ACT-Wazalendo kuwawekea mawakili waathirika wa kamchape
Muktasari:
Vitendo vya kamchape siyo tu huambatana na vurugu, bali pia wizi, uporaji, upotevu na uharibifu wa mali. Wakati mwingine vitendo hivyo husababisha vifo kama ilivyotokea Kijiji cha Kazuramimba.
Uvinza. Chama cha ACT-Wazalendo kitawawekea mawakili wananchi wa Wilaya za Uvinza, Kasulu na Kigoma wanaokabiliwa na mashtaka yanayohusiana na matukio ya lambalamba maarufu kamchape.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumanne Novemba 21, 2023 na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe aliposimama Kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Uvinza kusalimia wananchi akiwa njiani kwenda mjini Uvinza katika ziara yake ya kichama inayoendelea katika majimbo ya Mkoa wa Kigoma.
“Nimepata taarifa ya madhira yaliyowakumba wananchi kuhusiana na matukio ya mambo ya kamchape na kwamba wapo wenzetu wanakabiliwa na mashtaka mahakamani, tayari nimeagiza mawakili wa ACT-Wazalendo waende mahakamani kuwatetea ili kuhakikisha haki inatendeka,’’ amesema Zitto
Kiongozi huyo ametoa ahadi hiyo baada ya kupokea taarifa ya matukio hayo kutoka kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Petro Ndolezi ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Uvinza.
Katika maelezo yake, Ndolezi ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania nafasi ya ubunge Kigoma Kusini katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 amesema, matumizi ya nguvu kukabiliana na matukio ya lambalamba katika wilaya za Mkoa wa Kigoma inaibua hali ya sintofahamu kati ya wananchi na mamlaka za dola, hasa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kutokana na taarifa hiyo, Zitto ameahidi kuwasiliana na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi ili kushauriana nao kuhusu namna bora ya kukabiliana na matukio ya kijamii yanayohusiana na masuala ya kiimani.
“Mimi binafsi nitakwenda kuonana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kuhusu suala hili, sisi tunaamini katika elimu kwa umma na majadiliano kutafuta ufumbuzi wa masuala ya kiimani yanayoweza kuleta madhara kwa jamii kwa sababu masuala ya kiimani yanagusa mioyo na maisha ya jamii. Kamwe hayawezi kutatuliwa kwa nguvu ya dola,’’ amesema Zitto
Matukio ya kamchape
Hivi karibuni Mkoa wa Kigoma, umeshuhudia matukio kadhaa ya kundi la watu wanaojiita Kamchape/Lambalamba wanaozunguka maeneo mbalimbali ya vijiji wakiingia kwenye makazi ya watu wakidai kutoa uchawi.
Watu hao wanaodai wanauwezo wa kutoa uchawi katika makazi ya watu, wameibua mkinzano ndani ya jamii kwa kuwepo kundi la wanaounga mkono imani hiyo huku wengine wakipinga.
Katika mlolongo wa matukio hayo, watu watatu walifariki dunia na asakri polisi wawili kujeruhiwa katika vurugu zilizotokea Kijiji cha Kazuramimba Oktoba 4, 2023.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu, watu 49 walihojiwa kuhusiana na vurugu hizo na baadhi tayari wamefikishwa mahakamani.
Septemba 12, 2023, kundi la watu wanaounga mkono imani ya lambalamba lilivamia nyumbani kwa mfanyabiashara Khalid Mwela maarufu “Osama’’ mkazi wa Kijiji cha Mahembe Wilaya ya Kigoma na kuchoma moto nyumba yake baada ya kukataa kushiriki masuala ya kamchape. Mali kadhaa ya mfanyabiashara huyo iliharibiwa katika vurugu hizo.
Wanachokifanya Kamchape
Kundi hilo wakifika maeneo husika wamekuwa wakiunda kamati ndogo inayowasaidia kuzunguka katika nyumba zote za eneo hilo, kuwapikia chakula na mambo mengine huku wananchi wa eneo hilo huchanga kiasi cha Sh5,000 kwa kila kaya na kuwapa kwaajili ya kazi hiyo.
Vitendo vya kundi hilo husababisha migogoro kwa wananchi, hasa pale wenye nyumba inayodaiwa kuwa na uchawi wanapogoma kuwaruhusu kamchape kuingia kutoa uchawi.
Vitendo vya kamchape siyo tu huambatana na vurugu, bali pia wizi, uporaji, upotevu na uharibifu wa mali. Wakati mwingine vitendo hivyo husababisha vifo kama ilivyotokea Kijiji cha Kazuramimba.