Abiria asiyevaa barakoa Dar kushushwa

Abiria asiyevaa barakoa Dar kushushwa

Muktasari:

  • Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam imetangaza rasmi kuanza kuwashusha abiria wote ambao wataonekana ndani ya vyombo vya usafiri wa umma bila kuvaa barakoa ikiwa katika kupambana na maambukizi ya kasi ya virusi vya Covid-19.



Dar es Salaam. Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam imetangaza rasmi kuanza kuwashusha abiria wote ambao wataonekana ndani ya vyombo vya usafiri wa umma bila kuvaa barakoa ikiwa katika kupambana na maambukizi ya virusi vya Covid-19.

Vyombo vilivyotajwa ni pamoja na daladala, mabasi ya mwendokasi, mabasi yaendayo mikoani, vivuko vya majini ‘pantoni’.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Agosti 12, 2021 katika mdahalo wa kitaifa kuhusu Covid-19 unaoendelea kufanyika hivi sasa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere JNICC.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija amesema zoezi hilo litafanyika kwa kufanya ukaguzi.

“Abiria ambao watakuwa hawajavaa barakoa tutasimamisha gari na kuwashusha , maagizo yalishatolewa na uelimishaji umefanyika kwa kipindi kirefu kinachotakiwa sasa kila mtu achukue tahadhari".


“Kumekuwa na upotoshaji mwingi katika suala la chanjo na kujikinga lakini tunashukuru mwitikio ni mkubwa, wananchi wameendelea kupokea chanjo imeleta fursa tuna vituo vingi vya kutosha kwenye hospitali zetu waepukane na upotoshaji unaofanyika...

“Afya ni yako mwenyewe, heri kinga kuliko tiba watu wamepata changamoto hizi na zinapojitokeza zinazuia uzalishaji mali,” amesema Makalla.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Dk Ntuli Kapologwe amesema mapambano yaliyopo sasa nchini ni namna ya kupambana na upotoshaji wa taarifa za chanjo ya ugonjwa huo.

“Mapambano tuliyonayo sasa ni dhidi ya upotoshaji katika ugonjwa huu, lakini lazima tuangalie chanjo pekee haitoshelezi lazima tujikinge kwa kunawa, kutakasa mikono na kunawa kwa maji tiririka na sabuni lakini pia tukikaa umbali wa mita moja,” amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Fatma Mrisho amesema ni wakati sasa kila mmoja kuhakikisha anaungana na nguvu za viongozi kukinga na kutokomeza ugonjwa huo kwa kufuata kanuni za afya na kuchanja.

Imeandikwa na Herieth Makwetta na Rukia Kiswamba, Mwananchi [email protected]