Watu wasiojulikana wamuua dada wa kazi

New Content Item (1)

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Lukuyu, kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro Edmund Masamba  (anayezungumza na simu) akihojiwa  na Mwananchi Digital leo Aprili 15,2024 kuhusiana na kifo hicho.

Muktasari:

  •  Polisi wanaendelea kuchunguza chanzo cha mauaji sambamba na kuwasaka waliotekeleza mauaji hayo.

Morogoro. Watu wasiojulikana wamemuua dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Monica (22) mkazi wa Bigwa Manispaa ya Morogoro usiku wa kuamkia jana mjini hapa.

Taarifa za kuuawa kwa dada huyo zimethibitishwa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alipozungumza na Mwananchi Digital.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Hata hivyo, amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mauaji hayo bado unaendelea.

"Ni kweli tukio hilo lipo na tunaendelea na uchunguzi ili tuweze kutoa taarifa, kwa taarifa za awali zinaonyesha tukio hilo lilifanyika Aprili 14, mwaka huu, lakini taarifa zaidi tutatoa baadaye kwa sababu tunaendelea na uchunguzi,” amesema Kamanda huyo.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lukuyu, Edmund Masamba amesema taarifa za mauaji hayo alizipata jana Jumapili saa tatu usiku.

“Ni kweli kuna tukio la dada wa kazi wa Jackline Shayo ambaye alifahamika kwa jina moja la (Monica 22) amekutwa amekufa nje ya nyumba yao, nilipigiwa simu saa  tatu usiku na majirani kwamba kuna msiba wa dada wa kazi kajinyonga, baada ya kufika hapa nikakuta majirani na  mwenye nyumba (Jackline Shayo) akiwa amepaki gari lake nje huku anapiga yowe.”

Anadai baada ya kudodosa aliambiwa mama mwenye nyumba alienda Mikumi kuchukua watoto wake waliokuwa likizo.

“Kwa mujibu wake Jackline, alimpigia simu Monica Jumamosi usiku ili kujua kama kafunga vizuri milango yote, naye akamjibu kuwa amefunga. Anasema jana asubuhi akampigia simu tena kujua ameamkaje, simu yake ikawa  haipatikani mpaka alipofika nyumbani hapo saa mbili  usiku, akabisha hodi kimya, ndipo akaamua kutoka kwenye gari akakuta geti limeegeshwa,” amesimulia mwenyekiti huyo.

Amesema mama huyo alipoingia ndani akaendelea kumuita lakini hakuitika akazunguka nyuma ya nyumba ambako kuna mlango mwingine, akamkuta binti huyo amelala chini na mikono yake imefungwa kamba kwa nyuma na shingoni amefungwa shuka akiwa ameuawa tayari.

Masamba amedai  taarifa za awali walidhani alikuwa amejinyonga lakini walipofika wakabaini kuwa ameuawa na watu wasiojulikana.

Mwenyekiti huyo amesema watu hao pia waliingia chumbani kwa mwenye nyumba na kupekua na wakaondoka na televisheni ya nchi 72 na sabufa.


Jirani azungumzia mauaji hayo

Akizungumzia mauaji hayo, jirani wa Shayo, Abubakar Suleiman amesema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika mtaa wa Lukuyu, akieleza kuwa  jirani yao huyo hakuwa akiongea na mtu.

"Ni kweli tumepata msiba wa dada wa kazi kukutwa amefariki nyumbani kwa bosi wake, lakini huyo jirani yetu ana mwaka mmoja tangu ahamie hapa na hana cha rafiki wala nini, maana yeye alikua mtu wa getini na hata akitoka na gari lake alikuwa haongei na mtu wala alikua hasalimii kama wengine wanavyosalimia majirani zao.”

"Mimi baada ya kufika eneo la tukio nilikuta watu wengi wamefika yule binti alikua ameuawa na amefungwa mikono kwa nyuma, tulipomuinua ili kumuweka kwenye machela, kuna damu ilikuwa imeganda pale alipokua amelazwa, lakini hakuwa na majeraha kokote zaidi ya kufungwa mikono na shuka shingoni,” amedai Suleiman.

Jirani mwingine Geofrey Julius amesema taarifa za kifo cha Monica alizipata baada ya kufika tu nyumbani akitokea kazini.

“Nahisi wauaji huenda waliruka ukuta na inaonekana ni watu ambao wanaijua vizuri hii nyumba maana kama waliondoka na televisheni na sabufa si walikua wanajua kila kitu,” amesema Julius

Naye Grace philemon amesema,

"mimi ninamfahamu Monica kama binti wa kazi  na jirani yetu maana alikua anajituma katika kazi, na wakati wa kwenda dukani alikua akinisalimia lakini taarifa za kifo chake kiukweli zimenisikitisha sana.”

Jirani huyo ameliomba Jeshi la Polisi liwasake  wauaji hao ili sheria ichukue mkondo wake.

Severine Imanga amedai Aprili 13, 2024  alimuona binti huyo akiwa na fundi ambaye alikuwa akijenga nyumbani hapo akashangaa jana anapigiwa simu kuwa amekufa kwa kuuawa.

“Nilipigiwa simu na jirani mwenzangu akinitaka twende kwa jirani (kwa kina Monica) kuna  jambo limetokea, kwa kuwa sikuwa na mazoea ya kuingia mle ndani nikashtuka kidogo maana hatuna mawasiliano, nikashangaa, nilipofika usawa wa getini nikaingia, jirani akanipokea akaniambia nizunguke baada ya kuzunguka nikakuta dada wake wa kazi amelala amefungwa kamba mikononi na shuka shingoni, tulitoa taarifa  Polisi wakaja wakachukua mwili wakaupeleka hospitali kuhifadhiwa,” amesimulia jirani huyo.

Hata hivyo Mwananchi lilipomtafuta Shayo azungumzie tukio hilo amesema hayuko tayari kulizungumzia kwa sasa tumpe muda.

"Sina nguvu za kuzungumzia hili tukio kwa sasa naomba mniache kwanza,” amesema mama huyo.