Miaka tisa ya ACT-Wazalendo kufanyika Mkuranga
Muktasari:
- ACT-Wazalendo kuadhimisha miaka tisa ya kuanzishwa kwake Mei 5 wilayani Mkuranga, chaanza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema keshokutwa chama hicho kitasherehekea miaka tisa ya kuanzishwa kwake wilayani Mkuranga, mkoani Pwani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kichama.
ACT-Wazalendo kilipata usajili wa kudumu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa mwaka Mei 5, mwaka 2014 na mwaka jana sherehe za kutimiza miaka minane ya kuanzisha kwake zilifanyika mkoani Mwanza kwa kuendesha kampeni ya kuchangia damu na kupanda miti.
Mwaka huu chama hicho kinafanya maadhimisho ya kutimiza miaka tisa katika Kata ya Mwandege, Mkuranga ambapo watahamasisha uhifadhi na ulinzi wa mazingira.
Ado ameeleza hayo leo Mei 3, 2023 katika taarifa iliyotolewa na ACT-Wazalendo kwa vyombo vya habari. Amesema kuanzia leo hadi kesho watafanya shughuli za kijamii, kupanda miti, kufanya usafi wa mazingira katika Zahanati ya Mwandege.
“Tumeamua kuyatumia maadhimisho ya miaka tisa ya ACT- Wazalendo kupanda miti ili kushiriki katika utunzaji wa mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi.
“Madhara yake yameonekana kwenye sekta mbalimbali hasa za kilimo, nishati, utalii na maji. Uzalishaji wa chakula na umeme unashuka kila mwaka kwa sababu ya uhaba wa mvua," amesema Ado.
Amesema ACT-Wazalendo wameamua kushughulika na kiini cha tatizo kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa vitendo. Amesema ofisi yake kwa ushirikiano na msemaji wa sekta wa mazingira, watakuja na mkakati maalum wa kuwahimiza viongozi wa ngazi zote, wanachama na wananchi kupanda miti na kuyatunza mazingira.