Mwanamke auawa, mwili watupwa shambani kwao

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa.

Muktasari:

  • Tukio hilo litokea usiku wa kuamkia jana Jumatatu Julai 31, mwaka huu, ambapo inadaiwa kuwa, watu walifanya unyama huo kisha kuutupa mwili wake shambani kwao.

Moshi. Mary Mushi (30) mkazi wa kibosho Kirima, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Tukio hilo litokea usiku wa kuamkia Jumatatu Julai 31, mwaka huu, ambapo inadaiwa kuwa, watu waliofanya unyama huo walimpigia simu, usiku wa saa tatu na kisha kuondoka naye na baada ya mauaji hayo waliutupa mwili wake shambani kwao.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa leo Jumanne Agosti 1, 2023, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kuwa, wanamshikilia mtu mmoja, na kwamba uchunguzi unaendelea ili kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Kamanda amesema taarifa za awali zinaonyesha kuwa tukio hilo limesababishwa na wivu mapenzi na kwamba uchunguzi bado unaendelea.

“Ni kweli kuna tukio hilo na tunamshikilia mtu mmoja, tunaendelea kufuatilia watu wengine, lakini taarifa za awali zinaonyesha kuna viashiria vya wivu wa mapenzi,”amesema Kamanda Maigwa.

Akizungumzia tukio hilo, Rachel Mushi ambaye ni mama wa marehemu, amesema alibaini mtoto wake kuuawa baada ya watoto wa waliokuwa wakipita asubuhi kwenda shule, kuona mwili wake ukiwa umetupwa shambani.

“Watoto wa shule walisema kuna mtu amefia barabarani eneo la shambani, sasa nilipokwenda nikakuta ni mwanangu,” amesema.

Diwani wa Kata ya Kirima, Inyasi Mushi amesema kitendo hicho ni cha kinyama na kwamba wataendelea kufuatilia kuhakikisha wote waliohusika na tukio hilo wanakamatwa.

“Ni kitendo cha kinyama, mtu amekatwakatwa kama mbuzi au ng’ombe inavyokatwa kwenye mabucha, tunaahidi kufuatilia tukio hili hadi kuhakikisha waliohusika wamekamatwa,”amesema Diwani Mushi.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kirima Juu, kulikotokea tukio hilo, Thadei Mushi amesema tayari wametoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na uhalifu uliopo katika kijiji hicho na kuwataka kutoa taarifa za wageni wote wanaoingia kijijini hapo.

“Tumewaambia wananchi jinsi kijiji chetu kilivyo kwenye uhalifu na kuwataka wageni wote wanaoingia kwenye hiki kijiji, wafike kwa wenyeviti wa vitongoji na wajiorodheshe majina yao, ili na wenyeviti wa vitongoji walete kwenye ofisi ya kijiji, tujue wamekuja kwa lengo gani na wanafanya kazi gani,” amesema