10 wadakwa kwa tuhuma za utapeli wa ajira, biashara Mwanza
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake leo Jumamosi Julai 18, 2026 mkoani Mwanza.
Muktasari:
- Watuhumiwa hao walikamatwa Julai 16, 2026, saa 4:30 asubuhi katika Mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, kufuatia taarifa zilizotolewa na wananchi.
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata watu 10 wanaodaiwa kujihusisha na makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu na utapeli kwa kutumia ahadi za ajira na fursa za biashara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema hayo leo Jumapili Julai 19, 2026 ofisini kwake jijini Mwanza.
Kamanda Mutafungwa amesema watuhumiwa hao walikamatwa Julai 16, 2026, saa 4:30 asubuhi katika Mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, kufuatia taarifa zilizotolewa na wananchi.
Amesema uchunguzi wa awali unaonesha kikundi hicho kilikuwa kikishawishi wananchi kutoka mikoa mbalimbali, ikiwamo Geita, Kigoma, Tabora na Morogoro kwenda Mwanza kwa madai ya kupewa ajira na fursa za biashara kupitia Kampuni ya Alliance in Motion Global.
Amewataja waliokamatwa ni Adhumani Hamis (29), anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo, Emmanuel Manyau (27), Avison Mwemezi (23), Justine Joseph (23), Stephano Laurent (23), Tinalile Andrew (23), Fraison Lufungulo (24), Happyness Henry (23), Peter Kiyombi (54) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma Kati, Andriano Ngodoki (40).
Mutafungwa amesema baada ya kufika Mwanza, waathirika walitakiwa kulipa fedha kwa madai ya kujisajili na kupewa mfumo wa kuanzisha biashara, lakini wengi wao hawakupata huduma walizoahidiwa.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao mzima wa uhalifu huo na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika.
"Uchunguzi ukikamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika," amesema.
Kamanda huyo amewataka wananchi kuwa waangalifu wanapoahidiwa ajira au fursa za biashara zinazowataka kulipa fedha kabla ya kupata huduma, akisisitiza umuhimu wa kuhakiki uhalali wa kampuni au taasisi husika kabla ya kujiunga nazo.
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumshambulia na kumjeruhi mkazi wa Kijiji cha Kisamba, Wilaya ya Magu, wakimtuhumu kujihusisha na vitendo vya ushirikina.
Mutafungwa amesema Julai 17, 2026, saa 8:00 usiku, Mihayo Budaga (78), mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Nyambono, alivamiwa nyumbani kwake na watu waliovunja mlango kabla ya kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali kichwani upande wa kulia.
Kutokana na shambulio hilo, Budaga alipoteza damu nyingi na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa matibabu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kutokana na hali yake kuwa mbaya.
"Kwa sasa anaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari," amesema Mutafungwa.
Amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina na madai ya kulipiza kisasi, watuhumiwa walikuwa wakimtuhumu mzee huyo kuwafanyia uchawi ndugu zao.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Lusana Kaswahili (39), fundi ujenzi na Mbizo Kaswahili (33), mkulima.
Jeshi la Polisi limeonya wananchi dhidi ya tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa madai ya ushirikina au visasi, likisisitiza kuwa vitendo hivyo ni makosa ya jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika mara uchunguzi utakapokamilika.