhi wamekuwa wakishika miwa mikono isiyo safi; mara ameshika hiki mara ameshika muwa bila kunawa, glasi haoshi vizuri. Sasa hapo badala ya kupata faida za juisi, unaweza kupata maambukizi ya magonjwa.”

Mkazi mwingine, Juliana James anasema utengenezaji juisi hizo kwa baadhi ya watu umekuwa haujali afya.

“Niko radhi nitafune muwa kuliko kukamuliwa. Niliwahi kuona mtengenezaji wa juisi kaiweka miwa sehemu chafu halafu anachukua mmoja baada ya mwingine na kuikwangua kigamba kidogo cha juu na kusaga,” alisema.

“Niliwaza mengi, lakini nikaona bora nisiwe nakunywa maana hata ndoo ambayo juisi hiyo ilikuwa inaingia duh, hapana kwa kweli.”

Hata ambaye anapulizia dawa kuua wadudu kama inzi, bado anatia shaka wateja kama Esry Soud alivyoona.

“Nilishtuka, lakini baadaye niligundua kuwa eneo hilo limepuliziwa dawa ya kuua wadudu. Niliwaza kuwa itakuwaje kama imeingia katika juisi au ilipuliziwa katika miwa na ikasagwa bila kuoshwa, niliogopa,” anasema Soud.

Dk Zacharia Kabona kutoka Hospitali ya AAR alisema kuna uwezekano mkubwa kwa watengenezaji wa juisi ambao hawatumii glovu, kuhamishia vijidudu kwenda kwenye kinywaji.

“Wakati mwingine yeye mwenyewe ndiyo huwa mgonjwa na akitoka kujisaidia haoshi mikono yake vizuri sasa kupitia yeye ndiyo wadudu wale wataweza kusambaa kwenda kwa wengine,” alisema.

“Hapo ndiyo tutakutana na shida za maradhi ya tumbo, kuharisha, vidonda vya tumbo, kipindupindu, amoeba au typhoid kutokana na uchafu wa mikononi.

“Pia, hata kama hawana maambukizi huweza kuhamisha vijidudu kutoka sehemu mbalimbali kama hawataosha mikoni yao vizuri.”

Akizungumzia suala la kupulizia dawa za kufukuza na kuua nzi, Dk Kabona alisema dawa hizo hutengenezwa kwa viambata sumu ambavyo huweza kuleta athari kwa binadamu kama akiitumia kwa kiasi kikubwa.