Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Abiria wa mabasi Kilimanjaro Express wakwama Moshi, Dar

Abiria waliokwama wakiwa kituoni mjini Moshi

Muktasari:

  • Siku mbili baada ya Latra kusimamisha leseni ya kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro Express, abiria waliokuwa wamekata tiketi za safari, leo wamekwama mkoani Kilimanjaro na Dar es Salaam na kuzua malalamiko.

Moshi. Mamia ya abiria waliokuwa wakisafiri na mabasi ya Kilimanjaro Express kutoka Moshi kwenda mikoa mbalimbali nchini, wamekwama katika ofisi za mabasi hayo zilizopo mkoani Kilimanjaro baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kuyafungia kutoa huduma kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni.

Abiria hao walifika tangu saa 11 alfajiri katika ofisi hizo lakini mpaka muda waliozungumza na Mwananchi saa 4 asubuhi walikuwa wamekwama, wakiomba Latra kuwasaidia ili warejeshewe nauli zao.

Juhudi za kuupata uongozi wa kampuni hiyo, akiwamo Meneja wa kampuni hiyo anayetambulika kwa jina moja la Ester, hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita muda mrefu bila kupokelewa.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika katika ofisi ya kampuni hiyo mjini Moshi ameshuhudia abiria waliokuwa wakishinikiza uongozi wa kampuni hiyo kurejesha nauli zao na kujua hatma za safari zao, wakikosa majibu baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kujifungia ndani.

Januari 6, mwaka huu Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo aliyasimamisha magari yote ya kampuni hiyo kutoa huduma za usafirishaji baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika stendi ya mabasi ya Magufuli na ofisi zao zilizopo Shekilango jijini Dar es Salaam akidai kukiukwa kwa masharti ya leseni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti abira hao ambao baadhi  ni wagonjwa na wengine ni wanafunzi, wamesema tangu Januari 6 walikata tiketi na hawakuelezwa kama kuna changamoto zozote za usafiri na hata walipofika leo hakuna chochote walichoelezwa.

Reward Shelukindo, mmoja wa abiria aliyekwama katika ofisi hizo, amesema tangu asubuhi saa 11 alfajiri yupo kwenye ofisi hizo na kwamba hajui hatma yake ya kusafiri licha kwamba ana mgonjwa ambaye anatakiwa kuwepo Dar es salaam leo.

"Tupo hapa tangu saa 11 alfajiri, hakuna tunachoelezwa kuhusu kusafiri, hapa nilipo mke wangu anakwenda kliniki na anatakiwa awepo Dar es Salaam jioni leo.

"Tunachotaka waturejeshee nauli zetu, tutafute usafiri mwingine, maana hakuna wanachotumbia hapa zaidi ya kutuchosha, wengine wapo wapo na watoto tangu asubuhi na wamekaa tuu hapa," amesema Shelukindo.

Kwa upande wake Efrasia Festo, mmoja wa abiria anayesafiri kwenda Dar es Salaam amesema tangu saa 12 asubuhi yupo na watoto na hawajui kama wanasafiri au la.

"Nimekaa na watoto hapa tangu alfajiri, mpaka sasa hatujapata usafiri na hatujui hatma ya kusafiri, kama Kuna changamoto basi wangetueleza ili tusikate tiketi, kwa nini walichukua fedha zetu na hawatuambii chochote, waturudishie fedha zetu," amesema abiria huyo.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Nyello amesema kwa sasa wanaangalia ya abiria hao kutafutiwa usafiri mwingine ama warejeshewe nauli zao ili waendelee na safari.

"Baada ya zuio hili kampuni ilipaswa kuanzia leo Januari 8 isitoe huduma lakini mpaka jana na leo ameendelea kukata tiketi ilhali wanajua amefungiwa kutoa huduma hizo, hivyo tumeongea nao pamoja na mambo mengine wasitishe hizi huduma maana wanaleta adha kwa wasafiri," amesema Paulo.


Dar es Salaam

Kwa upande wa Dar es Salaam, baadhi ya abiria wa mabasi hayo waliokuwa wamekata tiketi wamerudishiwa fedha zao na kutafuta usafiri mwingine.

"Nilikata tiketi kwa ajili ya kuanza safari kwenda mkoani lakini nimerudishiwa nauli inaniumiza nilitakiwa kuwahi kazini nimeshapotezewa muda," Saimon Akaro

Akaro amerudishiwa sh 42000 aliyotoa na alitakiwa awe ameshaondoka toka asubuhi kwenda Arusha kumpeleka mdogo wake shuleni.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Joyce Minja aliyerudishiwa nauli yake baada ya basi hilo kuzuiwa kuondoka hadi pale litakapotekeleza kanuni zilizowekwa.

"Tumepotezewa muda unajua sahizi hatuwezi kupata basi makampuni mengine yamesatoka na Arusha ni mbali nimeingizwa gharama nyingine na kuharibu mipango yangu," amesema.

Wakati abiria wengine wakirejeshewa nauli zao, baadhi ya abiria wamelalamika kukatishiwa nauli na kukosa usafiri asubuhi ya leo.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika katika ofisi zao zilizopo kituo cha mabasi cha Magufuli na kituo cha Shekilango jijini hapa ameshuhudia ofisi zao zikiendelea na kazi za kukatisha tiketi za kawaida.

"Tangu jana tulikuwa tunakaribishwa hapa kukata tiketi na ealituhakikishia safari zipo tumefika hapa alfajiri tunaambiwa safari hakuna kwanini hawakutuambia toka ile jana," amesema Lazaro Tarimo.

Amesema kampuni hiyo kama ilikuwa inajua ipo kwenye adhabu ilipaswa kutumia busara kuheshimu mamlaka badala ya kuendelea kuwatesa abiria wanahitaji kusafiri kuwahi majukumu mengine ya kimaendeleo.

"Nimejikuta nikiwa kwenye matatizo niliondoka kazini sikuaga lengo langu nije mara moja lakini hali imekuwa tofauti hali kama mnavyoona sijuhi itakuwaje," amesema.

Naye Magreth Charles ameitupia lawama Latra kama walitoa adhabu hiyo walipaswa kuweka utepe ofisi za kampuni hiyo lakini kitendo cha kuacha watu wamekata tiketi na mipango yao ilikuwa waondoke sasa wanasitisha safari.

"Hatuelewi tunaweza kufanya jambo gani? Makosa ya mtoa huduma shida tunakuja kupata tunahitaji huduma Latra wamekosa umakini," amesema

Hata hivyo, Ofisa Mawasiliano kutoka Latra, Salum Pazi amesema maofisa hao pamoja na Jeshi la Polisi walitembelea kwenye ofisi za kampuni hiyo kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.

"Tumekuja katika ofisi hizi kuhakikisha kampuni inatekeleza agizo lilitolewa na kikubwa tutakuwa tayari kuruhusu shughuli ziendelee baada ya kutekeleza maagizo yaliyopo na yaliyomfanya kusitishiwa huduma,” amesema.

Mwananchi ilimtafuta Meneja wa Kampuni hiyo kuzungumzia sakata hilo ambaye hakuwa tayari kutaja majina yake amesema, "Siwezi kuzungumza jambo lolote mnataka kutuaharibia biashara yetu."

Hata hivyo, Pazi amesema Mmiliki wa Kampuni hiyo anatarajiwa kwenda kufanya mazungumzo na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

"Mazungumzo yatafanyika ofisi za Latra, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam atazungumza na mmiliki wa kampuni ya Kilimanjaro," amesema Pazi