Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo kutambulisha nembo, bendera mpya ikiadhimisha miaka 10

Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama cha ACT Wazalendo, Shangwe Ayo akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2024

Muktasari:

  • ACT Wazalendo kusherehekea miaka 10 kwa kutambulisha nembo na bendera mpya.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kutambulisha nembo na bendera yake mpya, lengo likiwa ni kuzidi kukipendezesha chama hicho.

 Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 15, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Shangwe Ayo alipokuwa akieleza kufanyika kwa maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza Aprili 21, 2024 na kilele chake kufanyika Mei 5, 2024, katika viwanja vya Mwami Ruyagwa, Kata ya Gungu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.

Ayo amesema katika maadhimisho hayo zitafanyika shughuli mbalimbali hadi siku ya kilele na mojawapo ni kutambulishwa kwa nembo na bendera mpya ya chama, shughuli itakayofanyika makao makuu ya chama Magomeni, Dar es Salaam na kwa upande wa Zanzibar itafanyika ofisi za chama pale Vuga.

"Aprili 27 chama hicho kitafanya mkutano wa kidemokrasia mkoani Kilimanjaro na wanachama wa nchi nzima watakutana na Kiongozi wa Chama Doroth Semu, kujadiliana naye masuala ya chama chao.

"Katika mkutano huo wa kidemokrasia ndipo nembo na bendera mpya ya chama vitazinduliwa rasmi," amesema Ayo.

Aidha, Ayo amesema ukiacha kutambulisha bendera na nembo mpya, shughuli nyingine zitakazofanyika katika maadhimisho hayo ni pamoja na kongamano la vijana Zanzibar litakalofanyika Aprili 21.

"Katika kongamano hili vijana watajadili dhima na wa wajibu wa vijana  katika kuipigania Zanzibar mpya, Zanzibar  moja na Zanzibar yenye mamlaka kamili. Kongamano litahudhuriwa na vijana wa Zanzibar pamoja na viongozi wa kitaifa wa chama na wadau mbalimbali wa mageuzi nchini," amesema Ayo.

Shughuli nyingine ni kutoa kwa jamii ambapo wanachama pamoja na viongozi wa kitaifa wataweka kambi wilayani Rufiji kufanya huduma za kijamii kwa waathirika wa mafuriko.

Vilevile chama hicho kinatarajia kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuchangia damu katika benki ya Damu ya Taifa, kufanya usafi kwenye masoko, hospitali na kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika hospitali hizo, shughuli zitakazofanyika Tanzania Bara na Zanzibar.

Pamoja na hayo, Mei 4, 2024 kutakuwa na mkesha makao makuu ya chama  Magomeni na  ofisi Kuu za Chama Zanzibar, mkesha utakaoshuhudia kupandishwa kwa bendera mpya ya chama na Mei 5 iitakuwa kilele ambapo Mwenyekiti wa chama, Othuman Masoud Othman atapandisha rasmi bendera mpya ya chama katika mkutano mkubwa wa hadhara ambapo pia atahutubia Taifa.

"Chama kinatoa rai kwa wanachama wake, viongozi wote, wapenzi na mashabiki nchi nzima  kushiriki maadhimisho hayo kushehereka miaka 10 ya mafanikio makubwa katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi hapa nchini," amesema Ayo.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ya miaka kumi ya ACT Wazalendo ni "Miaka 10 ya kupigania maslahi ya wote na Zanzibar yenye mamlaka kamili.'