ACT-Wazalendo 'waitaka' Kigoma chaguzi zijazo

Mhonga Said Ruhwanya, mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo. Picha na Peter Saramba

Muktasari:

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo, Mhonga Said  Ruhwanya amewataka wakazi wa Mkoa wa Kigoma kuwachagua wanaotokana na chama hicho katika chaguzi zijazo ili waonyeshe tofauti ya kiuongozi na viongozi kutoka vyama vingine vya siasa.

Kigoma. Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo, Mhonga Said  Ruhwanya amewataka wakazi wa Mkoa wa Kigoma kuwachagua wanaotokana na chama hicho katika chaguzi zijazo ili waonyeshe tofauti ya kiuongozi na viongozi kutoka vyama vingine vya siasa.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Kigoma leo Ijumaa Desemba Mosi, 2023, Ruhwanya amewaomba  wapiga kura mkoani Kigoma kutekeleza adhma hiyo kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

"ACT-Wazalendo tumewahi kuonyesha uwezo wetu kiuongozi tulipounda na kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na ubunge wa Jimbo la Kigoma mjini lakini mipango ya maendeleo tuliyoasisi imedorora. Tunaomba wananchi mtuamini tena kwa kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa, madiwani na wabunge wa ACT-Wazalendo kuendeleze ambayo wenzetu wameshindwa," amesema Ruhwanya

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Sendwe Ibrahim ametumia mkutano huo kuwataka wanachama wa chama hicho na wana Kigoma kwa ujumla kujiandaa kwa chaguzi zijazo kwa kujiandikisha wakati wa kurekebisha daktari la wapigakura ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Hoja ya kuwaondoa madarakani viongozi na wawakilishi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  imeungwa mkono na Waziri Kivuli wa Uchukuzi wa ACT-Wazalendo, Kiza Mayeye akisema chama hicho tawala kimeshindwa kushughulikia na kutatua matatizo ya wananchi.

"Serikali ya CCM inadai kuwa huduma za afya kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano inatolewa bila malipo; lakini kiuhalisia huduma hizo zinalipiwa na ndio maana utawaona wajawazito wakibeba vifaa wanapoenda kujifungua," amesema Kiza

Waziri Kivuli huyo amegusia pia suala la fedha za mfuko wa Tasaf akiishauri Serikali kubadilisha mfumo wa sasa wa wanufaika kulazimika kufanya kazi kwenye miradi ya maendeleo kama masharti ya kupata fedha.

"Wengi wa wanufaika wa fedha za Tasaf ni wazee ambao baadhi yao ni wastaafu kiumri, siyo sahihi kuwafanyisha kazi ya kuchimba barabara, mitaro au kusomba mawe na matofali kwenye miradi ya maendeleo," amesema Kiza