Kikongwe wa miaka 92 auawa, anyofolewa macho

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe

Muktasari:

  • Kikongwe Minza Maduhu (92), mkazi wa Mtaa wa Mwakibolo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ameuawa na watu wasiojulikana ambao pia wamemnyofoa macho.

Bariadi. Kikongwe Minza Maduhu (92), mkazi wa Mtaa wa Mwakibolo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ameuawa na watu wasiojulikana ambao pia wamemnyofoa macho.

Ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye, taarifa kutoka familio ya kikongwe huyo zinaeleza kuwa mauaji hayo yalifanyika Julai 31, 2023.


Simulizi ya mjukuu

Akizungumzia kifo cha bibi yake, mjukuu wa kikongwe huyo aliyejitambulisha kwa jina la Anna Maduhu ambaye amesema aligundua kifo cha bibi yake baada ya kufika nyumbani kwake kumsaidia kazi za kawaida za nyubani ikiwemo usafi na kuandaa chakula.

"Katika mipangilio ya kazi, mimi na bibi tulikubaliana niwahi asubuhi kwa ajili ya kwenda kusaga mahindi kwa ajili ya unga wa ugali; na kwa kawaida nikifika, huwa nimwita kupitia dirishani ili anifungulie mlango. Siku hiyo nilishangaa kumwita bila majibu wala mlango kufunguliwa,’’ amesema Anna

Amesema kutokana na hali hiyo, alizungukia upande ulipo mlango na kugundua ulikuwa umefungwa kwa nje na alipoufungua akamkuta bibi yake akiwa amelala kitandani.

‘’Nilianza kumuita bila yeye kuniitikia na kwa sababu kulikuwa na mwanga hafifu niliwasha tochi ya simu kummulika ndipo nilipomwona akiwa amening’iniza kichwa kichwa uvunguni huku kitandani kukiwa na damu,’’ anasimulia mjukuu huyo

Mtoto mkubwa wa kikongwe huyo, Gulinja Mahangila amesema taarifa za hali isiyokuwa ya kawaida aliyokutwa nayo mama yake zilipomfikia alikimbia mara moja eneo la tukio na kushuhudia mwili wake ukiwa kitandani huku kichwa kikiwa kimeinamia uvunguni.

"Nilipoangalia kwa makini niliona damu ambayo tayari ilikuwa imeganda huku kukiwa na tundu kwenye eneo la jicho ndipo nikatoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa," amesema Gulinja.

Mganga mfawidhi Zahanati ya Bunamhala, Dk Praygod Charles amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha kifo ni kuvuja damu nyingi.

"Mwili umekutwa na jeraha karibu na eneo la sikio na macho yote mawili yameondolewa,’’ amesema Dk Praygod

Amesema mwili wa kikongwe huyo tayari umekabidhiwa kwa familia kwa taratibu za mazishi.

Mtendaji wa Kata ya Bunamhala, Kalimbiya Kiyumbi ameviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika katika tukio hilo huku akiiomba jamii kutoa ushirikiano kufanikisha wahusika kutiwa mbaroni.