Wataka kasi ya Mwendokasi idhibitiwe, bodaboda wafuate sheria

Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu akizungumza leo Aprili 1, 2024 kuhusu maombi ya wananchi Kata ya Kisutu kuhusu kudhibiti ajali za barabarani.
Muktasari:
- Uendeshaji wa kasi wa mabasi ya yaendayo haraka, bodaboda kutofuata sheria na kutokuwepo kwa taa za barabarani vimetajwa kuongeza ajali zinazotafuna maisha ya watu kila kukicha.
Dar es Salaam. Wakazi mtaa wa Mtendeni Kata ya Kisutu wameitaka Serikali kuwawekea taa na kutoa elimu ili kudhibiti ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara katika jiji hilo.
Ajali hizo zimetajwa kusababishwa na kutofuatwa kwa sheria kwa watumiaji wakiwemo waendesha bodaboda na uendeshani magari kwa mwendo kasi.
Akizungumza na waandishi kwenye kikao kilichowakutanisha viongozi wa mtaa wa Mtendeni, Mbunge wa Ilala Mussa Zungu na wananchi, Jumatatu Aprili mosi, 2024, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtendeni Kata ya Kisutu, Mustakim Darugar amesema mtaa huo hauna taa, jambo ambalo limekuwa ni chanzo cha ajali nyingi.
“Mtaa huu una watu wengi, kuna umuhimu kuwekwa taa kwenye barabara zake, kwa sasa wananchi wameamua kuchangia kuziweka kunusuru maisha ya wengi,” amesema Darugar.
Amesema elimu inahitajika kwa watumiaji wa barabara zote za ushoroba wa mabasi yaendayo haraka (BRT), hususani kwenye makutano ya barabara hizo, wafuate sheria ili wawe salama.
Kwa upande wake, Mohsin Bharwani mkazi wa mtaa huo amelalamikia mabasi ya Mwendokasi.
Amedai madereva wake wanatembea mwendo mkubwa na kuwa waendesha bodaboda nao hawafuati sheria, hivyo kuchangia ajali zinazoua na kujeruhi watu wengi.
“Sisi wananchi wa eneo hili tuko tayari kuchangia kama kuna ufinyu wa bajeti katika kuweka taa, kwa sababu tunapoteza nguvukazi yetu kila kukicha,” amesema Bharwani.
Naye Ally Kipepe anayefanya shughuli zake eneo hilo amesema umakini unahitajika kuanzia waendesha mabasi ya Mwendokasi kutokana na eneo hilo kuwa na watu wengi.
Mkurugenzi wa Miundombinu na Kusimamia Uendeshaji wa Mabasi yaendayo Haraka, Philemon Mzee amesema mabasi hayo yamepangiwa spidi maalumu katika maeneo ya watu wengi.
“Tulishawaambia na kuwasisitiza madereva wetu spidi isizidi 30 kwenye maeneo ya watu wengi kama Kisutu na Msimbazi wasizidishe zaidi ya hapo, japo watu tunatofautiana lakini tumeyachukua haya na tunayafanyia kazi,” amesema Mzee.
Kuhusu suala la taa, amesema watazungumza na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kwa kuwa ndio wenye dhamana na barabara hizo.
Akizungumzia mawazo yaliyotolewa kuhusu kuwekwa taa na miundombinu ili kudhibiti ajali, Mbunge wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema wamelipokea na watalifanyia kazi ikiwemo kupelekwa hadi bungeni.
“Niendelee kuwasisitiza watumiaji kama bodaboda kufuata sheria kwa sababu waliowengi hawazifuati, pia wote wafuate sheria ili kuokoa maisha yao pamoja na mali,” amesema Zungu.