Paroko auawa Karatu

Arusha. Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Karatu mkoani Arusha, Pamphili Nada, ameuwa kwa kupigwa na kitu kizito na mtu anayesadikiwa kuwa na matatizo ya afya akili ambaye alilazimisha kuingia kanisani kwa madai ya kutaka kusali.

Hata hivyo baada ya mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Romani Leonard (30) kufanya mauaji hayo, nae akauawa na wananchi wenye hasira.
Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo amethibitisha leo Jumatano Julai 19, 2023 kutokea mauaji hayo.

"Padri alifariki wakati anapelekwa hospitali na mtuhumiwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kupata taarifa za tukio hilo," amesema.

Wakizungumza na Mwananchi Digital baadhi ya wakazi wa Karatu wamesema mtu huyo, alikuwa akilazimisha kuingia kanisani kusali tangu usiku wa kuamkia leo, hata hivyo hakufankiwa baada ya walinzi kumzuia.

Mmoja wa wakazi hao Rehema Baha amesema hata hivyo ilipofika alfajiri mtu huyo aliendelea kupiga kelele kutaka kuingia kusali na ndipo Padri Nada alitoka nje na kumwambia mlinzi amfungulie mlango.

"Baada ya kuingia ndani (kanisani) na akiwa na Padri tu, ndipo alichukuwa chuma cha mlango na kumpiga Padri ambaye alifariki akikimbizwa hospitali," amedai

Peter Yohana anasema kutokana na tukio hilo kengere la kanisa ilipigwa na wananchi kukusanyika na baada ya kupata taarifa hizo walianza kumpiga mtu huyo na kusababisha kifo chake.

"Tunamfahamu huyu mtu anatoka Kijiji Gekum Rambo na amekuwa Karatu kwa muda sasa," amedai

Taarifa zaidi za tukio hili tutaendelea kuzitoa fuatilia gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii.