Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayosubiriwa kabla ya kuanza safari treni za SGR

Muktasari:

  • Katika ujumbe wa mwaka mpya wa 2024, Rais Samia aliagiza kuanza kwa shughuli za treni ya kisasa kabla ya Julai

Dar es Salaam. Ukiwa umesalia takribani mwezi mmoja kabla ya kuanza shughuli za treni ya kisasa ya umeme kati ya Dar es Salaam na Makutupora mkoani Dodoma, baadhi ya masuala muhimu bado hayajashughulikiwa.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa muda hadi Julai  mwaka huu treni hiyo iwe imeanza kufanya kazi.

Masuala ambayo bado hayajashughulikiwa ni kutangazwa nauli, makabidhiano ya mradi na kukamilisha ununuzi wa vichwa vya treni ya umeme (EMUs).

Katika ujumbe wa mwaka mpya wa 2024, Rais Samia aliagiza kuanza kwa shughuli za treni hiyo ya kisasa kabla ya Julai, mwaka huu ili kukidhi matarajio ya umma kuhusu mradi huo mkubwa.

Reli ya kisasa (SGR) inatekelezwa kwa awamu, ya kwanza na ya pili, kati ya Dar es Salaam na Makutupora kupitia Morogoro, ikiwa imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 95 hadi sasa.

“Nimekuwa nikisikia kuhusu mabadiliko ya tarehe za kuanza kwa huduma za treni, na watu wamechoshwa na visingizio. Wanataka kuona treni ikifanya kazi,” alisema Rais Samia katika hotuba hiyo.

Kushughulikiwa kwa mambo hayo ni muhimu ili kufanikisha uzinduzi na utendaji kazi kwa ufanisi wa mradi huo muhimu wa miundombinu ambao unaelekea kuimarisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya uchukuzi nchini.

Akizungumza na Mwananchi Digital wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) ndiyo iliyopewa mamlaka ya kutangaza nauli.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema upangaji wa nauli za treni za umeme ulikuwa karibu kukamilika.

“Kuna baadhi ya masuala ya kiufundi ambayo yanahitaji kukamilika kabla ya tangazo hilo. Hata hivyo, nauli zitakazotangazwa zina baraka za wadau wote,” amesema bila kutaja tarehe inayotarajiwa kutangazwa.

Kuhusu makabidhiano ya reli ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Makutupora, Kadogosa alisema masuala kadhaa yanahitajika kuanzishwa kabla ya makabidhiano rasmi na kuanza kazi.

“Takribani mwaka mmoja umepita tangu tuanze kufanya operesheni ya upimaji kati ya Dar es Salaam na Morogoro. Majaribio hayo yanalenga kubaini ubora wa vipengele mbalimbali katika mradi, ikiwa ni pamoja na madaraja na majengo,” amesema.

"Tunastahili kujihakikishia kuwa kuna uzingatiaji wa hali ya juu zaidi wa usalama kabla ya kuanza shughuli,” amesema akiahidi umma utajulishwa tarehe kamili ya kuanza kwa huduma hiyo.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Reli wa Latra, Hanya Mbawala alisema majaribio yaliyofanywa yalilenga kuhakikisha miundombinu ya SGR na vifaa vimethibitishwa kwa usalama wa abiria.

“Sheria ya Reli ya mwaka 2017 inatoa fursa na wajibu kwa Latra kukagua miundombinu mipya iliyojengwa na uthibitishaji wa vifaa,” amesema.

“Tumeangalia na kukagua treni, lakini tunatarajia kufanya majaribio ya mwisho Mei ambayo yatatuwezesha kuthibitisha ubora wa treni,” amesema akibainisha Latra iliiagiza TRC kushughulikia masuala machache yaliyosalia.

Amesema  TRC imeagizwa kuwasiliana na mkandarasi wa njia ya reli na wasambazaji wa mabehewa ili kufanya marekebisho au maboresho ambayo ni utaratibu wa kawaida kabla ya kufanya uthibitisho wa mwisho.

“Ni mchakato unaohitaji ukaguzi kadhaa wa vipengele vya kiufundi,” amesema.

Alisema huduma hiyo itatumia tiketi za kielektroniki, hivyo itawaepusha wananchi na usumbufu usio wa lazima.

Kuhusu treni za umeme, TRC ilitangaza mwezi uliopita kupitia taarifa kuwasili kwa seti ya awali ya vichwa vitano vya umeme na mabehewa ya abiria ambayo yanatoa taswira ya mustakabali wa usafirishaji wa abiria nchini Tanzania.

Treni hizi za kisasa zilinunuliwa kutoka Hyundai Rotem nchini Korea Kusini, na kila treni ikiwa na uwezo wa kuchukua hadi abiria 589.

TRC inasema wanatarajia kupokea jumla ya seti 10 za vichwa vya treni za EMU, na vilivyosalia vinatarajiwa kuwasili kila mwezi hadi Oktoba 2024.

Shirika hilo linasema mabebwa 65 ya abiria na vichwa tisa vya treni za umeme vimepokewa.

Mapema mwaka huu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alisisitiza kwamba ukomo wa muda uliowekwa hadi kuzinduliwa rasmi kwa treni ya umeme utafikiwa.

“Hakutakuwa na maagizo mengine. Hakuna mabadiliko yanayopaswa kutarajiwa baada ya agizo la hivi karibuni la mkuu wa nchi,” amesema.

Treni za umeme za SGR zinatarajiwa kupunguza muda wa usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma hadi takriban saa nne kutoka safari ya sasa ya saa nane kwa basi na saa 10 kwa treni kwenye reli ya zamani.

Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 hadi Novemba mwaka jana ulifikia asilimia 98, huku ule wa kilometa 442 kutoka Morogoro hadi Makutupora ukiwa ni asilimia 94.