61 wanapata kipindupindu Sengerema

Muktasari:

  • Kata  zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa kipindupindu  ni Chifunfu na  Kasenyi zilizoko  pembezoni mwa ziwa Victoria ambako wakazi wa maeneo hayo ni wavuvi.

Sengerema. Watu 61 wameripotiwa kuugua    ugonjwa wa Kipindupindu wilayani Sengerema mkoani  Mwanza kuanzia Januari 30, 2024 hadi Februari 2, 2002 mwaka huu.

Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga amesema wagonjwa wamelazwa kwenye vituo mbalimbali wakiendelea kupatiwa matibabu.

Nganga amevitaja vituo vya afya ambako wagonjwa hao wamelazwa kuwa ni kituo cha afya Ngoma Mtimba kilichopo kata ya Chifunfu, Kituo cha afya Katunguru kilichopo kata ya Katunguru, Kituo cha afya Project kilichopo kata ya Nyatukala na Hospitali teule ya wilaya ya Sengerema (DDH).

Kufuatia hatua hiyo Nganga amewaka watendaji wa vijiji, kata, madiwani na wananchi kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo.

"Tayari timu ya afya kutoka Mkoa wa Mwanza wakishirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Sengerema wamepiga kambi wilayani hapa  kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo,” amesema Ngaga.

Aidha wakati wa kikao cha baraza la Madiwani la Halmashauri ya Sengerema la kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2024/ 2025 wajumbe waliweka mikakati ya kupambana na hali hiyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chifunfu, Denis Dominic amesema timu ya afya inatakiwa kupiga kambi kijijini hapo ili kudhibiti hali hiyo.

Diwani wa Kata ya Nyamazugo, Enock Sengerema amewaomba wataalamu wa afya kuweka nguvu kwenye maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo, ili waudhibiti usisambae kwenye maeneo mengine.