Zitto awang’ang’ania vigogo wa Serikali Kakonko kifo cha kijana Enos
Muktasari:
Kifo cha Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa maofisa wa Uhamiaji Wilaya ya Kasulu kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa katika pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kasulu. Chama cha ACT-Wazalendo kimeipongeza Serikali kwa kuchukua hatua kwa kuwashikilia maofisa Uhamiaji wanne wa Wilaya ya Kakonko kwa mahojiano kuhusika na kifo chenye utata cha kijana Enos Elias (20) waliyemshikilia kwa mahojiano kuhusu uraia wake.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe wakati akihutubia mikutano yake ya hadhara mjini Kasulu na Kijiji cha Kagerankanda wilayani humo akisema kushilia kwa maofisa hao ni ishara njema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua kutafuta ukweli na haki kuhusu kifo cha Enos ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa umezikwa porini na watu wasiojulikana.
Kifo cha Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa maofisa wa Uhamiaji Wilaya ya Kasulu kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa katika pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kabla ya kutoweka, Enos aliwapigia simu ndugu zake kuwajulisha kuwa anashikiliwa na maofisa wa Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Kakonko baada ya kutiliwa mashaka uraia wake ambapo aliomba atumiwe namba ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) ya mama yake mzazi, Juliet Joseph ili aweze kuthibitisha uraia wake.
‘’Naipongeza Serikali kwa kuwashikilia kwa mahojiana maofisa Uhamiaji waliohusika kumkamata Enos; hili lilikuwa moja kati ya maombi manne ya familia na wote wenye maenzi mema kuhusu utata wa kifo cha kijana huyu. Bado tunaiomba Serikali kutekeleza maombi mengine matatu yaliyalia,’’ amesema Zitto ambaye tayari amefika Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko kuhani msiba huo na kuipa pole familia
Ametaja maombi mengine ya familia na wapenda haki yanayotakiwa kufanyiwa kazi na Serikali kuwa ni kuwawajibisha viongozi na watendaji wakuu wa Serikali na taasisi zake wilayani Kakonko kwa kosa la kujaribu kuficha ukweli wa tukio hilo kwa njia moja au nyingine.
Akifafanua, Zitto amesema katika hatua za awali za sakata la kifo cha kijana Enos, viongozi na watendaji wa Serikali na taasisi zake wilayani Kakonko siyo tu walikana kufahamu iwapo kijana huyo alikamatwa na kulazwa mahabusu, bali pia hata kufahamu taarifa zake kila wakati ndugu walipokuwa wakifuatilia kwa takriban siku saba mfululizo kuanzia Oktoba 27, 2023 aipokamatwa hadi Novemba 3, 2023.
“Ni dhahiri DC (Mkuu wa Wilaya), OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) na Mkuu wa Uhamiaji wote walifahamu taarifa za kijana Enos kwa sababu familia iliwafikia katika jitihada za kumtafuta. Lakini hawakuonyesha ushirikiano hadi vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ilipofichua tukio hilo,’’ amesema Zitto
Ameongeza; ‘’Hawa ama wanapaswa kuwajibika au kuwajibishwa na mamlaka zao za nidhamu kwa kutowasimamia vema watumishi walio chini yao wanaliotuhumiwa kumshikilia Enos ambaye baadaye amekutwa amefariki,’’
Maelezo ya familia
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Juliet Joseph, mama mzazi wa kijana Enos amesema yeye, familia na jamii wanaamini kijana huyo amefikwa na mauti akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa vyombo na taasisi za Serikali.
Mama huyo anasema mara ya mwisho kuwasiliana na familia, Enos alikuwa mikononi mwa maofisa Uhamiaji na kuomba uchunguzi kuanzia kwa maofisa waliomkamata na kituo cha polisi Kakonko alikolala kabla ya kukabidhiwa tena kwa maofisa Uhamiaji.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Angel Elias ambaye ni dada wa Enos akisema ndiye aliyezungumza naye kwa njia ya simu Jumamosi Oktoba 28, 2023 akimtaka kumtumia namba ya kitambulisho cha mama yao ili awathibitishe uraia wake kwa maofisa Uhamiaji waliokuwa wanamshikilia.
‘’Wakati nazungumza naye, mimi na mama tulikuwa shambani; na kwa sababu namba ile ilikuwa imeandikwa kwenye karatasi ambayo ilikuwa nyumbani kwa wakati huo, ilibidi mama arejee nyumbani kuichukua lakini tulishindwa kumtumia baada ya simu yake kutopatikana hewani,’’ amesema Angel
Maiti kufukuliwa porini
Akisimulia jinsi mwili wa ndugu yake ulivyopatikana, Angel anasema baada ya kumtafuta kwenye ofisi ya Uhamiaji na Kituo cha Polisi Kakonko bila mafanikio tangu Oktoba 27, 2023 alipokamatwa, Novemba 3, 2023, familia ilipigiwa simu ikitakiwa kufika Kituo cha Polisi Kakonko na kujulishwa kuwa kuna kaburi imeonekana katika pori la Kichacha, umbali wa zaidi ya kilometa 25 kutoka Kakonko mjini.
‘’Tuliongozana na askari hadi porini na baada ya kaburi kufukuliwa na mwili kutolewa, mama aliutambua kuwa ni wa marehemu kaka Enos kutokana na alama iliyokuwa nayo kwenye meno,’’ amesema.
Anasema hadi sasa, familia inajiuliza ni kwanini maofisa Uhamiaji waliomkamata na wenzao wa Jeshi la Polisi alikohifadhiwa baada ya kukamatwa walikana kumshikilia wala kujua taarifa za Enos ambaye tayari amezikwa kwenye makaburi ya umma kijijini hapo Novemba 14, 2023.
Kamati ya RC, uchunguzi wa polisi
Kutokana na utata uliogubika kifo cha Enos Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mwanamvua Mrindoko ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi ameunda kamati ya watu sita kuchunguza sababu, mazingira na wahusika na kifo hicho.
Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Andrew Mrama ameiambia Mwananchi kuwa kamati hiyo iliyoundwa Novemba 15, 2023 inatakiwa kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake kabla au ifikapo Novemba 22, 2023 kuwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki.
Hatua ya uongizi wa mkoa kuunda kamati ya uchunguzi inaenda sambamba na uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi ambayo kwa kupitia msemaji wake, David Misime imetangaza kuanzisha uchunguzi kubaini sababu, mazingira na wahusika wa kifo cha Enos.