Prime
Vigingi kukabili utapeli mtandaoni-2
Muktasari:
- Mabadiliko ya teknolojia yamekuwa yakiambatana na mabadiliko ya mbinu za kihalifu, jambo linalohitaji mikakati ya kisasa zaidi ya kukabiliana nayo.
Dar es Salaam. Uwepo wa mawakala wa laini za simu wanaotumia taarifa za wananchi vibaya na kuwa chanzo cha kuchochea utapeli mtandaoni umeibua hoja ya kuwapo kwa udhaifu katika usimamizi wa sheria.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, licha ya kampeni za uelimishaji na operesheni za mara kwa mara zinazofanywa na vyombo vya dola, baadhi ya mawakala wasio waadilifu hutumia taarifa za wananchi kusajili laini za ziada ambazo hutumika katika utapeli wa mtandao wa simu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sura ya 443, Kifungu cha 12(1), mtu yeyote anayefanya udanganyifu kwa kutumia mfumo wa kompyuta, mtandao au kifaa cha kielektroniki kwa lengo la kujipatia faida au kumsababishia mwingine hasara ya mali, fedha au haki yoyote anatenda kosa la utapeli wa mtandaoni.
Makosa hayo yanajumuisha kutuma ujumbe wa uongo kwa njia ya SMS au WhatsApp kuomba fedha, kujifanya taasisi za fedha au kampuni za simu, kuomba taarifa za siri za kifedha, kutumia viunganishi bandia, pamoja na matangazo ya uwekezaji hewa, mikopo feki na ajira za uongo.
Vilevile, matumizi ya taarifa za watu kusajili laini bila ridhaa yao yanaweza kuangukia pia chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, ambayo inakataza ukusanyaji au matumizi ya taarifa binafsi bila idhini ya mhusika.
Uchunguzi wa Mwananchi unaonesha kuwa changamoto kubwa si tu uwepo wa wahalifu hao, bali pia ukimya wa baadhi ya wananchi wanaofahamu shughuli zao lakini hawatoi taarifa kwa mamlaka husika.
Kwa mujibu wa wakazi wa Ifakara, wilayani Kilombero, na mjini Morogoro, baadhi ya watuhumiwa wa utapeli mtandaoni ni ndugu, jamaa au marafiki wa jamii inayowazunguka.
“Wapo wanaojulikana, lakini si rahisi mtu kutoa taarifa kwa sababu ni watu wanaofahamika katika maeneo haya tunayoishi. Wengine wanaona fedha wanazopata zinaongeza mzunguko wa biashara katika maeneo yao, hivyo wanaamua kukaa kimya,” anasema Issa Abdalla, mkazi wa Morogoro mjini.
Kwa upande wake, mkazi wa Ifakara, James Fidelis, anasema baadhi ya watuhumiwa huweka akiba ya fedha kwa ajili ya matumizi ya dharura pindi wanaposikia taarifa za operesheni za polisi.
“Wengi wao wanafahamu kuwa wanafanya kosa, hivyo hujiandaa kukimbia au kujificha wanapopata taarifa za uwepo wa operesheni za kiusalama,” anasema.
Mtazamo wa mwanasheria
Akizungumza na Mwananchi, wakili Khamis Masoud anasema, licha ya Jeshi la Polisi kuendelea kuwakamata watuhumiwa wa uhalifu wa mtandaoni, hali hiyo inaonesha kuwa kukamata pekee hakutoshi ikiwa hakutakwenda sambamba na kuimarisha uwezo wa taasisi za usalama kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu wa kidijitali.
“Kwa maoni yangu, changamoto ni upungufu wa wataalamu waliobobea katika masuala ya teknolojia ndani ya vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi. Kadiri matumizi ya Akili Unde (AI), mitandao ya kijamii na mifumo ya kidijitali yanavyozidi kuongezeka, ndivyo wahalifu wanavyobuni mbinu mpya za kuwalaghai wananchi.
"Ili kukabiliana na hali hiyo, ni lazima taasisi za usalama ziwe na wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika uchunguzi wa kidijitali na matumizi ya teknolojia za kisasa,” anashauri.
Anasema uwepo wa akaunti feki mitandaoni, pamoja na wahalifu kutumia akaunti hizo kujifanya watu au taasisi halali na kuwashawishi wananchi kutoa fedha au taarifa zao binafsi, unaonesha kuwa mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandaoni yanahitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika teknolojia na mafunzo kwa askari na wachunguzi.
Vilevile, anasema nchi inahitaji kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa sheria za teknolojia na uhalifu wa mtandao.
“Wanasheria, waendesha mashtaka na wachunguzi wanapaswa kupewa mafunzo yanayoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ili waweze kusimamia kesi hizi kwa ufanisi,” anasema.
Kuhusu usimamizi wa sheria, anasema: “Naona bado kuna maswali mengi kutoka kwa wananchi. Mara nyingi tunasikia taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa wa utapeli wa mtandaoni, lakini baadaye umma haupewi taarifa kuhusu mwenendo wa kesi hizo mahakamani au hukumu zilizotolewa. Ukosefu wa taarifa hizi unaweza kuwafanya wananchi kuamini kuwa wahalifu hawaadhibiwi ipasavyo.”
Anasema ni muhimu mamlaka husika zikaweka utaratibu wa kutoa taarifa kuhusu hatua zinazofikiwa katika kesi kubwa za uhalifu wa mtandaoni ili kuongeza uwazi na kuonesha kuwa sheria inafanya kazi, huku adhabu zinazotolewa zikiwa fundisho kwa wengine wanaokusudia kufanya uhalifu huo.
Mbali na hayo, anasema ipo haja ya kuimarisha usimamizi wa usajili wa laini za simu.
“Lengo la kuunganisha laini na taarifa za vitambulisho vya Taifa (Nida) lilikuwa kurahisisha utambuzi wa wahalifu. Hata hivyo, bado zipo taarifa za matumizi ya laini zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine, jambo linalowapa nafasi wahalifu kuficha utambulisho wao,” anasema.
Uimarishaji wa ufuatiliaji
Ikizungumzia hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema inaendelea kufanya ukaguzi wa usajili wa laini za simu, pamoja na kutumia mfumo wa ufuatiliaji unaopokea na kuchambua taarifa za usajili kutoka kwa watoa huduma wote wa mawasiliano.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TCRA, Rolf Kibaja, anasema mamlaka hiyo huchukua hatua za udhibiti pale inapobaini ukiukwaji wa sheria au kanuni za usajili wa laini za simu.
“Pale inapobainika taratibu za usajili hazikuzingatiwa, hatua za kisheria na kiudhibiti huchukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023,” anasema.
Anasema TCRA inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwezesha upatikanaji wa taarifa zinazohitajika kwa ajili ya uchunguzi na utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya dola.
Mbali na hatua hizo, TCRA imesema imeanzisha mifumo mbalimbali ya kuwasaidia wananchi kujilinda dhidi ya ulaghai wa simu.
Kibaja anasema matumizi ya namba maalumu 100 yamewezesha wateja kuwasiliana moja kwa moja na watoa huduma wao bila kutumia namba za kawaida zinazoweza kutumiwa vibaya na matapeli.
Vilevile, anaeleza kuwa wananchi wanaweza kutumia huduma ya *106# kuangalia laini zote zilizosajiliwa kwa kitambulisho chao.
Anasema akibaini namba asiyoitambua, mteja anashauriwa kuwasiliana na mtoa huduma husika kwa ajili ya kuifuta au kuchukua hatua stahiki.
Pia, namba 15040 imewekwa mahsusi kwa ajili ya kuripoti namba za simu zinazohusishwa na uhalifu wa mtandaoni na vitendo vya ulaghai.
Umuhimu wa elimu
Akizungumza na Mwananchi, msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, anasema mabadiliko ya teknolojia yamekuwa yakiambatana na mabadiliko ya mbinu za kihalifu, jambo linalohitaji mikakati ya kisasa zaidi ya kukabiliana nayo.
Anasema baadhi ya wananchi bado hukumbwa na utapeli kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu mbinu zinazotumiwa na wahalifu, kushindwa kuthibitisha taarifa wanazopokea au kuchukua uamuzi kwa haraka bila kufanya uhakiki.
“Baadhi ya wananchi hawatafuti ushauri wala kuthibitisha ukweli wa taarifa wanazopewa kabla ya kufanya uamuzi. Pia, matukio mengi hayaripotiwi mapema, jambo linalowapa wahalifu nafasi ya kuendelea na vitendo vyao,” anasema.
Kwa mujibu wa Misime, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia falsafa ya Polisi Jamii, kuimarisha mafunzo kwa askari wa uchunguzi wa makosa ya mtandao, pamoja na kupanua huduma za uchunguzi wa makosa hayo katika kanda mbalimbali nchini.
Anasema juhudi nyingine zinahusisha ununuzi wa vifaa vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia ili kubaini, kuzuia na kuchunguza kwa haraka matukio ya uhalifu wa mtandaoni.
“Hatua muhimu zaidi kwa wananchi ni kutambua kuwa uhalifu huu upo, kuwa waangalifu, kutafuta taarifa sahihi kabla ya kutuma fedha na kuepuka kufanya uamuzi kwa haraka au kutokana na tamaa,” anasema.
Mapendekezo ya wadau
Mchumi anayejikita katika uchumi wa kidijitali, Francis Nyonzo, anasema utapeli wa simu unaweza kudhoofisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Anashauri kuwe na ushirikiano mkubwa zaidi kati ya kampuni za simu, taasisi za fedha na vyombo vya dola ili kufuatilia fedha zinazopokewa kupitia namba zinazohusishwa na matukio ya ulaghai.
Kwa upande wake, mchumi Oscar Mkude anasema sehemu kubwa ya utapeli huo inaweza kuzuilika iwapo watumiaji wa huduma za kifedha wataongeza umakini kabla ya kutuma fedha.
“Wananchi wanapaswa kuthibitisha taarifa wanazopokea kabla ya kufanya miamala. Kupiga simu kwa mhusika anayehusika na muamala kunaweza kuzuia hasara zinazotokana na ujumbe wa kitapeli,” anasema.
Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, anasema kuendelea kwa matukio ya utapeli kunaweza kurudisha nyuma jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali ikiwa wananchi watapoteza imani katika matumizi ya simu na mifumo ya malipo ya kielektroniki.
Anapendekeza matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa za kutambua mapema ujumbe wenye viashiria vya ulaghai, ikiwamo mifumo inayotumia Akili Unde na uchambuzi wa data kubaini ujumbe unaofanana na ule unaotumiwa na wahalifu.