Zanzibar yafuta gwaride sherehe za Mapinduzi

Muktasari:

  • Zanzibar inatarajia kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu Januari 12, 2023 ambapo kawaida kilele cha maadhimisho hayo huambatana na gwaride katika uwanja wa Amaan, Zanzibari.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hakutakuwepo na hafla ya gwaride la kilele cha sherehe za miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

  

Kilele cha maadhimisho hayo hufanyika Januari 12 ya kila mwaka kuadimisha Mapinduzi Matukufu Zanzibar ambapo sherehe hizo kwa kawaida hufanyika katika uwanja wa Amaan, Zanzibar.


Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habara leo Jumamosi Desemba 31, 2022, Dk Mwinyi amesema fedha zilizotakiwa kutumika kwenye kilele cha maadhimisho hayo zitakwenda kwenye miradi ya maendeleo sekta ya elimu.


Amesema: “Huwa tunakuwa na gwaride kwenye uwanja wa Amaan, safari hii halitakuwepo, sababu kuu ni mbili; ya kwanza, tumeona kama serikali tujipange kuadhimisha jambo kubwa zaidi kwa mwaka ujao ambapo mapinduzi yetu yatatimiza miaka 60,” amesema


Dk Mwinyi amesema kuwa sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi zitakuwa kubwa, hivyo zinahitaji muda wa maandalizi.


“Sherehe za miaka 60 zitakuwa kubwa zaidi, zitakuwa na mambo mengi zaidi kuliko kawaida, kwa maana hiyo Serikali itajipanga ili kutimiza maadhimisho hayo ya miaka 60 katika mwaka ujao,” amesema na kuongeza


“Kwa mwaka huu kuna skuli nyingi tunazifungua, tumeamua kama serikali Kupeleka fedha zilizokuwa zimepangwa kwaajili ya kilele cha Mapinduzi mwaka huu katika sekta ya elimu ili skuli zetu ziwe na vifaa vya kutosha. Hiyo Ndio sababu ya pili” amebainisha.


Akizungumzia kiasi kilichokuwa kimetengwa kwaajili ya kilele hicho, Dk Mwinyi amesema kuwa Sh450 milioni zilitengwa kwa ajili ya kilele cha maadhimisho hayo ambazo zitaelekezwa kwenye sekta ya elimu.


“Awali fedha zilizopangwa kwaajili ya maadhiumisho hayo zilikuwa Sh700 milioni, lakini tuliona ni nyingi tukafanya vikao mbalimbali kujaribu kuzipunguza na hatimaye zikaishia kwenye Sh450 milioni na ndizo ambazo tutazipeleka kwenye sekta ya elimu,” amesema Rais Mwinyi.


Kilele cha sherehe za Mapinduzi Matukufu Zanzibar hufanyika kila mwaka Januari 12, ambapo Januari 12, 2023 Zanzibar itaadhimisha miaka 59 ya mapinduzi hayo.

Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ilifuta hafla ya kitaifa na gwaride la maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika za mwaka huu zilizokuwa zifanyike Desemba 9, 2022.


Akitangaza uamuzi huo wa Serikali Desemba 5, 2022, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene alisema Sh960 milioni zilizotakiwa kutumika kwenye maadhimisho hayo zitakwenda kwenye ujenzi wa mabweni ya shule zenye uhitaji maalum.


Kutokana na kufutwa kwa garidi hiulo, maadhimisho ya Uhuru mwaka huu yalifanyika katika ngazi ya wilaya kwa kufanya midahalo na makongamano ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijamii.